Makamu wa Pili wa Rais Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemedi Suleiman leo Septemba 6, 2024 amefungua mashindano ya Michezo ya Baraza la Michezo la Majeshi Tanzania (BAMATA), huku akiwataka wananchi kujitokeza kuunga mkono michezo hiyo.
Mashindano hayo yanashirikisha majeshi yote ya Ulinzi na Usalama nchini ambapo itafanyika kwenye Uwanja Jamhuri Mkoani Morogoro.
Aidha ametoa pongezi kwa BAMATA kwa maandalizi mazuri, akielezea umuhimu wa michezo hiyo ikiwa ni pamoja na kupunguza hatari ya kupata maradhi yasiyo ambukiza, kuhamasisha vijana kuacha uhalifu.
Aliyataka majeshi kutumia michezo hiyo kutengeneza umoja na mshikamano huku akisisitiza ichezwe kwa weledi na itumike kama kipimo cha kupima nidhamu ya majeshi yote.
Majeshi yatakayoshiriki michezo hiyo ni pamoja na JWTZ, Polisi, Magereza, Zimamoto, Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na waalikwa ambao ni Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA).
Michezo itakayochezwa ni soka kwa wanaume na Wanawake, mpira wa kikapu, Pete, Wavu, riadha na ulengaji shabaha.