31 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

Vinara wa vyeti feki kizimbani

034029571-judge-gavel-judge-court

NA MANENO SELANYIKA, DAR ES SALAAM

WASOMI wawili wa elimu ya chuo kikuu na mfanyabiashara mmoja wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashtaka 132 ya kughushi nyaraka mbalimbali pamoja na kuwa na mihuri ya Serikali.

Wasomi waliofikishwa mahakamani ni Mwamba Mwamba (38) ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) na Mahundi Zubeir (24), mwanafunzi wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma (VETA).

Mwingine ni mfanyabiashara, Ashraf Maumba, mwenye umri wa miaka 37.

Mbele ya Hakimu Respicius Mwijage, mwendesha mashtaka wa Jamhuri Nassoro Katuga aliyewaongoza wenzake Jackson Chidunda na Elia Athanas, alidai kwamba mashtaka yanayowakabili watuhumiwa hao watatu ni kula njama ya kutenda makosa hayo.

Wakili Katuga aliiambia mahakama kuwa tarehe isiyofahamika katika maeneo ya Buguruni, Dar es Salaam watuhumiwa kwa pamoja walikamatwa wakijihusisha na utengenezaji wa vyeti na mihuri ya bandia huku wakitambua kuwa ni kinyume cha sheria.

Aliendelea kusema kuwa watuhumiwa wanakabiliwa na makosa ya kutengeneza jumla ya vyeti 60 vilivyotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) na katika vyeti hivyo kipo chenye namba ACS 0359955 cha mtu anayefahamika kwa jina la Abdulla Mohamed Noor na kwamba ni halali kimetolewa na baraza hilo.

Alivitaja vyeti vingine walivyoghushi katika mashtaka hayo kuwa ni pamoja na cheti kimoja kutoka katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kilichotolewa Novemba 2009 na kimoja kutoka Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT).

Wakili Katuga aliendelea kuieleza mahakama kuwa watuhumiwa wanakabiliwa na makosa ya kughushi mihuri mbalimbali ya Ofisi za Mamkala ya Mapato Tanzania (TRA), Chuo cha Mamlaka ya Bandari, Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na mingine kutoka ofisi mbalimbali za umma.

Aliendelea kuwa mashtaka mengine ni kukutwa na jumla ya kadi za gari 53 zinazoonyesha ni halali kutoka katika ofisi ya TRA. Vyeti vingine saba vimetoka katika Ofisi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na vingine kutoka katika Ofisi ya Msajili wa vizazi na vifo wilayani Sumbawanga.

Watuhumiwa walikana kutenda makosa hayo huku Mwamba na Zubeir ambao ni wanafunzi wakiomba mahakama iwape dhamana kwa kuwa wanajiandaa na mitihani itakayofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

“Mheshimiwa upelelezi wa kosa hili bado haujakamilika ila kulingana na unyeti wa kosa lenyewe kupitia kifungu cha 148, tunaomba watuhumiwa wapewe masharti mazito ya dhamana.

“Pili kwa kuwa suala la kughushi limehusisha ofisi nyeti za Serikali na majina tunaomba wasidhaminiwe kwa kuwa watakapotoka wanaweza kuathiri ushahidi na upelelezi unaoendelea kwa sasa,” alidai Wakili Katuga.

Hakimu Mwijage alikubaliana na maombi ya upande wa Jamhuri na kuipa muda wa mwezi mmoja ili kukamilisha taratibu za upelelezi.

Watuhumiwa wote walirudishwa rumande hadi Agosti 11 mwaka huu kesi yao itakapoanza kusomewa maelezo ya awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles