25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

Wakili Msando aendelea kushikiliwa polisi kwa tuhuma za uchochezi

Janeth Mushi -Arusha

JESHI la Polisi mkoani Arusha, linashikilia watu wawili akiwemo Wakili Albert Msando (40), mkazi wa Lemara kwa madai ya kutoa taarifa za uchochezi dhidi ya Serikali juu virusi vya corona.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Koka Moita, alisema walimkamata Msando juzi Aprili 29 saa 8:30 mchana.

Moita alisema kupitia video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii, inaonyesha Msando akieleza kwamba hali ya corona Arusha ni mbaya sana, wakati hana mamkala ya kueleza lolote juu ya ugonjwa huo.

Alisema mtuhumiwa anadaiwa kutoa kauli hiyo wakati anazungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, alipokuwa akigawa vifaa vya kujikinga na virusi vya corona kwenye Ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, zilizopo Kaloleni.

“Ikumbukwe kwamba Serikali ilitoa maelekezo kuwa wenye mamlaka ya kutoa taarifa juu ya ugonjwa huo ni Waziri Mkuu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na watoto na Mganga Mkuu wa Serikali,”alisema Moita.

Kamanda huyo akinukuu maneno ya Msando, alisema “ukweli ni kwamba na niseme bila kuficha, hali ni mbaya kwa Arusha hali ni mbaya na ndugu waandishi ninyi lazima mfike mahali muweke mguu chini mseme ukweli ili wananchi, Serikali na kila anayehusika atambue kwamba tupo katika hali mbaya  ambayo kila mmoja wetu anapaswa kuchukua hatua mkirudi nyuma na kuogopa kusema tutazikana.”

Katika hatua nyingine, Kamanda Moita alisema Aprili 29 walimkamata Agness Shinji (49), Mkazi wa Lemara jijini hapa kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo mitandaoni.

Alisema Aprili 9 mwaka huu mtuhumiwa huyo kupitia group la Whatsapp liitwalo Football for life, alisema mtangazaji wa TBC 1, Gloria Maiko amefariki dunia kwa corona wakati si kweli hali ambayo ilizua taharuki kwa ndugu, jamaa na marafiki.

“Mara baada ya jeshi la polisi kubaini uzushi wa taarifa hiyo, lilianza kumfuatilia mtuhumiwa na jana (juzi) Aprili 29 tulifanikiwa kumkamata ambapo katika mahojiano amekubali kulifahamu tukio hilo la kutumia taarifa ya kifo cha mtangazaji huyo bila kuwa na uhakika,”aliongeza

Alisema watuhumiwa wote wawili watafikishwa mahakamani mara baara ya upelelezi kukamilika ili sheria ichukue mkondo wake.

“Natoa onyo kwa makundi yote wakiwemo viongozi wa siasa na wananchi kwa ujumla kutokuwa wasemaji wa Serikali na wanapaswa kutii amri na maelekezo yanayotolewa na viongozi wakuu wa Serikali badala ya kwenda kinyume kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria,”aliongeza

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles