24.8 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

Wakulima wagoma kuuza korosho

Na FLORENCE SANAWA -NEWALA



MNADA wa kuuza korosho wilayani Newala na Tandahimba, Mkoa wa Mtwara umevunjika.

Ulivunjika jana mbele ya Naibu Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji, Omary Mgumba baada ya wakulima kukataa kuuza korosho ghafi katika mnada wa wazi wa kwanza uliofanyika Kijiji cha Makukwe, Wilaya ya Newala.

Wakati wa mnada huo kulikuwa na kampuni 15 zilizotuma zabuni za kununua korosho ghafi kwa bei ya juu ya Sh 2,717 kwa kilo moja na bei ya chini ikiwa ni Sh 1,711.

Wakati wanunuzi hao wakitaka kununua kwa bei hiyo, msimu uliopita katika mnada wa kwanza, kilo moja ya korosho ilinunuliwa kwa Sh 3,850.

Pamoja na hali hiyo, ununuzi wa korosho mwaka huu wanunuzi wanatakiwa kufika wenyewe katika minada wakiwa na barua za zabuni tofauti na misimu iliyopita ambayo walikuwa wakipeleka barua katika vyama vikuu na kusubiri minada.

Akizungumza baada ya wakulima kukataa kuuza korosho zao, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gellasius Byakanwa, aliwapongeza na kusema wamefanya uamuzi sahihi kwa kuwa wanunuzi wamekuwa wakiwaibia kwa kuwapangia bei ya kununua zao hilo.

“Wingi wa wanunuzi waliofika hapa haukuwa wa kawaida kwani wengine walifika kuangalia bei ya korosho hali ambayo ilionesha wana uhitaji wa bidhaa hiyo.

“Kwahiyo, nawapongeza wakulima kwa kusimamia thamani ya korosho yetu kwani hata tathmini niliyoifanya wakati barua zikisomwa, inaonesha wanunuzi walikuwa wamepanga bei.

“Kwa kweli mmenifurahisha sana kwani mahitaji ya korosho ni makubwa.

“Pamoja na kwamba leo mnada haukufanyika, bado naamini watakuja tu, yaani hakuna namna, korosho zetu ni bora hatuwezi kulima sisi na kuzihudumia kwa gharama kubwa halafu wanunuzi watupangie bei ya kuuza, haiwezekani,” alisema Byakanwa.

Naye Muksin Baba ambaye ni mkulima wa korosho wilayani Newala, alisema ni bora wakulima wakabaki na korosho zao badala ya kuziuza kwa bei ya chini kwa sababu wanatumia gharama kubwa kulima zao hilo.

“Haiwezekani tuuze korosho kwa shilingi 2,717 kwa kilo wakati tukibangua tunauza kwa shilingi 17,000 kwa kilo.

“Kwa kifupi ni bora tubaki nazo maana hawa wanunuzi hawajui kiasi gani tunataabika kwenye kulima na kuandaa korosho, lazima tuwe na msimamo ili kuwakomesha wanunuzi wasiojua thamani ya mkulima wa zao hilo,” alisema Baba.

Kwa upande wake, Hamis Juma ambaye ni mkulima wilayani Tandahimba, alisema bei iliyotajwa kwenye barua za wanunuzi haijawaridhisha kwa kuwa ni ndogo na haiwasaidii chochote kwa kuwa wanatumia gharama kubwa katika kilimo chao.

Awali akifungua mnada huo, Naibu Waziri Mgumba alisema wakulima wanapaswa kuandaa korosho katika ubora unaofaa sokoni kwa kuwa ubora mdogo husababisha bidhaa kuwa na bei ndogo.

Aliwataka wakulima hao kutunza ubora za korosho ili kuliongezea thamani zao hilo kwa kuwa litahitajika zaidi katika soko la dunia.

“Kamwe tusitumie vibaya fursa hiyo kwa sababu korosho zetu ni nzuri na zinajiuza sokoni. Lazima tukemee udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wakulima wanaosababisha ubora wa korosho zetu kuwa mdogo,” alisema Mgumba.

Wakati huo huo, Meneja Mkuu wa Tanecu, Mohamed Mwinguku, alisema msimu huu unaonesha kuna dalili za bei kushuka tofauti na msimu uliopita.

“Pamoja na hayo, mimi si msemaji wa zao hilo bali wanaohusika na kushuka kwa bei ni Bodi ya Korosho Tanzania ambao ndio wasemaji,” alisema Mwinguku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles