29 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Walimu wamkabili Pinda

mabangoMWANDISHI WETU, BUKOBA

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amepokewa kwa mabango mjini Bukoba, alipokuwa akimuwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye maadhimisho ya Siku ya Walimu duniani.

Walimu hao walimtaka Waziri Mkuu kuhakikisha mshahara wa mwalimu kwa mwezi unalingana na posho ya siku moja ya Mjumbe wa Bunge la Katiba ya Sh 300,000.

Mabango hayo ni yale yaliyokuwa yamebebwa na walimu waliokuwa wakiandamana kutoka Ofisi za Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Kagera, kuelekea Uwanja wa Kaitaba ambako maadhimisho ya siku ya walimu duniani yalifanyika kitaifa.

Baadhi ya ujumbe uliokuwa katika mabango hayo ni “Serikali ithamini kazi ya mwalimu kwa kutoa mshahara unaolandana na kipato cha siku moja cha Mbunge wa Katiba, hatuna makazi, tunanyanyasika nyumba za kupanga, Serikali ibadilishe mfumo wa pensheni za wastaafu kwani kiwango kinachopendekezwa ni unyonyaji.”

Katika hali ya kushangaza polisi walikamata bango lililokuwa likielezea kuwa ‘Serikali ithamini kazi ya mwalimu kwa kutoa mshahara unaolandana na kipato cha siku moja cha Mbunge wa Katiba’.

Bango hilo lilikamatwa na askari polisi na kulivunja hali iliyozua tafrani kwa walimu hao huku baadhi yao wakiingiwa na hofu.

Kutokana na hali hiyo walimu hao walisikika wakipinga hatua hiyo ya askari hao kwa kulaani kuvunjwa kwa bango hilo.

Akizungumzia ujumbe uliokuwa kwenye mabango, mashairi, nyimbo na risala Waziri Mkuu Pinda, alisema Serikali imeguswa na ujumbe wa walimu hao na wataufanyia kazi.

“Serikali imeguswa na ujumbe wa walimu uliotolewa kwa njia ya nyimbo, mashairi pamoja na mabango yaliyoonyeshwa katika maandamano haya, ujumbe huo Serikali itaufanyia kazi kupitia vikao mbalimbali vitakavyohusisha chama cha walimu,” alisema.

Alisema kuwa Serikali inajitahidi kuboresha maslahi ya walimu na kwamba, ilikuwa ikidaiwa Sh bilioni 85 na mpaka sasa imelipa Sh bilioni 65.

Waziri Mkuu alisema ni kweli walimu wanalipwa mshahara mdogo kwa kuwa Serikali ina mahitaji mengi katika kuhudumia jamii na wafanyakazi wake wote.

“Serikali tumeazimia kuboresha miundombinu katika vyuo vya ualimu ili wapatikane walimu bora, siyo bora walimu,” alisema Pinda.

Alisema pia kuwa Serikali itaboresha pensheni wanazolipwa walimu pindi wanapostaafu.

Awali Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Taifa, Yahaya Msulwa, alisema walimu nchini wanaidai Serikali zaidi ya Sh bilioni 11, kama malimbikizo ya mishahara pamoja na nauli zikiwemo fedha za matibabu na likizo wanazostahili kupata kwa mujibu wa sheria.

Msulwa amesema katika miaka miwili iliyopita, Serikali imelipa kiasi cha Sh bilioni 65.48 lakini malimbikizo hayo yamekuwa yakiendelea kuongezeka hali inayoathiri utendaji wa walimu.

Alisema kuchelewa kupandishwa madaraja ni changamoto nyingine inayowakabili walimu kwani mpaka sasa walimu 37,486 hawajapanda madaraja.

Aliongeza kuwa walimu waliopanda madaraja na kulipwa stahili zao ni 37,056.

“Serikali iboreshe maslahi ya walimu kwa kuwaongezea mshahara na posho ya kufundishia ikiwemo ya mazingira magumu ili kuleta ufanisi wa kazi,” alisema Msulwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenesta Mhagama, alisema Serikali imeanza kuweka mikakati ya kuboresha kazi na maisha ya walimu kwa kuandaa mpango wa kuwaendeleza kitaaluma kwa muda stahili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles