24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

UJENZI WA VIWANDA NA CHANGAMOTO YA UMEME WA UHAKIKA

NA MWANDISHI WETU-TANGA


MOJA ya ajenda za Rais John Magufuli, ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya uchumi wa viwanda, jambo ambalo linaonekana kupokelewa kwa mwitikio chanya.

Miongoni mwa wafanyabiashara walioitikia wito huo, ni wale wa kiwanda cha nondo cha Unique Steel Rolling Mills, kilichopo mkoani Tanga.

Msimamizi wa Unique Steel Rolling Mills, Jagjeet Singh, anasema kiwanda hicho ni kati ya viwanda vikongwe nchini ambavyo vilianzishwa wakati wa serikali ya awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Nyerere mwaka 1971.

Hata hivyo kiwanda hiki kiliondoka kwenye mikono ya Serikali kupitia sera ya  ubinafsishaji katika serikali ya awamu ya tatu.

Licha ya historia yake hiyo, kiwanda hicho katika siku za karibuni kilishindwa kuendelea na uzalishaji kutokana na kuyumba kwa mtaji.

Ili kukabiliana na hali hiyo, Singh anasema uongozi wa kiwanda hicho umeamua kuomba mkopo wa Dola milioni 5 za Marekani (Sh bilioni 12) benki ili kukifufua upya.

Anasema “sisis hatutumii chuma chakavu kutengeneza nondo kama wengine, sisi tunaagiza bidhaa ijulikanayo kwa kiingereza kama ‘billet’ kutoka Afrika ya Kusini ambayo ndiyo hasa inayotumiwa na viwanda vyote vikubwa vya nondo duniani.

“Nondo inayozalishwa hapa siyo ya kubahatisha, soko tunalo kubwa nala kutosha kwenye mikoa hii ya Kaskazini lakini zaidi Arusha na Tanga yenyewe.”anasema.

Anasema  Mkuu wa Mkoa huo wa Tanga, Martin Shigela, ndiye aliyewasaidia kupata hati ya kiwanda hicho,  ambayo wameitumia kuomba mkopo benki.

“Awali tuliangaika bila mafanikio, uwekezaji wetu ulikwama kwa kukosekana mtaji tulikuwa hatuwezi kupata mkopo benki. Kwa muda mfupi Shigela ametusaidia kupata hati hiyo ambayo tumeitumia kupata mkopo.”anabainisha.

Anasema wakishapata mkopo hupo, watakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 45 mpaka 60 za nondo kwa siku.

Anasema  soko, la bidhaa zao ni katika mikoa yote ya Kaskazini ikiongozwa na Arusha.

“Soko la nondo zetu ni kubwa katika mikoa yote ya Kaskazini na sasa ujio wa mradi mkubwa wa bomba la mafuta na upanuzi wa bandari ya Tanga, ni fursa nyingine huko watahitaji nondo nzuri na bora kutoka kwetu,” anasema.

CHANGAMOTO

Mhasibu wa kiwanda hicho, Sikander Omary, anasema kutokuwepo kwa nishati ya uhakika ya umeme, ni changamoto kwa viwanda vikubwa na hususani vya chuma.

“Sisemi Tanesco hawafanyi vizuri, lakini nawapa angalizo tunapoingia kwa kasi katika uchumi wa viwanda lazima tuhakikishiwe umeme wa uhakika, ambao haukatiki mara kwa mara.

“Kiwanda kama hiki cha nondo, umeme ukipata hitilafu  wakati tuko kwenye uzalishaji, nondo nyingi hukatika na  kusababisha hasara, nondo ikishakuwa kwenye tanuri ikapoa ndani ya sekunde moja, haina kazi tena.

“Ni bahati mbaya viwanda vyote vya chuma havitumii jenereta, kwa hiyo dharula yoyote ya umeme ikitokea ni  hasara kubwa”. anasema Omary.

Kuhusu ajira, mpaka sasa kiwanda kina wafanyakazi 30 lakini matarajio yao ni kuongeza idadi hiyo kufikia 60 watakapoanza uzalishaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles