23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 11, 2024

Contact us: [email protected]

Wajasiriamali wafundwa njia bora uzalishaji mkaa mbadala

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa masuala ya Kiuchumi na Umaskini (REPOA) wameanza kuwajengea uwezo wajasiriamali wanaojihusisha kutengeneza mkaa mbadala ili wafahamu uzalishaji bora wa nishati hiyo.

Wajasiriamali wakizalisha mkaa mbadala unaotumia malighafi za taka za kilimo na misitu katika Shirika la
Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa mwongozo wa nchi wenye lengo la kuhakikisha kunakuwa na nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza Septemba 12,2023 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uzalishaji mkaa mbadala kwa wajasiriamali, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Profesa Mkumbukwa Mtambo, amesema yanashirikisha wazalishaji 22 kwa lengo la kuwaongezea ujuzi na ufahamu wa uzalishaji bora wa mkaa safi.

“Mafunzo haya yametayarishwa baada ya kufanyika utafiti katika mikoa 12 hapa nchini na kutembelea wazalishaji mkaa mbadala 58 na watumiaji 122.

“Utafiti ulifanywa na TIRDO kwa kushirikiana na REPOA ukiwa na lengo la kuimarisha uzalishaji wa mkaa mbadala na kukuza matumizi yake kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi nchini.

“Tutaweza kujua ni kwanini watumiaji wengi wa bidhaa wanabadili mawazo na kutumia nishati nyingine na si mkaa mbadala,” amesema Profesa Mtambo.

Amesema watafiti walichukua sampuli 43 za mkaa mbadala kutoka kwa wazalishaji katika mikoa hiyo na kupima kwenye maabara ambapo matokeo ndiyo yaliyopelekea mashirika hayo kufanya uboreshaji baada ya kubaini changamoto za viwango na ubora unaotakiwa.

Mkuu wa Kitengo cha Nishati katika Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania, Hossen Kayumba, akionesha mashine inayotumika kupima sampuli za nishati mbadala.

Mkurugenzi huyo amesema pia watafiti wameweza kusanifu mashine ya kuchomea malighafi za bayomasi yenye uwezo wa kupunguza niashati ya kuchomea kwa asilimia 50, kuvuna joto ambalo linatumika kukaushia mkaa na kuvuna vinega.

Mkurugenzi Mkuu wa REPOA, Dk. Donald Mmari, amesema wamebaini wazalishaji wengi hawana ujuzi wa kutosha kuzalisha mkaa mbadala wenye viwango vinavyokubalika.

Amesema mkaa mbadala utasaidia kutunza mazingira na misitu kwa sababu asilimia 85 ya Watanzania wanatumia mkaa unaotokana na miti.

“Unapokuwa na mkaa mbadala tutaokoa sehemu kubwa ya misitu yetu na kusaidia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa ambayo inachangia kwenye mabadiliko ya tabianchi na kuleta athari kubwa,” amesema Dk. Mmari.

Mwenyekiti wa Wazalishaji na Wasambazaji wa Nishati Safi Tanzania, Phinias Magesa, amesema bado kuna changamoto ya kutambuliwa kwa teknolojia ya uzalishaji nishati mbadala.

“Watu wanaozalisha teknolojia kama hizi wanaonekana hawana chochote lakini wana mchango mkubwa sana, tunashukuru Serikali imekuwa sikivu na wameanza kuwatambua wazalishaji wa mkaa mbadala…tukijikita katika mkaa mbadala tutapunguza ukataji miti,” amesema Magesa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles