30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

WALIMU DODOMA WALIA NDOA ZAO HATARINI KUVUNJIKA

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WALIMU wa kike katika Manispaa ya Dodoma  wamemlilia Mkuu wa Wilaya hiyo, Christina Mndeme kuwa ndoa zao zimekuwa zikiingia migogoro mingi na wakati mwingine kuvunjika kwa  sababu ya kupangiwa vituo vya kazi mbali na waume zao.

Pamoja na kilio hicho, Mndeme amewajia juu na kuwataka wasisingizie kigezo cha waume zao kuwa mbali  bali wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kulinda ndoa zao.

Hayo yalisemwa jana na mwakilishi kutoka Kitengo cha Chama cha Walimu Wanawake Manispaa ya Dodoma, Joyce Kaishozi, wakati wa semina ya walimu wanawake kujifunza sheria za kazi na ajira kwa ajili ya kuwajengea uwezo na kuzifahamu   kuondokana na ukiukwaji wa maadili.

Kaishozi ambaye ni mwalimu, alisema ingawa walimu wanawake wanafanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii, wamekuwa wakikutana na changamoto kubwa ikiwamo kukaa mbali na waume zao.

Alisema jambo hilo linaweza kusababisha magonjwa kwa wanandoa kama maambukizi ya virusi vya Ukimwi, ndoa kuvunjika, migogoro ndani ya ndoa na watoto kuwa na malezi ya mzazi mmoja.

“Waume zetu ni muhimu wakati mwingine, tunakaa nao mbali, unajikuta ufanisi wa kufanya kazi unapungua,” alisema.

Alisema changamoto nyingine ni kutopandishwa madaraja na kupata mishahara stahiki kulingana na daraja husika kwa wakati.

“Kuna walimu ambao hawapo kwenye madaraja stahiki, wamepunjwa, hii inatokana na kutopandishwa madaraja kwa wakati,” alisema.

Naye  Mndeme aliwataka walimu kufanya kazi kwa bidii bila ya kuchagua maeneo ya kufanyia kazi.

Alisema mwalimu anatakiwa kufanya kazi sehemu yoyote, isipokuwa anaweza kubadilishiwa kituo cha kazi  ambako atabainishwa na daktari kuwa ana tatizo lolote la afya.

“Tusichukue kisingizio cha mume, bali kinachotakiwa kuheshimu ndoa zenu, nawaomba walimu wangu msihatarishe ajira zenu kwa kisingizio cha ndoa ila kama familia ina matatizo lazima tuzingatie,” alisema.

Aliwataka walimu hao kutumia fursa ya Serikali ya kuhamishia makao makuu Dodoma kwa kuwa wabunifu wa miradi mbalimbali waweze kujiongezea kipato.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,391FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles