27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 4, 2023

Contact us: [email protected]

Wanawake waongoza kufa kwa pombe Amerika

VIFO vinavyotokana na pombe barani Amerika vimepaa kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, hasa kwa wanawake, utafiti mpya nchini Marekani umebaini.

Kati ya mwaka 2007 hadi 2017; vifo vinavyohusiana na pombe vilifikia asilimia 35 lakini kwa upande wa wanawake pekee vilifikia asilimia 67.

Takwimu hizo kutoka Chuo Kikuu cha Washington nchini humo, ambazo awali ziliripotiwa katika Jarida la USA TODAY, zimekuja mwaka mmoja baada ya takwimu za Shirikisho kuonesha ongezeko kubwa la unywaji wa vileo kwa wanawake na wazee.

Watafiti wanasema kwa vile mkazo mkubwa umetiliwa ili kukabiliana na ongezeko la kutisha la matumizi ya bangi na mihadarati, ongezeko la vifo kutokana na pombe limepaa na hivyo kuzua wasiwasi kutokana na kutotiliwa maanani.

“Jambo la kusikitisha ni kwamba hakuna mtu anayeona hili kama ni tatizo kubwa,” anasema Max Griswold wa Taasisi ya Afya na Tathimini (IHME), iliyoanzishwa katika Chuo Kikuu cha Washington na bilionea Bill na mkewe Melinda Gates.

Anaonya: “Ni tatizo ambalo halikuwahi kufanyiwa utafiti huko nyuma, na iwapo litaachwa, kuna siku tutazungumza mengine tukiwa tumeshachelewa.”

Data za IHME zilikuwa sehemu ya utafiti uliokuwa ukitazama viwango vya vifo, sababu za vifo hivyo, kiwango cha uzazi, uwezo wa kuzaa na zaidi katika ngazi ya kidunia.

Utafiti huo uliojikita zaidi katika takwimu za Marekani, umeonesha kwamba mwelekeo wa unywaji pombe na vifo kwa wanawake unatia wasiwasi.

Awali, pombe ilikuwa mwiko kwa wanawake, lakini kwa sasa imekuwa sugu kwao.

Sasa hivi ulevi uliopitiliza kwao si kitu cha ajabu, mwelekeo huo hauonekani kuendana na maumbile yao.

Wakati bailojia ya mwili wa binadamu ikiwa haijabadilika, matumizi ya pombe hasa kwa wanawake yameongezeka kinyume na namna miili yao inavyoweza kupokea ongezeko hilo.

Kwa ujumla, unywaji wa pombe unaweza kusababisha madhara makuwa katika mwili wa mwanamke kuliko wa mwanamume.

“Imetoka kuwa mwiko kwa wanawake kunywa pombe hata walau kidogo hadi kuwa wingi ikihusisha kundi kubwa la wataalamu, ambao pia hunywa hadi kiwango cha kusababisha sumu mwilini,” Deidra Roach, Mkurugenzi Mtendaji wa Mradi wa Afya katika Taasisi ya Tiba na Utafiti anasema.

Anaongeza: “Wanawake ni wadogo kuliko wanaume na wana kiwango kidogo cha maji na mafuta mwilini.

Kiwango cha damu hupanda zaidi na haraka na hukaa kwa muda mrefu katika mwili wa mwanamke na hivyo, kuleta madhara hata kama mwanamke na mwanaume hunywa kiwango sawa, basi dalili za pombe zitaonekana haraka kwa wanawake.

Pombe inaweza kusababisha vifo kwa njia nyingi. Inaweza kusababisha maradhi ya ini, saratani, ajali na masuala ya mfumo wa chakula yanayotishia uhai.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya IHME, viwango vya vifo vinavyotokana na pombe viko juu katika majimbo ya Washington, DC, Georgia na Albama.

Majimbo mawili ya mwisho haishangazi kwa sababu eneo la kusini mwa nchi lina historia ya kuwa na viwango vikubwa vya matumizi ya pombe, ulevi sugu, uvutaji sigara, unene na viwango vya chini vya bima ya afya.

Hali hiyo inamaanisha watu wengi hawana madaktari wa kuwashauri namna ya kuishi staili yenye afya ya maisha. Umasikini pia uko juu, kitu kinachochea kupaisha kiwango cha ulevi.

Lakini kiwango cha kutisha cha vifo vinavyotokana na pombe kimeonekana katika maeneo mengine pia ya nchi, hasa Kaskazini na Kaskazini Magharibi.

Wiki iliyopita, kikosi cha nguvu kazi ambacho hushauri madaktari wa Marekani juu ya viwango kiliongeza pendekezo la ushauri katika suala la uchunguzi wa pombe.

Kilisema, madaktari wanapaswa kuchunguza wagonjwa wote kuhusu matumizi ya pombe yasiyo na afya, na kutoa ushauri nasaha kwa wale wanaoonekana kuwa na tatizo.

“Nchini Marekani, mgonjwa mmoja kati ya sita wameripotiwa kujadiliana na daktari wao kuhusu pombe; viwango ambavyo pia barani Ulaya viko chini,” Angela Bazzi na Dk. Richard Saitz wa Shule ya Afya ya Umma, Chuo Kikuu cha Boston nchini Marekani wanaandika tahariri katika Jarida la JAMA.

Wanaongeza kuwa kuna ushahidi kuwa kujadiliana na daktari kunavyoweza kuleta athari chanya kwa tabia ya mtu.

Katika suala la namna ya kufuatilia hili, kikosi kazi kilipendekeza kuwapo ratiba za utoaji ushauri nasaha usiopungua saa mbili.

Wanasema ushauri nasaha unaweza kufanywa ana kwa ana au hata kwa njia ya mtandao.

Takwimu hizo zinakuja huku nyingine zilizotolewa Juni mwaka huu nchini humo zikionesha uwapo wa viwango vya vifo vikifikia asilimia 57 miongoni mwa wanawake vikitokana na ini kuathirika kutokana na pombe kwa wale walio na umri kati ya miaka 45 hadi 64 kwa kipindi cha mwaka 2000 hadi 2015 nchini Marekani, ikilinganishwa na asilimia 21 ya wanaume.

Kiwango hiki kilipanda kwa asilimia 18 kwa wanawake walio na umri kati ya miaka 25 hadi 44, licha ya kuongezeka kwa asilimia 10 kwa wanamume wenye umri kama huo.

Idadi ya wanawake watu wazima wanaozuru hospitalini kwa dharura baada ya kunywa pombe kupita kiasi wameongezeka.

Wanasayansi wamegundua kwamba wanawake huzalisha viwango vya chini vya vimeng’enya vinavyoitwa kitaalamu alcohol dehydrogenase (ADH), ambavyo hutoka ndani ya ini na kuvunja vunja pombe mwilini.

Wakati huohuo, mafuta huzuia pombe huku maji yakitumika kuitoa mwilini.

Wanawake walio na tatizo la unywaji pombe hujikuta wakinywa tena uzeeni zaidi ya wanaume, ambapo huchukua muda mfupi kuipenda.

Wanawake pia hupata ugonjwa wa ini, moyo na kuathirika neva zao ikilinganishwa na wanaume.

Tofauti hii kubwa ya kijinsia kuhusu athari ya pombe mwilini hazikugundulika hadi miongo ya hivi karibuni.

Utafiti wa mapema kuhusu tofauti za kijinsia ulifanyika mwaka 1990, na kwa sababu tatizo la unywaji wa pombe lilionekana kuwa la wanaume, hakuna mtu aliyejali kwamba kuna kitu wanakosa kutoka kwa wanawake.

Hilo lilibadilika wakati taasisi za serikali kama ile ya kitaifa ya afya nchini Marekani ilipoagiza wanawake washirikishwe katika kufanyiwa utafiti, hatua iliyolazimu tofauti za kijinsia katika tafiti za matibabu kuanzishwa.

”Wanasayansi walidhani kwamba unapowafanyia wanaume utafiti, matokeo yake pia yatawaathiri wanawake,” anasema Sharon Wilsnack na kuongeza:

“Watu hawakuwafikiria wanawake.”

Akisomea shahada yake ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani, mapema miaka ya 70, Wilsnack aliandika kuhusu wanawake na pombe, huku akiruhusiwa kufanya tafiti saba katika chuo hicho.

Akiwa na mumewe, mwanasosholojia huyo aliongoza utafiti wa kitaifa kuhusu tabia za wanawake za unywaji pombe.

Miongoni mwa matokeo ya utafiti wake ni ugunduzi kwamba wanawake wanaotumia pombe hunyanyaswa kijinsia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles