Wataka bima vifaa tiba saidizi

0
684

Aveline Kitomary -Dar es salaam

MKUU wa Kitengo cha Vifaa Tiba Saidizi katika Taasisi ya Mifupa (Moi), Leah Mamseru, ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuweka utaratibu wa bima kwa vifaa tiba saidizi.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana Dar es Salaam, Mamseru alisema wapo wagonjwa ambao wanashindwa kupata viungo saidizi kutokana na gharama ya viungo hivyo kuwa kubwa kwani wengi wanapoteza uwezo wa kufanya kazi.

“Bima nyingi hazina fao la vifaa tiba saidizi, kwahiyo hawa watu wanashindwa kupata huduma kwa sababu wengi wana bima, lakini zina ‘limitation’ katika utoaji wa huduma zake, kwahiyo tunaomba Serikali iwaongezee fao la vifaa tiba saidizi katika bima ya afya,” alisema Mamseru.

 Alisema mtu akipoteza kiungo hata kimoja anaathirika katika uzalishaji, pia utafutaji wa fedha, hivyo wengi wanashindwa kupata viungo tiba.

“Mtu akishaathirika, uwezo wake wa kumudu gharama za kupata viungo bandia inakuwa shida, hiyo ni changamoto kubwa sana hapa, uwezo ni mdogo, mtu anakuwa hajiwezi, wengine wamepoteza uwezo wa kutembea uwezo wa kufanya kazi, wanashindwa kumudu uwezo wa kufanya kazi.

“Hali ya gharama kubwa inatokana na upatikanaji wa viungo bandia unakuwa wa shida kwani ‘material’ tunapata nje ya nchi na hakuna uhakika wa kupata kwa wakati,” alisema Mamseru.

 Hata hivyo, alitoa ushauri kwa jamii kuwawahisha watoto wao hospitali pindi wanapogundua wana tatizo la viungo kwani hii inasaidia mtoto kupona na kurudi katika hali ya kwaida.

“Wapo watoto wanaozaliwa wakiwa na matatizo au wamepata madhara katika viungo vyao, watoto wengi wanaoletwa tayari wameshapata madhara makubwa na uwezo wa kupona unakuwa ni mdogo, hivyo nawashauri wazazi wawahishe watoto mapema ili wapatiwe matibabu,” alishauri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here