25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wasimamizi uchaguzi Zanzibar wanolewa

KHAMIS SHARIF -ZANZIBAR

TUME ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), imewataka maofisa na maofisa wasaidizi wa uchaguzi kisiwani Unguja, kuhakikisha wanazingatia matakwa ya katiba, sheria na kanuni za uchaguzi ili kuenda sambamba na chaguzi watakazozisimamia.

Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Mbarouk Salim Mbarouk, alitoa agizo hilo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa maofisa hao Kikwajuni mjini Unguja.

Alisema pamoja na baadhi ya maofisa kuwa na uzoefu wa kuendesha chaguzi mbalimbaali nchini, wanatakiwa kuzingatia maelekezo watakayopewa na tume badala ya kufanya kazi  za uchaguzi kwa mazoea.

Aidha Jaji Mbarouk alisema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali, hivyo kufuatwa na kuzingatia kwa hatua na taratibu hizo ndio msingi wa uchaguzi na kuufanya kuwa bora na wenye ufanisi.

“Uchaguzi ni uchaguzi tu, hakuna uchaguzi mkubwa wala mdogo, tufuate melekezo sahihi ili kuondoa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi” alisema Jaji huyo.

Alisema NEC imewaamini ndipo ikawateuwa kwa sababu wana uwezo wa kufanya kazi hiyo, hivyo  ni lazima jambo hilo lifanywe kwa misingi ya kujiamini na kujitambua kwamba wanapaswa kuzingatia katiba ya nchi, sheria za uchaguzi, kanuni zake na maadili.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 74 (6), tume imepewa jukumu la kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na wabunge wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na madiwani kwa Tanzania bara.

“Tume imewateuwa ninyi kwa mujibu wa sheria na kuzingatia utendaji na uzoefu wenu katika masuala ya chaguzi, pia kwa kusoma alama za nyakati, simamieni wajibu wenu ili kuona kila hatua inaenda sawa ,” aliongeza.

Alisema katika utekelezaji wa majukumu yao ni muhimu kuzishirikisha vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika masuala ambayo yanastahili kushirikishwa.

Sambamba na hayo alieleza ni muhimu kuyajua na kuyatambua vyema maeneo yao wanayofanyia kazi ikiwemo miundombinu ya kufika katika kata na vituo vya kupigia kura.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Sheria NEC, Emmanuel Kawisha, alisema chini ya kanuni ya 16 (1) (b) na (3) ya kanuni za uchaguzi wa Rais na wabunge 2020 na kanuni ya 14 (1) (b) na (3) ya kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa msimamizi yoyote hatotakiwa kuwa mfuasi wa chama chochote cha siasa na kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria ya uchaguzi.

Aliwataka maofisa hao kuhakikisha hawavai sare za chama wala kushabikia chama chochote cha siasa kuanzia sasa na atakaebainika kufanya hivyo atavuliwa cheo chake na kupewa mtu mwengine atakayeweza kutunza kiapo cha uchaguzi.

Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 89 a na (b) cha Sheria ya Uchaguzi, mtendaji au msimamizi yoyote atakaesababisha uchaguzi kuharibika basi atatozwa faini ya Sh 1,000,000 au miaka miwili jela au vyote viwili kwa pamoja.

Mbali na hayo aliwasihi kutunza siri za kiapo kwa kuzingatia katiba na sheria ya uchaguzi, huku akisema kuna makosa ambayo yanafanywa na watendaji wa uchaguzi wakati wa uchaguzi ikiwemo usimamizi hafifu wa maofisa katika vituo vya kupigia kura na kukosa umakini katika kuchagua watendaji mbalimbali wa uchaguzi.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar, Hamidu Mwanga, aliwaomba maofisa hao, kuimarisha mahusiano ya karibu katika kuhakikisha zoezi la uchaguzi linafanyika kwa urahisi Oktoba 28 mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles