Magufuli azua kizaazaa katikati ya jiji

maguuliRAIS Dk. John Magufuli, jana alizua kiazazaa kwa wananchi wa maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam baada ya kuvamia Benki ya CRDB   akitumia gari lenye namba binafsi.

Kiongozi huyo wa nchi   alikwenda katika benki hiyo tawi la Holland akiwa kwenye gari lenye namba binafsi T 182 DFQ   likiwa halina nembo ya Adamu na Hawa wala bendera ya Rais.

Tukio hilo la aina yake ambalo lilichukua dakika 25, lilitokea asubuhi   katika tawi hilo ambalo liko katika makutano ya barabara za Ohio na Samora.

Baada ya Rais Magufuli kufika katika eneo liliko tawi hilo, barabara hizo zilifungwa ndipo aliposhuka kwenye gari hiyo aina ya BMW   na kuingia ndani ya benki hiyo.

Alipokuwa akikaribia kuingia katika benki hiyo,  baadhi ya wateja walijikuta wakikwama kuingia ndani ya benki hiyo baada ya  kuzuiwa na walinzi wa Rais huku huduma ikiendelea kwa wateja waliokuwa ndani.

Baada ya kuingia ndani baadhi ya wateja wa tawi hilo na wananchi wengine, walibaki wakishangaa huku wengine wakijiuliza ilikuwaje kiongozi huyo wa nchi   aingie ndani ya benki kwa staili ya aina yake likiwa ni tukio tofauti na marais waliomtangulia.

Mmoja wa wananchi waliokuwa jirani na benki hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina la James Charles na ambaye ni dereva wa teksi, alisema baadhi ya wananchi waliokuwa kwenye eneo hilo baada ya kuona ulinzi unaimarishwa, walishtuka na mara wakamuona Rais Magufuli akishuka kwenye gari, hali iliyowafanya wafikirie anakwenda kutembelea ofisi yake ya zamani.

“Lakini kufumba na kufumbua tukamuona anaelekea kwenye benki ya CRDB, tukajiuliza vipi Rais leo (jana), kaamua kuwa kama mteja?

“Hata hivyo hatujui kama hiyo ilikuwa inawezekana. Lazima kutakuwa na kitu. Haiwezekani aende akachukue fedha kwa utaratibu ule. Ngoja tusubiri tutasikia amefuata nini,” alisema Charles.

Naye Joyce Godwin ambaye ni mwanafunzi Chuo cha Elimu ya Juu, alisema hatua ya Rais Magufuli kwenda katika benki hiyo  kwa  kushtukiza   kuliwashtua wafanyakazi  ambao walidhani kwenda kwake alikuwa anatumbua majipu.

“Mimi wakati Rais Magufuli anaingia nilikuwapo ndani kwenye foleni nikisubiri huduma. Kwa ujumla kila mmoja wetu alishtuka lakini hatukujua kilichomleta,” alisema.

Baada ya Rais Magufuli kumaliza kazi yake iliyompeleka alitoka na kuingia kwenye gari huku akiwapungia mkono wananchi waliokuwa nje ya benki.

Novemba 6, mwaka jana, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Wizara ya Fedha, Hazina.

Tofauti na ziara za viongozi wengine wakiwamo mawaziri waliowahi kuongoza ofisi hiyo ambao walikuwa wakiingia katika vyumba vya mikutano au ofisi za viongozi, Dk. Magufuli yeye alianza kwa kuingia katika ofisi za watumishi wa kawaida.

Dk. Magufuli aligeuka kivutio kwa wananchi alipotoka katika lango kuu la Ikulu Dar es Salaam kwa miguu, kwenda Hazina kupitia njia ambayo hutumiwa zaidi na wananchi.

Rais alishangazwa kukuta meza sita kati ya nane katika moja ya ofisi hizo zikiwa hazina watumishi, akalazimika kuuliza majina ya watumishi husika na alipoambiwa walikuwapo alihoji walikokwenda akajibiwa kuwa walikuwa wamekwenda kunywa chai.

Huku akionekana kutoridhishwa na majibu hayo, Dk. Magufuli alitikisa kichwa  akisema, “wameenda kunywa chai eee!” na kuondoka ofisini hapo kwenda kwenye ofisi za viongozi wa wizara hiyo.

Alipoingia ndani alifanya kikao cha muda mfupi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile  na makamishna wa fedha na alipotoka taarifa za wizara hiyo zilieleza kuwa Dk. Magufuli aliagiza watumishi wa wizara hiyo inayosimamia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuhakikisha wanaongeza kasi ya ukusanyaji mapato na akaelekeza hasa kwa wafanyabiashara wakubwa.

Novemba 9 mwaka jana, alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako pamoja na mambo mengine alimsimamisha kazi aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi, Dk. Hussein Kidanta.

Machi 10 mwaka huu,  Rais Magufuli alifanya ziara ya kushitukiza katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ambako   aliiagiza benki hiyo kusimamisha mara moja malipo   ambayo yalikuwa yamekwisha kuidhinishwa   na badala yake yarejeshwe Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki.

Taarifa za awali zilieleza kuwa BOT ilikuwa katika mchakato wa kufanya malipo ya Sh bilioni 925.6, fedha ambazo Wizara ya Fedha ilikuwa imetoa idhini zilipwe.

Rais Magufuli aliiagiza Wizara ya Fedha ifanye upya uhakiki wa malipo hayo   kubaini kama walengwa walioidhinishwa kulipwa walikuwa wanastahili kulipwa au vinginevyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here