23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Viwanja vibovu vinapoteza ladha ya mpira wa kikapu

basketball1NA THERESIA GASPER, DAR ES SALAAM

MCHEZO wa mpira wa kikapu ni miongoni mwa michezo iliyojikusanyia umaarufu mkubwa duniani.

Tunaweza kusema kuwa mchezo huu unashika nafasi ya pili ukiachilia mpira wa miguu ambao unaongoza kwa kuwa na mashabiki lukuki.

Timu ya Savio si ngeni masikioni mwa Watanzania wengi na ikiwa tayari imefanikiwa kuchukua ubingwa Mkoa wa Dar es Salaam mwaka huu.

Savio imeweza kuchukua ubingwa mwaka huu, baada ya miaka miwili kupita ambapo mara ya mwisho timu hiyo kuibuka bingwa ilikuwa ni 2013.

MTANZANIA limefanya mahojiano na kocha mkuu wa timu hiyo, Is’haka Masood ambaye anaeleza mambo mbalimbali yanayohusu mchezo huu.

MTANZANIA: Kikosi chako kimefanikiwa kuchukua ubingwa wa mkoa mara ngapi?

MASOOD: Hii ni mara yetu ya tatu kuibuka mabingwa, kitu ambacho tunahitaji kiendelee ili tuitangaze Tanzania vema kupitia mchezo huu na wachezaji wetu wapate soko kimataifa.

MTANZANIA: Timu gani tishio kwenu na mmekuwa mkionyesha upinzani mkali hapa nchini.

MASOOD: Sisi kwetu kila timu ni mpinzani wetu, jambo ambalo limekuwa likitufariji kwani zimekuwa zikipata wakati mgumu pindi tunapocheza nazo.

MTANZANIA: Unamzungumziaje  Hashim Thabit na mipango yenu kuhakikisha tunapata wachezaji wengi watakaolitangaza taifa katika timu za mpira wa kikapu nje ya nchi.

MASOOD: Kwanza najivunia nchi yangu kuwa na mchezaji ambaye anatuwakilisha kimataifa kupitia mchezo huu.Ili Tanzania iendelee kuuza jina kupitia lazima ikubali kufadhili mashindano mbalimbali na kuwawezesha wachezaji wetu kuonyesha vipaji vyao kwenye michuano mikubwa duniani.

Anasema wachezaji wetu wakipata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa na kufanya vizuri wataweza kusajiliwa katika timu za nje.

MTANZANIA: Unazungumziaje ufinyu wa viwanja vya mchezo huu hapa nyumbani.

MASOOD: Ningependa kuona siku moja na sisi tunacheza katika viwanja vyenye viwango vizuri kama nchi za wenzetu, kwani vile tunavyovitumia hivi sasa vinachangia ladha ya mchezo huu kupotea kutokana na ubovu.

Itapendeza zaidi endapo mashabiki pamoja na wapenzi wakaja kuangalia mchezo huu wakiwa wamekaa katika viti vizuri na mandhari nzuri, viwanja vyetu ni vibovu havina mpangilio maalumu.

MTANZANIA: Nini kifanyike kuzuia fujo ambazo zimekuwa zikitokea mara nyingi na kupelekea mechi kuvunjika.

MASOOD: Ulinzi uongezwe, wengi wanaamini mchezo huu umekuwa ukichezwa kwa amani lakini wanakosea, pia nidhamu ndogo ya wachezaji wasiojitambua imekuwa ni sababu kubwa inayoleta vurugu uwanjani.

Anasema anaependa kuona kunakuwa na ulinzi wa kutosha kama ilivyo kwenye mchezo wa mpira wa miguu.

MTANZANIA: Ni changamoto gani ambazo mnakumbana nazo katika timu yenu pamoja na mpira wa kikapu kwa ujumla?

MASOOD: Kiukweli changamoto ni nyingi lakini kubwa timu yetu haina ufadhili kitu ambacho kinatugharimu sana, wachezaji wanatumia fedha zao binafsi.

Kama unavyofahamu mchezo huu unawapenzi wengi sana kama mpira wa miguu, basi ni vema serikali ikatupia jicho na huku angalau na sisi tupate wafadhili au hata kufanya kampeni ambazo zitaweza kuungatangaza.

MTANZANIA: Unatoa ushauri gani kwa wadau wanachama pamoja na wapenzi wa mchezo huu?

MASOOD: Kwanza kabisa mchezo huu upewe kipaumbele ili vijana waweze kujiajiri, vile vile ningependa kuwaomba wanachama na wadau kuweka viingilio, kwani mara nyingi mashabiki wanaokuja uwanjani kuangalia mechi wanaingia bure.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles