29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Walimu wa kujitolea waula Dar

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Walimu 150 wa masomo ya sayansi waliokuwa wakijitolea katika shule mbalimbali za sekondari za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wamepewa ajira za mkataba kukabili upungufu uliopo.

Juni 2023 Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ilitoa mwongozo unaoelekeza kuwatumia walimu waliohitimu vyuo ambao bado hawajaajiriwa ili kuboresha taaluma na utaalam wao wakati wakisubiri kuajiriwa na serikali au taasisi binafsi.

Akizungumza Aprili 16,2024 wakati wa kikao kazi na walimu hao Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Doreen Massawe, amesema mahitaji ya walimu wa sayansi ni 1,146 lakini waliopo ni 547.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akizungumza wakati wa kikao na maofisa elimu kata, wakuu wa shule na walimu wa ajira za mkataba wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

“Tuna upungufu wa walimu 599, mkurugenzi aliona changamoto hii akaamua kuwaajiri walimu waliokuwa wakijitolea kwa kuwapa ajira ya mkataba, tutapunguza changamoto ya walimu wa sayansi na itasaidia kupandisha ufaulu,” amesema Massawe.

Mmoja wa walimu hao Anselimin Ligoho ambaye amejitolea kwa miaka minne katika Shule ya Sekondari Binti Mussa, ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha ufaulu wa masomo ya sayansi unaongezeka.

“Tunashukuru kwa kuaminiwa kwa muda ambao tumeutoa, tulisikiliza sana walimu ambao tuliwakuta na tulifanya kazi hata pasipo malipo. Tuliamini ipo siku moja na sisi tutaonekana hivyo, tukafanya kazi kwa bidii, tunashukuru Mungu ametuona,” amesema Mwalimu Loyce Danford anayefundisha Shule ya Sekondari Mnazi Mmoja.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema wameajiri walimu hao kwa sababu wanaweza kuwalipa kwa kutumia mapato ya ndani ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi.

Kwa mujibu wa Mpogolo, katika mwaka wa fedha wa 2023/24 waliweka lengo la kukusanya Sh bilioni 89 lakini mpaka sasa wameshakusanya zaidi ya Sh bilioni 83 na kuahidi kuwa watavuka lengo la kukusanya zaidi ya Sh bilioni 120.

“Tunahitaji walimu wa kutosha na hatuwezi kusubiri Serikali Kuu peke yake, lazima tuwe na jitihada za kwetu za kukabili changamoto mbalimbali.

“Mwajiri anatazamia kuona tija, tunataka kuongeza ufaulu kwenye shule zetu kwahiyo hakikisheni mnakwenda kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili,” amesema Mpogolo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles