24.8 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

‘WATAKAOISOMA’ NAMBA CCM KUJULIKANA JUMAPILI

 

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kutangaza maazimio ya kikao cha Kamati Kuu siku ya Jumapili, baada ya kumaliza kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho.

Kamati Kuu ya chama hicho  ilianza kukaa juzi ikiongozwa na Mwenyekiti wake, John Magufuli lakini haikufahamika mara moja uamuzi uliofikiwa katika kuchuja majina ya wagombea wa nafasi za uongozi katika ngazi ya wilaya.

Chama hicho tawala, kimeanza mchakato wa uchaguzi wa viongozi wake kuanzia ngazi ya shina na sasa umefikia wilayani ambako majina ya wagombea yanachujwa na vikao vya juu ambavyo vinafanyika Dar es Salaam.

Akizungumza na MTANZANIA jana kwa   simu, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alisema maazimio ya vikao hivyo vya juu yatatolewa   Jumapili.

“Maazimio ya kikao chetu tutayatoa Oktoba Mosi mwaka huu, baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa,”alisema Polepole.

Chama hicho kiliitisha kikao hicho Septemba 28 na 29 mwaka huu baada ya kumalizika  mchakato wa uchaguzi wa nafasi za viongozi ndani ya chama hicho kuanzia ngazi ya shina hadi taifa.

Katika kikao hicho, wajumbe walitakiwa kujadili majina ya wagombea huku majina mengine yakienda kuchujwa kwenye vikao vya juu.

Kutokana na hali hiyo, kikao cha Halmashauri Kuu ambacho kitafanyika  kwa siku mbili   kitakuwa na lengo la kubariki mapendekezo ya kamati hiyo  na utendaji wa chama.

CCM ilifanya kikao chake kwa usiri na baada ya kumalizika hakukuwa na taarifa yoyote iliyotolewa huku vyanzo vya habari vikidai   kikao hicho kilipokea taarifa ya kamati ya maadili kuhusu mwenendo wa wagombea wakati wa mchakato wa kuchukua fomu na kurudisha.

Katika mchakato huo, wagombea walipigwa marufuku kujitangaza kuanzia mchakato wa uchukuaji na urudishaji wa fomu na kwamba atakayefanya hivyo ataondolewa.

Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma, mtu yeyote anayewania nafasi ya uongozi ndani ya chama akiwa mtumishi wa umma,   baada ya jina lake kupitishwa, anatakiwa kuandika barua ya kuacha kazi ili kutumia nafasi aliyowania.

Katika kuhakikisha   suala hilo linafanikiwa, Rais Magufuli alipiga marufuku   viongozi wa chama au Serikali kushika nafasi mbili za uongozi na   kama kiongozi yeyote aliyewania nafasi hiyo, uwezekano wa kuondolewa ni mkubwa.

Kutokana na hilo, wanachama wa chama hicho ambao walizoea utamaduni wa zamani ikiwamo   kuanza kampeni mapema na wale ambao wamekuwa wakitajwa kutumia rushwa, wataanza ‘kuisoma namba’.

Pia wagombea ambao watapitishwa watakuwa na wakati mgumu wa kujua mustakabali wao hadi watakapotangazwa mbele ya mkutano wa uchaguzi.

Ugumu huo unatokana na wagombea watakaoteuliwa kutatakiwa kwenda mbele ya wapigakura na kukutana nao kwa mara ya kwanza siku ya uchaguzi badala ya utaratibu uliozoeleka ya kujitangaza kwa kufanya kampeni.

Utaratibu huo utawaangusha wagombea wengi ambao watakwenda kwa mazoea ya miaka mingi ya kutegemea fedha na umaarufu kama mtaji wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles