21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 4, 2022

WATOTO WASIO NA NJIA YA HAJA KUBWA WAONGEZEKA MUHIMBILI

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM                |


IMEELEZWA kuwa asilimia 30 hadi 40 ya watoto waliozaliwa na matatizo mbalimbali ambao hufikishwa katika Idara ya Upasuaji ya Watoto iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili, hawana njia ya haja kubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo jana kuhusu kambi ya upasuaji waliyofanya Julai 26 na 27, mwaka huu kwa kushirikiana na wenzao wa Chuo Kikuu cha Alexandria cha Cairo, Misri, Daktari Bingwa wa Upasuaji Watoto wa Muhimbili, Mwajabu Mbaga, alisema idadi hiyo ni kubwa.

“Kwa siku mbili mfululizo tumekuwa na jopo la watalaamu wenzetu 10 wa upasuaji kutoka Misri wakiongozwa na Profesa Saber Mohamed Waheeb ambaye ni Mshauri Mwelekezi katika upasuaji wa watoto na Dk. Mohamed Abdelmalak Morsi bingwa wa upasuaji wa watoto.

“Tumeshirikiana nao kufanya upasuaji wa watoto 24 kwa siku mbili katika upasuaji mgumu (difficult cases), kati ya watoto hao wengi walikuwa ni wenye tatizo la kukosa njia ya haja kubwa.

“Wapo ambao wanasumbuliwa na matatizo ya saratani na figo zao zilikuwa na matatizo, tumewafanyia upasuaji pia watoto wote wanaendelea vizuri bado wapo wodini tukifuatilia kwa ukaribu hali zao,” alisema.

Aliongeza:”Matatizo ya kuzaliwa nayo kitaalamu tunayaita ‘congenital disease’, hakuna sababu maalumu zinazosababisha kutokea lakini kuna vitu vingi huchangia tangu mimba ilipoingia, sababu nyingine hutoka kwa mama au kwa mtoto mwenyewe.

Naye Daktari Bingwa wa Upasuaji Watoto wa Muhimbili, Petronila Ngiloi, alisema changamoto kubwa iliyopo ni jinsi ya kuwapata watoto wenye tatizo hilo ili wapatiwe matibabu mapema.

“Utaona hata takwimu hiyo tuliyonayo ni ya hospitali pekee na si Tanzania nzima, ukihitaji takwimu kamili inabidi tufanye utafiti zaidi tujue, lakini tunaona wengi tunaowapokea hapa wanakabiliwa na tatizo hilo kuliko matatizo mengine.

“Changamoto ni kwamba, hufikishwa wakiwa muda umekwenda, jamii haina uelewa wa kutosha kuhusu tatizo hili,” alisema.

Awali akizungumza, Profesa Waheeb, alishauri kufanyiwa maboresho zaidi katika kitengo hicho hasa eneo la Chumba cha Uangalizi Maalumu kwa Watoto Wachanga (NICU) pamoja na Chumba cha Uangalizi Watoto Wakubwa (PICU).

“Tumekuwa na ushirikiano kwa muda mrefu sasa, tunajivunia kuendelea kushirikiana na Muhimbili kitengo hiki cha watoto katika kusaidia jamii,” alisema.

Alisema ushirikiano huo umeimarishwa zaidi na makubaliano ya ushirikiano yaliyowekwa na nchi hizi mbili kupitia balozi zake.

“Tunashauri mzidi kuimarisha kitengo hiki na kuendelea kuwapa mafunzo wataalamu ili wazidi kutoa huduma kwa kiwango cha juu zaidi,” alishauri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,654FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles