26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

UZALISHAJI SUKARI TPC WAZIDI MARADUFU BAADA UBINAFSISHAJI

 

Na LYAMUYA STANLEY, MOSHI


TPC Limited ni mojawapo ya mashamba makubwa ya sukari nchini ambalo liko umbali wa kilomita 20 kusini mwa mji wa Moshi.

TPC inazalisha jumla ya tani milioni moja (1,000,000) za miwa kwa mwaka ambazo pia huzalisha tani zaidi ya laki moja (100,000) za Sukari kwa mwaka.

Akilieleza hili Afisa Mtendaji Mkuu wa TPC, Robert  Baissac wakati wa mahojiano na Mtanzania katika ofisi yake iliyoko TPC zamani ikijulikana kama Arusha Chini hivi karibuni.

Akitoa historia fupi ya TPC alisema ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1930 kwa jina la A / S Tanganyika Planting Company Limited na A.P. Moller mfanyabiashara wa Denmark na kuongeza kuwa kampuni hii ilisajiliwa rasmi nchini kama TPC Limited tarehe 29 Juni 1973.

“Miwa ilianza kuvunwa mara ya kwanza Arusha Chini mnamo mwaka 1936, wakati ambapo tani 4,000 za sukari zilizalishwa. Uzalishaji uliongezeka hatua kwa hatua kadri miaka ilivyosonga mbele na ilipofika mwaka 1974/75 jumla ya tani 50,978 za sukari zilizalishwa.

Mnamo mwaka wa 1979, mbia (AP Moller) aliamua kujiondoa kwenye biashara na kuamua kuuza hisa zake zote katika Kampuni kwa serikali ya Tanzania na Januari 1, 1980 serikali ilinunua hisa zote na kuziweka chini ya Shirika la Maendeleo ya Sukari nchini (SUDECO),” alisema.

Akizungumzia juu ya jinsi zoezi la ubinafsishaji lilivyotokea alisema ilipofika Machi 2000, TPC Limited ilikuwa imebinafsishwa kwa Shirika la Uwekezaji wa Sukari likijulikana kwa lugha ya Kiingereza la Sukari Investment Limited (SIL) ambayo ilinunua jumla ya hisa asilimia sabini na tano (75%) katika Kampuni ambapo 25% iliyobaki ilishikiliwa na serikali.

Kuhusu ni nani anamiliki SIL alisema SIL imesajiliwa nchini Mauritius na kwa pamoja inamilikiwa na Kampuni ya Mauritius, Alteo Limited, na kampuni ya Kifaransa inayojulikana kama Tereos Ocean Indien.

“Ubinafsishaji wa TPC imekuwa moja ya hadithi za mafanikio ya serikali katika miaka kumi na saba (17) ya kazi (2000-2017) ambayo imeshuhudia ongezeko kubwa la uzalishaji Sukari, kuboresha ufanisi na utendaji pamoja na mazingira bora ya kazi na kuongezeka kwa mchango kwa uchumi wa taifa “alisema Bosi huyu wa TPC.

Kulidhihirisha hilo alisema hilo linatokana na ukweli kwamba mchango wa TPC kwa uchumi kupitia kodi kama vile kodi ya huduma (Service Levy), VAT, PAYE na kodi ya maendeleo ya shule zilifikia jumla ya shilingi bilioni 68.4 mwaka 2017 ikilinganishwa na shilingi bilioni 1.6 zilizorekodiwa mwaka 2000.

“Ninafurahi kusema kwamba mchango wa TPC Limited kwa serikali (gawio) ulikuwa kati shilingi bilioni 13.429 bilioni mwaka 2017” alisema na kuongeza kuwa gawio kwa serikali tangu mwaka 2004 hadi sasa ni jumla ya shilingi bilioni 74 .

Katika mazingira bora ya kazi alisema TPC ina wafanyakazi 3,000 katika orodha yake ambapo wafanyakazi 1,900 ni wa kudumu na 1,100 wa msimu na mkataba na kuongeza kwamba kama nyongeza kampuni yake inatoa ajira 1,000 kupitia wakandarasi wanaofanya kazi ya kuvuna miwa.

“Mbali na kuwalipa wafanyakazi wake mishahara ya kima cha chini ambayo huwa zaidi ya kima cha chini kilichowekwa katika sekta ya kilimo (kima cha chini kwa Mwezi kikiwa shilingi 191,408 ikilinganishwa na mshahara wa chini wa kisheria katika sekta ya kilimo Shs 100,000) TPC inatoa pia huduma nyingine na mafao mengi kwa wafanyakazi wake ambayo ni juu ya mahitaji ya kisheria,”alisema.

Aliyataja mafao hayo kama malazi kwa wafanyakazi asilimia sabini ( 70%), huduma za afya za bure kwa wafanyakazi na wategemezi ikiwa ni pamoja na wazazi, malipo ya kustaafu ambayo ni mshahara wa mwezi mmoja kwa mwaka wa huduma, bonasi kwa faida zilizopatikana kwa kila mwaka wa fedha (kwa mfano katika 2011/12, wafanyakazi chini ya kiwango cha usimamizi walilipwa jumla ya shilingi 1,078,000 kila mmoja kama faida juu ya bonasi, bonasi ya utendaji kwa wafanyakazi wa juu na mafao ambayo ni malipo  wakati wa mazishi.

Kulingana na yeye mafao mengine kwa wafanyakazi yalikuwa elimu ya msingi ya bure, msaada wa elimu kwa watoto wa wafanyakazi, usafiri wa bure kwa watoto wa wafanyakazi, mashamba kwa ajili ya kilimo cha chakula na mikopo ya baiskeli kwa ajili ya matumizi binafsi ya wafanyakazi.

Alipoulizwa kuhusu jinsi mafanikio haya yote ya TPC yalivyopatikana , alisema kuwa hayo yote ni kutokana na kwamba tangu ubinafsishaji mwaka 2000 uwekezaji mwingi ulifanyika  TPC ukilenga katika kiwanda na kwenye kilimo hususani kuboresha na kupanua kilimo cha umwagiliaji.

“Mpaka Juni 2018 jumla ya shilingi bilioni 201 zilikuwa zimewekezwa katika ukarabati na upanuzi wa Kampuni tangu ubinafsishaji mwaka 2000” alisema Mkuu huyo wa TPC huku akiongeza kuwa uwekezaji huo mkubwa ulipatikana kupitia fedha za ndani pamoja na mikopo kutoka kwa benki za ndani ya nchi.

Aliongeza kuwa uwekezaji huo hapo juu pia umechangia kuongeza nishati kutoka 9GWh hadi 75GWh kwa msimu ambao unatosha kutosheleza sio tu mahitaji yote ya kiwanda na umwagiliaji lakini pia kwa maeneo yote ya makazi ya TPC huku ukiacha jumla ya Megawati 2 hadi2.5 kwa mauzo ya nje kwa gridi ya kitaifa kuongezeka kwani tangu mwaka 2010, jumla ya Gega Wati kwa saa arubaini na tatu (43GWh) zimetolewa kwa TANESCO.

Katika masuala yanayohusiana na uhifadhi wa mazingira alisema kampuni yake inafanya mifumo bora ya umwagiliaji na upanuaji wa mifereji , uzalishaji wa 100MKWh ya nishati mbadala safi, mashamba ya miti ya majani ya asili na ulinzi na uhifadhi  wa hekta 4,400 za msitu wa asili kutokana na uharibifu.

Alipoulizwa ni wapi TPC inauza sukari yake, alisema yote inauzwa kwenye soko la ndani katika maeneo kama vile mikoa ya  Kilimanjaro, Arusha na Manyara tani 70,000, mikoa ya Tanga na Singida tani 30,000 na kuongeza kuwa juu ya yote anafurahia kuona bei ya sukari ikiwa imara katika soko ( stable sugar prices) tangu mwaka 2016.

Akiongelea changamoto zinazoikabili kampuni yake alisema TPC ina jumla ya hekta 16,000 ambapo zaidi ya hekta 8,000 hutumiwa kulima miwa ambapo sehemu kubwa ya ardhi iliyobaki haifai kwa kilimo cha miwa kwa sababu ya hali ya udongo ambao ni wa magadi na sodiki pamoja na upungufu wa maji kwa shughuli za umwagiliaji.

“Changamoto zetu kuu ni vikwazo wakati wa kuagiza mitambo na vifaa kutoka nje ya nchi, ardhi yenye magadi, masuala ya ustadi (reclamation), mchanga mweupe, masuala ya eldana na YSA, haki za maji katika masuala ya maji ya Miwaleni na kuanzishwa kwa kodi mpya , leseni na ada za ukaguzi” alisema .

Katika mipango ya baadaye ya Kampuni yake alisema kwa mujibu wa Mpango wa Biashara wa TPC Kampuni yake ina mpango wa kupanua maeneo chini ya kilimo cha miwa, kuongeza uwezo na ufanisi wa kiwanda, nishati ya majani (biofuels), mimea ya kitambaa, kuanzisha kiwanda cha chupa ,upanuzi wa hifadhi ya asili na uzalishaji na matumizi ya nishati ya jua.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles