25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge Kenya wataka Ruto achunguzwe

NAIROBI, KENYA



KASHFA ya muda mrefu ya mahindi nchini Kenya imeendelea kumwandama Naibu Rais William Ruto hadi kwenye ngome yake ya Bonde la Ufa baada ya wabunge na wakulima wa eneo hilo kutaka achunguzwe.

Hilo linakuja huku Ruto akiwa katika mikakati ya kutaka kumrithi Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2022.

Baadhi ya wabunge, wakulima na wazee wa Bonde la Ufa Kaskazini walieleza wazi kutoridhishwa kwao na namna Ruto anavyoshughulikia suala hilo la mahindi.

Kilimo cha mahindi na mtama ni shughuli kuu za wafuasi wake wengi wa eneo hilo, lakini baadhi yao wanahisi hakufanya kila linalowezekana kwa uwezo wake kushughulikia matatizo yao.

Wakulima wameendelea kulalamika bei ndogo ya mazao yao na kucheleweshwa kwa malipo ya mahindi waliyowasilisha kwa Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao (NCPB).

Wakizungumzia suala hilo, wabunge hao wa Chama tawala cha Jubilee; Alfred Keter (Nandi Hills), Joshua Kutuny (Cherangany) na Silas Tiren (Moiben) walitoa mwito Ruto achunguzwe kwa kashfa za mahindi na mbolea zilizoikumba nchi huko nyuma.

“Tunachojua ni kwamba matatizo haya yamesababishwa na Ruto na ofisi yake,” Keter, ambaye ni mkosoaji wa muda mrefu wa Ruto alisema bila kufafanua ushahidi wa madai hayo.

Kutuny alikumbushia kuwa Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri aliwahi kueleza kuwa watu wenye nguvu wanahusika na kashfa ya mahindi na hivyo Ruto anapaswa kuchunguzwa.

“Tunataka Ruto achunguzwe kwa sababu tumesikia amekuwa akiwapigia simu maofisa wa NCPB akiwaagiza juu ya nani wanaopaswa kulipwa fedha,” mbunge huyo alidai.

Wabunge hao walikuwa wakizungumza mkutanoni mjini Eldoret kujadili namna ya kukabili changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wabunge wa zamani Jesse Mais (Eldoret South) na Luka Chepkitony (Keiyo North).

Hata hivyo, washirika wa Ruto akiwamo Seneta wa Nandi, Samson Cherargei waliwakosoa wakulima na wabunge hao kwa kuingiza siasa katika suala la mahindi.

“Hatupaswi kumlaumu Ruto sasa na kuhusu suala la mahindi ni wajibu wake kulinda wakulima wote,” alisema na kuongeza;

‘Wabunge wanaotoka ukanda wa mahindi, ndio wanaowaangusha wakulima kwa kutounga mkono hoja za Serikali za kuongezewa fedha swerikali kununua mahindi kutoka kwa wakulima.”

Wiki iliyopita ilielezwa kuwa watu 62 watafikishwa mahakamani kwa kuwasilisha mahindi isivyo halali kwa NCPB na kulipwa mamilioni ya shilingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles