29 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

VYAKULA VYA KUSINDIKA KIENYEJI VINAWEZA KUATHIRI INI

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


UTAMADUNI wa kusindika vyakula hasa vya nafaka umekuwapo tangu enzi na enzi hadi sasa.

Vyakula kama vile karanga, mihogo, mbogamboga na vinginevyo vimekuwa vikisindikwa kwa njia ya kienyeji hasa kuanikwa juani.

Pamoja na kwamba ni utamaduni unaosaidia kuhifadhi chakula hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema ikiwa havitasindikwa vizuri vinaweza kusababisha mtu kupata magonjwa ya ini.

Hivi majuzi, MTANZANIA lilifanya mahojiano maalumu na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini, John Rwegasha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambaye ameeleza kwa kina kuhusu suala hilo.

Dk. Rwegasa anasema vyakula vilivyosindikwa kienyeji hutoa fangasi (afro-toxin) ambayo iwapo mtu akila chakula hicho huwala fangasi hao.

“Utaona mwanzo chakula kilikuwa na mwonekano wa rangi nyeupe lakini kinageuka kuwa cheusi, wale ni fangasi na mtu anapokula chakula hicho huwala wale fangasi na huingia mwilini mwake na ikiwa atakula wakiwa hai huwa wanatoa sumu,” anasema.

Anasema zipo tafiti ambazo zimewahi kufanyika katika mikoa ya Tabora na Shinyanga ambazo zinaonesha matatizo ya ini yalitokana na ulaji wa vyakula vilivyosindikwa kienyeji.

Daktari huyo anasema wakati mwingine mtu huweza kupata tatizo la ini kutokana na vinasaba vyake.

 

Hatari kuliko Ukimwi

Ugonjwa wa homa ya ini unatajwa kuwa hatari zaidi ya Ukimwi, uwezekano wa mtu kupata maambukizi ya virusi vya homa ya ini ikiwa atajamiiana na mtu mwenye virusi hivyo ni mara 10 zaidi ikilinganishwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.

Inaelezwa, homa ya ini ni hatari huku njia za maambukizi ni kama zile za maambukizi ya VVU na ikiwa mtu hatapata matibabu mapema huweza kuvisambaza virusi hivi kwa kasi kubwa mno kwa wengine.

Dk. Rwegasha anasema takwimu zinaonesha watu wanane kati ya 100 nchini wana maambukizi ya Virusi vya Homa ya Ini hususan Hepatit B.

“Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania imepewa kiwango cha asilimia tano cha maambukizi. Tunacho pia kiwango cha Kitaifa ambacho ni asilimia tano hadi 17,” anasema.

Anaongeza: “Kuna makundi ambayo yapo katika hatari ya kupata maambukizi wakiwamo watu wanaoishi na maambukizi ya VVU wenyewe kiwango chao ni asilimia 17, kundi la wajawazito wana kiwango cha asilimia tano.

 

Takwimu za WHO

Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), vifo vitokanavyo na ugonjwa wa homa ya ini duniani vinaongezeka ambapo mwaka 2015 kulikuwa na vifo milioni 1.34.

WHO linaeleza idadi hiyo ya vifo ilikuwa sawa na vile vilivyotokana na ugonjwa wa kifua kikuu na zaidi ya vile vilivyotokana na ugonjwa wa Ukimwi ambavyo vilikuwa vifo milioni 1.1.

Shirika hilo linaeleza mwaka 2015, kulikuwa na maambukizi mapya milioni 1.75 kwa watu wazima kutokana na virusi vya homa ya ini aina ya C na kwamba vilichangiwa na matumizi ya sindano yasiyo salama.

 

Wanaume hatarini

Dk. Rwegasha ambaye ni miongoni mwa wataalamu waliokwenda nchini India kujifunza jinsi ya kufanya upasuaji wa kupandikiza ini, anasema wanaume ndiyo kundi lililopo hatarini zaidi kupata maambukizi ya ugonjwa huo kuliko wanawake.

“Hapa hospitalini, kati ya wagonjwa wanaolazwa wodini tunaowatibu magonjwa ya ini, asilimia 60 ni wanaume na 40 ni wanawake,” anabainisha.

Anasema hiyo inatokana na baadhi ya wanaume kuwa na tabia hatarishi zinazowasababisha kupata magonjwa hayo ikiwamo  unywaji pombe hasa zile zisizothibitishwa ubora wake.

“Baadhi ya wanaume wana tabia ya kuwa na uhusiano na wanawake zaidi ya mmoja, ni hatari ikiwa anakutana na ambaye ana maambukizi ya virusi hivi basi huambukizwa kwa urahisi,” anabainisha.

Anasema katika kitengo hicho asilimia 60 ya wagonjwa wamepata matatizo ya ini kutokana na kupata maambukizi ya Virusi vya Homa ya Ini.

 

Makundi mengine

Anataja makundi mengine ambayo yanapaswa kupewa chanjo ili kudhibiti kiwango cha maambukizi kuwa ni wanaojidunga dawa za kulevya, wanaofanya biashara ya ngono na mengineyo.

“Duniani, takwimu zilizotolewa na WHO zinaoonesha kati ya watu bilioni mbili waliogundulika na kutibiwa virusi vya homa ya ini, 450 bado wanaishi navyo,” anasema.

Kwa mujibu wa WHO kila mwaka watu milioni 1.5 hufariki dunia kwa maambukizi ya virusi vya homa ya ini na kila mwaka kunagundulika kesi mpya milioni nne za watu wenye virusi hivi.

 

Chanzo saratani ya ini

Anasema tafiti zinaonesha asilimia 60 hadi 80 ya saratani ya ini zinazogundulika duniani huwa zimetokana (zimesababishwa) na maambukizi ya virusi hivyo.

“Changamoto tunayoiona ni kwamba wakati unatibu wagonjwa bado kunajitokeza maambukizi mapya, vifo na kuna makundi ya watu ambayo huwa ni carrier (wabebaji) wa virusi hivi ambao huvisambaza kwa kasi kwa wengine,” anasema.

 

Kuhusu upandikizaji

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha anasema:

“Jopo la wataalamu lililokwenda India lina madaktari bingwa wanne wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, wauguzi wawili wanaosimamia mifumo ya hadubini na mhandisi wa vifaa tiba anayesimamia mitambo ya hadubini,” anabainisha.

Anasema mafunzo hayo yatachukua miezi mitatu na wataalamu hao watarejea nchini wiki ya kwanza ya Machi, mwaka huu.

Anasema pindi watakaporejea wataongeza ufanisi katika uchunguzi na tiba ya magonjwa ya ini, kutoa mawe, kuzibua mifereji ya nyongo na kongosho iliyozibwa na uvimbe.

“Tutaweza kufanya upasuaji wa ini kuondoa uvimbe mkubwa unaodhoofisha afya na kutishia maisha ya wagonjwa, aidha lengo kubwa ni kujenga uwezo wa ndani kwa muda mfupi utakaowezesha kufanyika kwa upandikizaji wa ini kwa wagonjwa wenye mahitaji haya,” anasema.

Aligaesha anasema hatua hiyo imelenga pia kutekeleza adhima ya serikali kwa vitendo ya kupunguza rufaa za nje ambazo serikali ilikuwa ikigharamia fedha nyingi kutibu magonjwa hayo.

Kupitia taarifa aliyotolewa mapema, mwaka jana kwa vyombo vya habari Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema kwa Tanzania tafiti na takwimu chache zilizopo zinaonyesha uwepo wa maambukizi ya virus vya Hepatitis B na C.

“Kwa mfano, kati ya wachangiaji damu 200,000 kwa mwaka 2016, asilimia 6 kati yao (takriban watu 12,000) walikuwa na maambukizi ya Hepatitis B,” anabainisha.

Anasema tafiti zinaonyesha kuwa, kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini homa ya ini inayosababishwa na virusi vya aina B (Hepatitis B) inakadiriwa kuwepo kwa asilimia 16-50.

“Kwa upande wa homa ya ini inayosababishwa na virusi aina ya C (Hepatitis C) inakadiriwa kuwapo kwa asilimia mbili miongoni mwa wanajamii.

“Aidha, maambukizi ya Homa ya Ini ya aina ya B na C (Hepatitis B na C) ni tatizo kubwa miongoni mwa watu wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi,” anasema.

 

Matibabu

Waziri Ummy anasema gharama ya kutibu ugonjwa huo ni kubwa hivyo ni vema jamii ikajikinga kuuepuka.

“Kinga ni bora kuliko tiba, tiba kwa wagonjwa waliopata kirusi aina ya A na E, mara nyingi hutolewa kutokana na dalili zinazoambatana na ugonjwa huu,” anasema.

Anasema kwa wagonjwa waliogundulika kuwa na Hepatitis B au C, matibabu hutegemea hatua mgonjwa aliyofikia.

“Wakati mwingine magonjwa hulazimika kupewa dawa za kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa huo kwa kipindi chote cha uhai wake,” anasema.

Anaongeza” “Gharama za dawa hizi ni kubwa sana. Kwa mgonjwa aliyepata maambukizi ya Homa ya Ini kupitia Virusi aina ya C, gharama ya dawa ni kati ya Sh milioni tatu hadi tano kulingana na muda wa tiba.

 

Mradi maalumu

Anasema serikali kupitia mradi maalumu wa awali (Hepatitis B and C Pilot project), inatoa matibabu bila malipo kwa wagonjwa walioathirika na ugonjwa huo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

“Lakini hadi sasa hakuna dawa maalumu inayotumika kutibu virusi vya  aina ya Hepatitis D,” anabainisha.

 

Jinsi ya kujikinga

Waziri huyo anasema ugonjwa huo unaweza kukingwa kwa kutumia chanjo ambayo hutolewa kwa mtu asiye na maambukizi ya virusi hivyo.

“Kwa maambukizi ya kirusi aina ya B, chanjo ya ugonjwa huo hutolewa kwa mtu asiye na maambukizi ya virusi hivyo na hutoa kinga kwa kipindi chote cha maisha yake,” anasema.

Anasema hapa nchini chanjo hiyo kwa sasa hutolewa kwa watoto wachanga bila malipo.

“Chanjo hii ilianza kutolewa kwa watoto wachanga nchini waliozaliwa kuanzia mwaka 2003 ipo kwenye mchanganyiko wa Pentavalenti.

“Hadi kufikia mwaka 2015, inakadiriwa asilimia 97 ya watoto wote waliozaliwa kuanzia mwaka 2003 walipata chanjo hiyo,” anasema.

Anasema chanjo ya Hepatitis A ipo na inatumika kwa baadhi ya nchi lakini hapa nchini kwetu hatujaanza utaratibu wa kutoa chanjo hiyo kwa sababu tatizo kubwa zaidi linalotukabili kwa sasa ni Hepatitis B.

“Hakuna chanjo dhidi ya  Hepatitis C, D na E.  Hata hivyo ugonjwa wa Hepatitis D unaweza kuzuilika kwa kuwachanja watu dhidi ya Hepatitis B.

“Kama wajibu wa waajiri kuwakinga watumishi wao sehemu za kazi, chanjo ya kuzuia maambukizi ya Hepatitis B hutolewa kwa watumishi wa sekta ya Afya kwa gharama ya serikali.

“Lakini pia ni vema jamii ikaepuka kujidunga madawa ya kulevya, kuepuka ngono zembe pia kwani ni miongoni mwa njia zinazotajwa kuchangia mtu kupata ugonjwa huu,” anasema na kuongeza:

“Katika hatua za mwishoni mwathirika wa ugonjwa huu anaweza kupata saratani ya ini hivyo ni vema kujikinga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles