24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

Waliotelekeza mashamba ya chai watakiwa kuyafufua

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Dk. Hussein Omar, ameagiza wamiliki waliotelekeza mashamba ya chai kuyafufua na kuyatunza ili kuzalisha kwa tija na ubora unaotakiwa sokoni.

Agizo hilo amelitoa leo Novemba 13, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mnada wa chai kwa njia ya mtandao uliofanyika jijini na kuudhuriwa na wanunuzi,wauzaji, wazalishaji na wakulima wa zao hilo.

“Nielekeze wamiliki wote wa mashamba ambayo wameyatelekeza wahakikishe wanayafufua na kuyatunza vizuri na wahakikishe wanalima kwa tija na ubora unaotakiwa sokoni,” amesema.

Pia amewataka wamiliki wa viwanda kuwalipa wakulima wadogo ili kuongezea hamasa kuendelea na kilimo cha zao hilo.

Dk. Omar ameziagiza taasisi zinazosimamia zao hilo kwa kushirikiana na wadau wote wa chai kuweka mikakati mathubuti ya kuongeza uzalishaji, tija na ubora wa zao hilo.

Amesema ili kuweza kufanikiwa lazima kuwekeza  katika ubora na tija lakini pia wasindikaji wote wanapaswa kushiriki kwenye mnada wa chai unaofanyika nchini.

“Wasindikaji wanapaswa kushiriki kuinua mnada wa chai kwa kuuza angalau asilimia 15 ya chai wanayozalisha na kuwakilisha mauzo ya moja kwa moja kwenye mnada huu,”amesema Dk.Omar.

Aidha amewataka pia kuchochea ushirikiano na nchi jirani zinazozalisha zao hilo ili kuhamasisha kutumia mnada wa hapa nchini.

Naye Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Chai Nchini, Mary Kipeja, amesema  wanakabiliwa na changamoto  mbalimbali ikiwamo ufinyu wa bajeti wa kutangaza mnada kwenye masoko mpya na nje ya nchi.

Amesema kuanzishwa kwa mnada huo kutakuwa na manufaa makubwa kwa wakulima, wazalishaji na Serikali kuongeza pato la Taifa kwa kutumia  Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake.

“Taarifa za mauzo ya chai rekodi ya  Julai hadi Oktoba ni tani 2584 asilimia 18 ilibaki nchini asilimia 82 ilipelekwa Mombasa nchini Kenya, hivyo mnada kufanyaki nchini kutapunguza gharama kwa asilimia 50 na mkulima atapata faida,”amesema Mary.

Naye Kaimu Mwenyekiti  wa Chama cha Wazalishaji wa Chai Nchini (TAT), George Mwakamula amesema mnada huo utakuwa na manufaa  makubwa kwa wakulima  wa chai na Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima Wadogo wa Chai, Felix Chole amesema mnada huo  utanufaisha wakulima tofauti na kufanya mnada nchi nyingine wakati chai wanalima wenyewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles