23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

‘Utengenezaji bidhaa za mwisho za madini ufanyike hapa nchini’

Na ASHA BANI – BAGAMOYO


MKURUGENZI Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT), Dk. Rugemeleza Nshala, amesema ili nchi inufaike na madini, mafuta na gesi, ni vyema shughuli zote za mnyororo wa thamani, zikiwamo za utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, usafishaji na utengenezaji wa bidhaa za mwisho zifanywe na nchi husika.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa hivi karibuni, katika mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu kanuni na taratibu za kisheria katika masuala ya madini, mafuta na gesi.

Dk. Nshala alisema nchi nyingi za Afrika, ikiwamo Tanzania, zinashindwa kunufaika kutokana na kuziachia kampuni za kigeni kufanya shughuli za uzalishaji nje ya nchi.

“Kama wewe nchi unashiriki kutoa mazao ghafi ni lazima utapunjwa, maana thamani ya mnyororo wa thamani inaongezeka kutoka hatua moja kwenda nyingine.

“Nchi ikiishia kufanya uchimbaji tu basi itakuwa na hali mbaya na hili linaonekana katika mafuta, kwa sasa tunanunua mafuta safi wakati zamani tulikuwa na kiwanda chetu hapa nchini,” alisema.

Dk. Nshala alisema kitendo cha kuua Kampuni ya Tipper, iliyojihusisha na usafishaji wa mafuta, ni kosa kwa kuwa wanufaika kwa sasa ni wale wanaoingiza nchini mafuta safi.

Alisema kampuni kutoka nje ziliishauri vibaya Tanzania ili zijinufaishe na lengo lilikuwa kuiangamiza.

Kuhusu mikataba ya madini ya mwaka  1997, alishauri mazungumzo yaendelee ili kuachana nayo kwa kuwa haina tija.

“Kama nchi itaamua kuachana na mikataba hiyo, basi kampuni zina haki kwenda kushtaki kwa mabaraza ya usuluhishi au ya uamuzi ya migogoro nje ya nchi,” alisema.

Alisema Tanzania ina haja ya kujifunza kutoka Botswana na anayesema hakuna la kujifunza uzalendo wake una shaka.

Dk. Nshala alisema nchi haitakiwi kuridhika na hisa kutoka katika kampuni ndogo, badala yake inatakiwa kupata faida kutoka kwa kampuni mama zenyewe.

“Kama nchi haitakiwi kujiridhisha na kupata faida kutoka kwa kampuni tanzu zinazokuja hapa, badala yake inatakiwa kupata faida kwa kampuni mama, hapa itakuwa imefanya la maana,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles