23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

UTAMADUNI WA WANAUME KUBEBA WAKE, KUKIMBIA NAO

Na Joseph Hiza na Mashirika,

WANADAMU kwa kawaida huitwa wanyama wa kijamii na kila jamii duniani hufahamika kuwa na mila na desturi zake.

Baadhi ya mila na desturi au tamaduni huwa za kawaida katika maisha yetu ya kila siku huku nyingine zikiwa za kushangaza au kuchekesha.

Unaweza kudhani kuwa kutokana na kuenea na kuzidi kuimarika kwa sayansi na teknolojia, tamaduni za aina hizi zitakuwa hazina nafasi tena katika dunia hii. Hapo ni kujidanganya!

Kuna maeneo mengi duniani, ambayo bado wanafuata tamaduni zinazoonekana kuwa kioja lakini pia wakiendelea kuzidumisha katika sehemu ya maisha yao.

Miongoni mwa tamaduni hizo, ambayo ni makusudio ya makala haya ni kitendo cha waume kuwabeba wake zao na kukimbia nao.

Hilo linakuja licha ya kwamba ni kawaida katika maisha ya siku hizi kwa wanaume wengi kulalamika kuwa maisha ni magumu kwa sababu wanahisi kana kwamba wanatembea pia na mzigo wa wake zao mikononi au mgongoni kwa kipindi chote cha safari ya maisha yao.

Wakati kukiwa na wanaume wa aina hiyo wanaolalamikia mzigo wa kuwabeba wake zao, nchini Finland kuna utamaduni, ambao wanaume huwabeba kweli kweli wake zao wa ndoa na kukimbia nao kweli kweli.

Utamaduni huu unarudi nyuma katika zile zama za maharamia maarufu wanaoitwa Vikings.

Ni utamaduni unaoendekezwa kama sehemu ya kukumbuka vitendo vya utekaji nyara vilivyokuwa vikifanywa na wanaume hao wa Vikings.

Maharamia hao walikuwa wakiwateka kwa nguvu wanawake iwe wameolewa au la wakiwabeba mgongoni au kichwani na kuondoka nao.

Huko waliko waliwafanya kuwa wake zao kwa lazima.

Inaaminika kwamba hilo likaenda sambamba na uandaaji wa mashindano ya waume kuwabeba na kutimua nao mbio wake kila mwaka katika miaka ya 1800 ikiwa sehemu ya mashindano baina ya familia nchini humo.

Kwa taarifa Viking ni waliokuwa maharama hatari katika mataifa ya Scandinavia, yaani Finland, Denmark, Norway na Sweden, ambao pia wanakumbukwa mno wakati waliposhambulia na kuiteka nyara pwani nzima ya Ulaya kati ya karne ya nane na 10.

Kwa sasa utamaduni huu wa kubeba wake umekuwa ukifanyika zaidi kama sehemu ya kujifurahisha.

Hata hivyo, licha ya kwamba hutumika kama sehemu ya kujifurahisha, washindani huuchukulia mchezo huo baina yao wa kuwabeba na kukimbia na wake zao kwa uzito mkubwa.

Wameanzisha staili mpya mbalimbali za kuwabeba wanawake na kukimbia iwe majini, barabarani, mbugani, matopeni na kadhalika.

Kuna majaji wanaosimamia mchuano huo na ambao huwa na uamuzi wa mwisho. Zawadi mbalimbali hutolewa kwa washindi ikiwamo pombe.

Utamaduni huu kwa sasa umesambaa katika sehemu nyingine za dunia. Sasa watu katika nchi mbalimbali ikiwamo Marekani huandaa mashindano ya aina hii ambayo moja ya masharti ni mume na mke pamoja na makundi tofauti ya umri na uzito.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles