27 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau wa ardhi waomba Serikali ikamilishe sera ya nyumba

Na Clara Matimo, Mwanza

Wadau wa ardhi na maendeleo ya makazi wameiomba Serikali ikamilishe sera ya nyumba  pamoja na kutoa kipaumbele kwa siku ya makazi duniani ili kuhamasisha jamii kuwekeza katika suala zima la makazi.

 Maombi hayo yametolewana Oktoba 3, 2022 na mashirika yasiyo ya serikali yanayojishughulisha kuboresha makazi TAHEA pamoja na Shirika la Nyumba Vijijini (MRHP)  kwenye maadhimisho ya siku ya makazi duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Koromije wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza kupitia mradi wa kuboresha makazi kwa wanawake na vijana(PAHWAYP) unaofadhiliwa na Shirika la WE- EFFECT la nchini Sweden lenye makao yake jijini Nairobi nchini Kenya.

Meneja Mradi wa PAHWAYP, Victor Kitambi kutoka shirika la MRHP akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya makazi duniani yaliyofanyika Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza.

 Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye maadhimisho hayo mameneja mradi wa PAHWAYP, Musa Masongo na Victor Kitambi wamesema ardhi ni sekta muhimu sana katika ukuaji wa pato la taifa kwani inaweza kuajiri watu wengi wakiwemo vijana hivyo kuinua uchumi wa nchi,  kukamilika kwa sera ya nyumba kutakuwa na manufaa.

Masongo amesema changamoto iliyopo ni serikali kutoipa kipaumbele siku ya makazi duniani kwani haijatoa umuhimu wa kutosha kuhamasisha jamii kuwekeza katika suala zima la makazi kama inavyofanya siku ya wanawake duniani.

“Ingawa Wizara ya Maendeleo ya Jamii inahamasisha lakini bado  nguvu kubwa haijawekwa pia katika masuala ya urasimishaji wa ardhi tunaishauri serikali ijiwekee mikakati kila mwaka kupima maeneo ambayo hayajajengwa kama wasipopima ndiyo tunaelekea katika makazi ambayo hayajapangwa hatakama yatarasimishwa yanakuwa hayana ubora sana.

“Wakifanya hivyo lengo namba 11 la dunia lisemalo kuwa na miji bora litaweza kufikiwa kwa urahisi kwa sababu tutakuwa na miji bora iliyokwishapangwa maana siyo kwamba maeneo yote yamejengwa kuna maeneo ambayo hayajajengwa,”amesema Masongo.

Masongo ameeleza kwamba mradi wa PAHWAY unalenga wanawake na vijana maana ni makundi yanayokutana  na changamoto kubwa ya kutokuaminiwa kumiliki ardhi  kulingana na mila na desturi hali inayosababisha kuwakosesha fursa ya kupata mikopo kwenye taasisi za fedha kwa dhamana ya ardhi zao ili waweze kufanya maendeleo.

“Tunaiomba serikali iendelee kuweka mazingira bora hasa katika sheria ya miradhi ambayo ilikuwa ikimnyima mwanamke haki ya kumiliki mali,”amesema Masongo na kufafanua.

“Mradi huu unaofadhiliwa na  shirika la WE –EFFECT linalojishughulisha kuboresha makazi ya watu wanaoishi katika makazi duni, ulianza Januari mwaka 2018 utakamilika Desemba 30, 2022, lengo lilikuwa ni kuwafikia wakazi 1800 hadi sasa tumewafikia zaidi ya wakazi 3,000 waishio Wilaya ya  Ilemela, Misungwi na Halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza.

Baadhi ya wananachi waliohudhuria maadhimisho hayo wameishukuru serikali kwa kuwapa elimu jinsi ya kumilikisha ardhi na kupata hati miliki za makazi yao kwani miaka ya nyuma walikuwa hawajui umuhimu wa kumiliki ardhi kisheria.

Nao baadhi ya wanufaika wa mradi huo akiwemo Esther Masele Mkazi wa Kijiji cha Mungwe Kata ya Mabuki, Joyce Nkondo Mwenyekiti wa vikundi vya ushirika koromije na Yombo Nganza mkazi wa Kijiji cha Koromije Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza wameyashukuru mashirika ya TAHEA na MRHP kwa  kuwaelimisha jinsi ya kujenga nyumba bora maana kabla ya kupata elimu hiyo walikuwa na makazi duni yaliyowapa adha hasa kipindi cha mvua maana zilikuwa zikidondoka hivyo kupata shida.

“Shirika pia limetuelimisha kuhusu ujenzi wa vyoo bora, utengenezaji wa mitungi saruji kwa ajili ya kuvuna maji mengi ya mvua sasa wananchi wengi wamenufaika kupitia mradi huu maana hata ambao hawamo katika mradi wameiga kwetu nao sasa wameanza kuelimika na kujenga makazi bora yenye mahali pazuri pa kulala, choo, maji na nishati, ”amesema Esther.

Kwa upande wake Afisa Ardhi Wilaya ya Misungwi, Peter Kisena aliwasihi wananchi kuchangamkia fursa iliyotolewa na serikali ya kurasimisha ardhi zao kwani kuboresha makazi bila kuwa na hati miliki za ardhi  hakutakuwa na tija sana kwao.

Siku ya makazi duniani ilianza kuadhimishwa mwaka 1986 na huadhimishwa Jumatatu ya Oktoba kila mwaka, lengo ni kutathmini changamoto zinazoikbili sekta ya nyumba na makazi pamoja na hali ya miji midogo na mikubwa ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema punguza ombwe la ardhi kwa wanawake  na vijana usiache mtu wala eneo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles