23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Wanaobeza kiswahili wanastahili adhabu

Rais mstaafu Ally Hassani Mwinyi
Rais mstaafu Ally Hassani Mwinyi

Na Mwandishi Wetu,

KUNA mambo ambayo najivunia daima. Mojawapo ni kuwa muumini wa lugha ya   kiswahili. Nimekuwa katika pilika za mara kwa mara kujitahidi kujifunza zaidi lugha hiyo siku hadi siku.

Desemba mwaka 2006, nilipata mwaliko wa kuhudhuria mafunzo kwa vyombo vya habari kuhusu mlundikano wa kemikali mbalimbali zilizoingizwa barani Afrika na kutelekezwa huku zikileta madhara kwa wakazi wa bara hilo. Kemikali hizo ni kama vile dawa za kuua wadudu katika mazao.

Waandaaji wa mafunzo hayo wakashinikiza kuwa waalikwa sharti wajiandae kushiriki mijadala ambayo ingeendeshwa kwa lugha ya kiingereza. Wakasema kama kungekuwa na mshiriki ambaye hakuwa tayari kwa hilo basi atoe taarifa ili nafasi yake ichukuliwe na mtu mwingine.

Bahati nzuri ikawa upande wangu. Katika chumba changu cha habari kulikuwa na waalikwa wengine. Kwa pamoja tukafanya kikao kujadili sharti hilo. Tukajiuliza sababu za msingi za waandaaji kufanya hivyo. Tulipowapigia simu kuwauliza mashiko ya sharti lao hawakuwa na sababu za msingi. Washiriki wengi walikuwa Watanzania na Wakenya ambao kiswahili ni sehemu ya maisha yao.

Nasi kwa upande tukasema kuwa tusingekuwa tayari kushiriki mafunzo hayo kwa sharti la utumiaji wa Kiingereza. Kwamba kama mshiriki angejisikia kutumia lugha hiyo ya kigeni basi afanye hivyo kwa ridhaa na isiwe lazima. Mwishowe waandaaji wakanyosha mikono juu na kukubali hoja yetu.

Yapo matukio mengi yafananayo na hayo. Semina mbalimbali zimewalazimisha washiriki kutumia lugha ya kiingereza hata kama washiriki wengi ni Watanzania wanaojua vema kiswahili. Wanabaki na pingu zao kichwani. Pingu za utumwa wa akili zinazowafanya waendelee kuamini kuwa matumizi ya kiingereza na sehemu ya kuonekana mpevu katika masuala mbalimbali.

Hata watoto wa shule wanaozungumza kiingereza ni fahari kwa wazazi na walezi wao. Kundi hilo la watoto huonekana kuwa ni la werevu kuliko wanaozungumza kiswahili pekee. Wazazi wanasahau kuwa kukibeza kiswahili na kukikumbatia kiingereza pekee ni hatari kwa taifa na utamaduni wake.

Sisemi kuwa Kiingereza kisifundishwe nchini. Hoja iliyo mbele yetu ni umuhimu wa kukikumbatia Kiswahili ili kuendeleza utamaduni wetu. Kuipuuza lugha hiyo ni dhambi ambayo wanaohusika wanapaswa kutubu.

Mara kadhaa natumbukia nyongo ninapowasikia baadhi ya wabunge wakichangia mijadala mbalimbali ya Bunge kwa kutumia lugha ya kiingereza. Unashangaa ni namna gani mbunge huyo anashindwa kutambua kuwa yupo katika ardhi ya Tanzania na si kwa Malkia Elizabeth. Wapigakura wake wengi hawaelewi hoja yake inalenga kitu gani. Mbona wakati wa kampeni hatuwasikii mkitumia kiingereza? Wengi wenu mnazungumza kiswahili mnapoomba kura. Tena wengine huenda mbali na hapo na kuzungumza lugha za makabila yao. Hiyo ni hatua nzuri ya kuenzi mila na utamaduni.

Itoshe basi kusema kuwa kama mlikuwa mmejisahau, huu ni wakati wa kuamsha fikra zenu mpya na kukubali kuwa Kiswahili ni chetu na hatuna budi kukikumbatia. Usipothamini cha kwako nani atakithamini? Husemwa kuwa msahau kwao ni mtumwa.

Hivyo basi, huu ni wakati wa kujitambua na kukubali mema ya kwetu na kuachana kabisa na utumwa wa akili ambao umedumu kwa miaka mingi sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles