Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ameweka wazi dhamira ya Tanzania ya kuimarisha ushirikiano wake wa kiuchumi na China.
Pia Rais Dk. Samia amesisitiza umuhimu wa miradi ya miundombinu kama nguzo ya maendeleo ya taifa, akionyesha matumaini makubwa ya kufufuliwa kwa mradi wa reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), mradi ambao China imeahidi kuunga mkono kwa kiwango kikubwa.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 5, 2024 wakati akihutubia mkutano wa tisa wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika Beijing.
Makubaliano hayo, yaliyosainiwa mbele ya Rais wa China, Xi Jinping na Rais wa Zambia Hakainde Hichilema w yanalenga kuboresha miundombinu ya usafirishaji, ambayo itachochea biashara za kikanda na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchumi cha kanda. Hii ni hatua muhimu itakayochangia si tu kuimarisha uchumi wa Tanzania, bali pia kuleta maendeleo endelevu kwa nchi zote zinazohusika.
Katika hotuba yake, Rais Samia aligusia maeneo mengine muhimu ya ushirikiano kama kilimo, biashara, na teknolojia rafiki wa mazingira, akisisitiza kuwa Tanzania iko tayari kutumia fursa hizi kwa ustawi wa taifa.
 Aidha, alifichua kuwa China imepanga kuwekeza yuan bilioni 360 (Sh Trilioni 137) katika Afrika ndani ya miaka mitatu ijayo, fedha ambazo zitalenga kuimarisha miundombinu, kukuza biashara, na kuunda ajira kwa vijana wa Afrika.
Rais Samia alimalizia kwa kusisitiza kuwa ushirikiano wa Tanzania na China utakuwa chachu muhimu katika kuchochea ukuaji wa kiuchumi wa Tanzania na ushirikiano wa kikanda kwa ujumla. Tafsiri ya ushirikiano huu, hasa kwenye miundombinu kama reli ya TAZARA, itasaidia kuzifanya biashara za kikanda kuwa rahisi zaidi na kuongeza kasi ya maendeleo kwa sekta mbalimbali za uchumi.
Hotuba ya Rais Samia inadhihirisha juhudi zake thabiti katika kuimarisha uhusiano wa kimkakati wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania, huku akiweka msingi imara wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China.