22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Walezeni wananchi mafanikio ya Serikali-Matinyi

Na Gustafu Haule, Mtanzania Digital 

MKURUGENZI wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amewashauri viongozi wa Serikali kuhakikisha wanawaelezea wananchi miradi iliyotekelezwa katika maeneo yao ili kuondoa sintofahamu baina ya wananchi na serikali yao.

Matinyi amebainisha hayo jana katika mkutano wake uliofanyika Mjini Kibaha mkoani Pwani na kuhusisha viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa, Abubakar Kunenge, Wakuu wa wilaya, viongozi wa mkoa huo pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri.

Amesema, serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa ajili ya maslahi ya wananchi lakini wananchi hawaelezwi michanganuo na mengine ambayo yamefanywa na serikali.

Aidha, amesema viongozi wa mikoa wanatakiwa kusimamia fedha za utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kuleta matokeo chanya kwa wananchi sambamba na kuwashirikisha kwa kila hatua kwenye maeneo husika.

Akielezea kuhusu mkutano huo amesema ni moja  ya mpango uliozinduliwa hivi karibuni jijini Dodoma kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyofanywa na serikaii kwa kipindi cha miaka mitatu na itaendelea katika mikoa yote 26 ili taarifa za serikali ziwafikie wananchi.

Naye Mkuu wa Mkoa  wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema katika kipindi cha miaka mitatu Mkoa umepokea  Sh trilion 1.19 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi ya afya, Elimu, Maji na miundombinu na hivyo kupunguza vikwazo vilivyokuwa vinawakwamisha maendeleo kwa wananchi. 

Kuhusu miradi ya miundombinu ya barabara amesema serikali ipo mbioni kuanza ujenzi wa upanuzi wa barabara kuanzia Dar es Salaam-Chalinze-Morogoro ambayo itakwenda kuondoa msongamano . 

Aidha, Kunenge amefafanua kuwa ujenzi mwingine ni wa barabara ya Chalinze-Utete ambao kukamilika kwake kutafungua fursa ya wananchi  katika maeneo hayo kufanya biashara ambazo zitawapatia kipato na hivyo kuinua uchumi .

Katika mkutano huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Hemed Magaro ameishukuru Serikali kwa namna ilivyotoa fedha za miradi ambayo imekwenda kutatua vikwazo kwa wananchi hususani katika eneo la delta. 

Magaro amesema awali wananchi wa Mbwera walikuwa wanasafiri kilomita 90 kwenda kupata huduma za afya na wakati wa mvua walikuwa hawawezi kusafiri  hivyo ujenzi wa kituo cha afya katika eneo lao imeondoa tatizo lililokuwa linawakabili.

Kadhalika, Mkurugenzi huyo amesema ongezeko la vituo vya afya pamoja na vifaa tiba katika Halmashauri hiyo pia imechangia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles