22.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kisena wa UDA alipuliwa

kisena*Ni kuhusu mkataba tata wa mradi wa DART

* Waziri asema alifanya vitu kwa ujanja ujanja

Na Florian Masinde, Dar es Salaam

WAKATI hatima ya mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Entrprises na Jeshi la Polisi bado ipo gizani, Serikali imenusa harufu ya ufisadi katika mkataba unaoihusisha Kampuni ya Simon Group, inayomilikiwa na mfanyabiashara, Robert Kisena.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene, ameeleza namna mchezo mchafu ulivyotawala katika zabuni ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).

Kwa mujibu wa Simbachawene, zabuni iliyotangazwa ilipaswa iwe katika mfumo wa kimataifa, lakini katika hali ya kushangaza Kampuni ya Simon Group ilianza maandalizi ya kuendesha mradi huo kinyume cha utaratibu.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Simbachawene, alisema Serikali ililazimika kuingilia kati suala hilo kwa lengo la kujiridhisha kuhusu zabuni hiyo.

Alisema katika hatua hiyo, Serikali ilibaini utata katika mkataba wa kampuni hiyo, kwani kila kitu kilikuwa chini ya Simon Group ambao ni wamiliki wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).

“DART katika kumpata mwekezaji ilitangaza tenda kutokana na maoni mbalimbali ambapo ilitakiwa kutangaza kimataifa (International tender),  lakini ikafanya tofauti na maoni ya watu na kuipa Kampuni ya Simon Group kuendesha mradi huo.

“Kampuni ya Simon Group iliendelea kufanya maandalizi kwa ajili ya mradi na sisi tukaendelea kufuatalia uhalali wa mikataba waliongia na DART ili kuona ni jinsi gani huu mradi uanze, ndipo tulipokwenda halmashauri ya jiji na kuona namna walivyojipanga kushirikiana na wakala kwa ajili ya kusimamia mradi.

“…lakini tulichokikuta pale kila kitu kipo chini ya Kampuni ya Simon Group kwa kuwa wao ndio wamiliki wa Shirika la UDA na wamenunua hisa zote za shirika hilo, ndipo tulipo ulizia zile hisa ambazo haziuzwi bila wana hisa sambamba na kutaka kujua kama fedha zimeshalipwa ndipo napo tukagundua hakujalipwa hata senti tano na haijulikani ni nani kapokea zile hela,” alisema Simbachawene.

Alisema baada ya kufungua nyaraka walibaini tena kuwa hata mwanahisa haruhusiwi kuuliza juu ya ununuzi huo wa hisa.

“Hapa niliona kuna tatizo kubwa ndipo ikaja kubainika kulikuwa na ujanja sana katika kuingia mkataba na hivyo nikachukua jukumu la kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa DART, Asteria Mlambo kwa kuwa hata huyo Simon Group hakuwa mmliliki halali wa UDA na mradi ungekuwa hauko katika mikono ya mtu salama,” alisema.

Utata wa mabasi

Simbawene alisema baada ya hatua hiyo ya awali walihoji hatua ya uwezo wa mabasi ambapo walibaini tena mabasi aliyokuwa ameingiza yalikuwa 140 ingawa hayakuwa yamelipiwa kodi sambamba na vifaa vingine vya mradi huo.

“Kiukweli kampuni hii ilikuwa ikifanya vitu kiujanja na mradi ungeendelea kuchelewa. Kutokana na hali hiyo tuliamua kurudi kwa Rais (Dk. Magufuli), tukajadiliana naye ambapo licha ya kukasirika jinsi mchakato ulivyokuwa aliagiza kuondolewe kwanza kasoro hizo hata kama mradi utachelewa. Ndipo tuliporudi kwa huyo Simon Group na kukaa naye meza moja kuzungumzia namna mradi utakavyokamilika.

“Tulikuwa hatuna namna zaidi ya kurudi kwake kwa kuwa hapa Tanzania hakuna mtu mwenye uwezo wa kifedha na mzalendo anayemiliki mabasi mengi hivyo tulizungumza naye na kumpa masharti yetu kama Serikali ambayo alitakiwa ayatimize kama mwekezaji.

“Kwanza tulimwambia lazima arudishe zile hisa asilimia 49 zisizohamishika na yeye abaki na asilimia 51 na kutakiwa ziwe zimelipwa kwa kipindi cha miezi mitatu ambapo gharama zake zilikuwa Shilingi bilioni 5.8, kulipia kodi mabasi na vifaa vilinyokuwa havijalipiwa kodi na kuruhusu mfumo wa ukusanyaji kodi kwa njia ya kadi kusimamiwa na Serikali,” alisema Waziri Simbachawene.

Kubanwa

Alisema pamoja na mambo yote hayo ilikubaliwa katika awamu ya kwanza kulipa Sh bilioni 2.5 ambazo alilipa kwa mujibu wa masharti ya Serikali.

Pamoja na hali hiyo, Simon Group iliunda kampuni ambayo itakuwa inaendesha mradi huo ikijulikana kwa jina la UDA-RT na tayari inafanya kazi kwa taratibu za wamiliki wake.

“Katika taarifa niliyopokea baada ya kikao chetu cha Machi 31, mwaka huu maagizo yote ametimiza na mradi utaanza kufanya kazi ifikapo Mei 10, mwaka huu.

“Ili uanze kufanya kazi kutakuwepo muda wa mafunzo na zoezi la kuajiri wafanyakazi zaidi 100 sambamba na kufanyia majaribio mabasi yote mpaka yawe yametembea kilometa 250 na kukamilisha ujenzi wa vituo vya kuongozea mabasi,” alisema.

Alisema tangu awali iliwekwa misingi katika mikataba kwamba mradi huo ufanywe na sekta binafsi na miundombinu ya mradi itajengwa na Serikali lakini mabasi yatamilikiwa na watu binafsi.

Waziri Simbachawene, alisema aliingiwa hofu na kuhoji watu wa kufanya mradi huo  ingawa katika miji mikubwa yote duniani kampuni zinazotoa huduma zinakuwa na uwezo mkubwa na usiokuwa na shaka.

Kauli ya Kisena

MTANZANIA ilipomtafuta Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena, alisema  kampuni yake haijawahi kuingia mkataba na Serikali katika kuendesha mradi wa DART.

“Ninachoweza kusema kwangu sisi Simon Group hatujawahi kuingia mkataba na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu, ila ndio kwanza nasikia kutoka kwako,” alisema Kisena.

Kauli ya Rais Magufuli

Mwishoni mwa wiki Rais Dk. John Magufuli, alisema kuwa Serikali yake ililazimika kusimamisha kuanza kwa huduma hiyo baada ya kubaini dosari katika mkataba wa mradi ambazo zingesababisha upotevu wa fedha nyingi.

Alisema mradi huo ulikuwa unalenga kuwatwisha wananchi mzigo mzito wa viwango vikubwa vya nauli na kuwahakikishia wananchi wa Dar es Salaam kuwa mabasi hayo yataanza kutoa huduma hivi karibuni baada ya kurekebisha kasoro zilizobainika.

“BRT upo katika hatua za mwisho, tulichelewesha kwa sababu tuliona kulikuwa na utapeli, tukasema haitowezekana tukasimamisha ili hatua zimalizike, kuna watu walitokea wajanja wajanja wakataka share (hisa) za Serikali zipotee, walitaka kuweka utapeli wa ajabu mbele ya Serikali yangu, tukasema hapana,” alisema Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles