27.7 C
Dar es Salaam
Saturday, June 10, 2023

Contact us: [email protected]

WABUNGE SABA WANUSURIKA KIFO WAKITOKEA DODOMA

Na Waandishi Wetu-Dar es Salaam/Iringa/Morogoro


WABUNGE sita wa Zanzibar waliopata ajali eneo la Gwata, Morogoro wamefikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), pia Mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Cosato Chumi na familia yake wamenusurika kifo baada ya kupata ajali wakitokea mjini Dodoma kwenda jimboni kwake kusherehekea Sikukuu ya Pasaka na wapiga kura wake.

Wabunge hao kutoka Zanzibar wameumia vichwani, shingoni, mikononi, miguuni na vifuani na imeelezwa kuwa hali zao zimeanza kuimarika.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi ofisini kwake jana, Ofisa Uhusiano wa MNH, John Steven, alisema wamefikishwa Kitengo cha Magonjwa ya Dharura hospitalini hapo kwa uchunguzi zaidi.

“Tumewapokea saa saba mchana wakitokea Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Mbunge wa Makunduchi, Haji Ameir Haji, ambaye hali yake ilielezwa kuwa mbaya ameumia sehemu ya kichwani hivi sasa hajambo, anaendelea kupatiwa matibabu,” alisema.

Aliwataja wabunge wengine waliowapokea na majimbo yao katika mabano kuwa ni Juma Othman Hija (Tumbatu), Makame Mashaka Foum (Kijini), Khamis Ali Vuai (Mkwajuni) na Bhagwanji Maganlal Meisuria (Chwaka) na Ally Masoud (Mfenesini).

“Madaktari wetu wanafuatilia hali zao kwa ukaribu na wameanza kufanyiwa uchunguzi kwa kutumia mashine ya CT-Scan kujua hasa maeneo gani wamejeruhiwa ili kupata matibabu,” alisema.

Wabunge hao walinusurika kifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka.

Kamanda Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei, alisema ajali hiyo ilitokea saa mbili usiku jana katika eneo la Gwata wakati wabunge hao wakitokea Dodoma.

Matei alisema gari lenye namba za usajili Z.374HA iliyoendeshwa na Ally Masoud ikitokea Dodoma kwenda Dar es Salaam, iliacha njia na kusababisha wenzake kujeruhiwa.

Katika tukio jingine, Chumi na familia  yake walinusurika kifo kutokana na ajali  hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia jana eneo la Njiapanda ya Tosamaganga, Wilaya ya Iringa Vijijini kwenye Barabara ya Iringa-Mbeya.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyosababishwa na mwendesha  baiskeli.

“Ni kweli nilipata taarifa kuwa Chumi akiwa na familia yake akielekea jimboni kwake Mafinga alipata ajali na gari lake  liliacha njia wakati likimkwepa mwendesha baiskeli ila hakuna aliyepoteza maisha,” alisema.

Masenza alisema baada ya ajali hiyo kutokea Chumi alipata msaada wa gari jingine na kuendelea na safari ya kwenda Mafinga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire, alisema hana taarifa zaidi ya ajali hiyo na atakapofika ofisini kwake atawasiliana na mkuu wa polisi wilaya ili  kujua undani zaidi wa ajali hiyo.

Pia ajali nyingine ilitokea eneo la Iyovu baada ya basi la Kampuni ya New Force iliyoendeshwa na Emanuel Danford (44) liligonga gari ndogo Toyota Voltz yenye namba za usajili T 159 DKZ iliyoendeshwa na Luteni Oscar George wa Kikosi cha Mzinga cha JWTZ.

Matei alisema ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wawili na aliwataja waliofariki kuwa ni George (26) na Lucy Gadau (23) na miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,409FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles