22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

Timu ya wanaume kriketi kushiriki michuano ya Afrika

Na Mwandishi Wetu

Timu ya Taifa ya wanaume ya kriketi ya Tanzania inatarajiwa kushiriki katika michuano ya Kundi A ya Afrika kuwania kufuzu michuano ya Wanaume ya Kombe la Dunia ya T20 inayoandaliwa na Baraza la Kimataifa la Kriketi (ICC) iliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 21-26.

Michuano hiyo ya Kundi A ya T20 ya Afrika, kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Chama Cha Kriketi nchini (TCA) Atif Salim, itahusisha timu za taifa sita.

Salim alisema timu hizo sita zitachuana katika mtindo wa ligi na timu zitakazomaliza nafasi mbili za juu zitafuzu kushiriki hatua inayofuata.

Alizitaja timu hizo kuwa ni Cameroon, Ghana, Lesotho, Malawi, Mali, na wenyeji Tanzania.

Ofisa huyo wa TCA alibainisha kuwa michuano hiyo itachezwa katika viwanja vya Klabu ya Gymkhana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Timu ya taifa ya kriketi ya Tanzania itaanza kampeni yake katika michuano hiyo kwa kukabiliana na Mali katika uwanja wa UDSM Septemba 21.

Katika mechi nyingine iliyopangwa kuchezwa siku ya ufunguzi, Lesotho itachuana na Malawi katika uwanja wa Klabu ya Gymkhana, huku mechi ikitarajiwa kuanza saa 3.30 asubuhi.

Cameroon pia itaanza kampeni yake siku hiyo hiyo kwa kukwaana na timu mwenza kutoka Afrika Magharibi- Ghana.

Timu ya taifa ya Tanzania, katika mechi inayofuata, itachuana na timu kutoka Kusini mwa Afrika- Lesotho- Septemba 22.

Siku hiyo pia itashuhudia Cameroon ikicheza na Mali huku Ghana ikiikabili Malawi.

Timu ya taifa ya kriketi ya Tanzania inaundwa na nahodha Abhik Patwa, Ally Mpeka, Amal Rajeevan, Akhil Anil, Khalid Amiri, Harsheed Chohan, na Johnson Nyambo.

Wachezaji wengine wanaounda timu hiyo ni Jumanne Mohamed, Kassim Nassor, Laksh Bakrania, Mohamed Yunus, Mohamed Kitunda, Sanjay Thakor, na Zafar Khan.

Wachezaji wengine wawili- Mohamed Simba na Seif Athuman- wameteuliwa kama wachezaji wa akiba wa kikosi hicho.

Michuano ya Kriketi ya Wanaume ya Kombe la Dunia ya T20, iliyopangwa kuchezwa mwaka 2026, itakuwa ni michuano ya 10 ya mchezo huo inayosimamiwa na ICC.

Michuano hiyo itaandaliwa na nchi za Sri Lanka na India, ambazo ni baadhi ya magwiji wa kriketi duniani, kuanzia Februari mpaka Machi 2026.

Baadhi ya nchi ambazo zimeshafuzu kushiriki katika michuano hiyo ni timu 12 ambazo zilishafuzu kabla ya Michuano ya Kanda ya Kufuzu.

Nchi hizo ni Afrika Kusini (Afrika), Marekani na West Indies (Americas), Afghanistan, Bangladesh, India (wenyeji wenza), Pakistan, na Sri Lanka (wenyeji wenza) kutoka Bara la Asia.

Nchi nyingine ni washiriki kutoka Kanda ya East Asia-Pacific, Australia na New Zealand, sambamba na wawakilishi wa Ulaya, England na Ireland.

Sri Lanka na India zimefuzu moja kwa moja kushiriki katika michuano hiyo kutokana na kuwa wenyeji.

Timu hizo zitaungana na timu zilizomaliza katika nafasi nane za juu katika michuano iliyopita. Timu hizo pia zimefuzu moja kwa moja.

Timu nyingine zitakazoshiriki michuano hiyo zitapatikana katika Michuano ya Kuwania Kufuzu ya Kanda.

Michuano hiyo inajumuisha timu tatu kutoka Kanda za Asia na East Asia-Pacific, Afrika na Ulaya ambazo zitatoa timu mbili kila mmoja, sambamba na timu moja kutoka Kanda ya Americas.

Michuano ya Kundi A ya T20 ya Afrika itakuwa ni michuano ya pili ya mchezo wa kriketi kufanyika jijini Dar es Salaam msimu huu.

Jiji hilo hapo awali lilikuwa mwenyeji wa michuano ya Daraja la Pili ya Afrika ya Kuwania Kufuzu Kombe la Dunia kwa vijana walio chini ya miaka 19 iliyochezwa kuanzia Agosti 2-11, huku Tanzania ikitwaa ubingwa wa michuano hiyo.


- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles