30.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Uhusiano wa haiba ya mzazi, malezi

dreamstime_m_12445357_compressed

Na Christian Bwaya,

KATIKA mfululizo wa makala hii tunatarajia kujadili uhusiano uliopo kati ya haiba/tabia ya wazazi na namna haiba/tabia hiyo inavyoweza kuathiri vile tunavyolea watoto wetu. Tutaona namna malezi hayo yanavyoathiri tabia na mwenendo wa watoto tangu wanavyozaliwa mpaka wanapofikia umri wa kujitegemea. Tutaonesha kwamba kwa kiasi kikubwa tabia tunazoziona kwetu si za kuzaliwa na wala hazitokei kwa bahati mbaya. Ni matokeo ya haiba na uhusiano wenu na wazazi waliotulea.

Tafiti za uhusiano wa wazazi na tabia za watoto zilianza kufanyika katika kipindi cha vita ya pili ya dunia. Wataalamu wa malezi na makuzi ya mtoto walitafuta kuchunguza tabia za watoto waliokuwa wametengwa na wazazi wao kwa miaka kadhaa katika kipindi cha vita. Watoto hawa walijulikana kama ‘yatima wa vita’ kwa sababu wazazi walikuwa hai lakini hawakuwapo katika maisha ya mtoto kwa muda mrefu.

Matokeo ya tafiti hizi yalionesha kwamba watoto hawa waliotengwa na wazazi kwa sababu ya vita walianza kuonekana kuwa na matatizo kadha wa kadha ya kitabia ambayo kwa kweli yalihusishwa na uchungu wa ‘kupoteza’ wazazi mapema. Kadhalika, matatizo haya ya kitabia yalionekana kuathiri ukuaji wao wa kiakili na kimwili. Ikawa wazi kwamba uhusiano kati ya wazazi ndio msingi wa makuzi ya mtoto.

Baadae tafiti ziliendelea kupanuka na kuchunguza watoto wengine wanaotengwa na wazazi wao kwa sababu nyinginezo zaidi ya vita kama vile kazi, kuhama na kulazimika kumwacha mtoto mahali pengine zaidi ya kule aliko yeye. Hatimaye ikaanza kuwa wazi kwamba watoto wadogo wanaotengwa na wazazi wao kwa sababu yoyote ile hujikuta wakipitia misukosuko mikubwa ya kihaiba inayotokana na hofu ya kupoteza upendo wa wazazi.

Ikafahamika kwamba watoto hawa baada ya kuchoshwa na maombolezo kwa kipindi fulani ambayo hayakufanikiwa kumrejesha mzazi wanayemhitaji, walianza kukabiliana na hali ya kukata tamaa kwa kujifariji na kujilinda binafsi.  Kwa hiyo, watoto wakajenga hali tunayoweza kuiita ‘kumpotezea’ mzazi husika kwa kuvunja mahusiano kisaikolojia. Hapa tuna maana ya mtoto kumwondoa mzazi kichwani ili ajisikie kawaida. Ilipotokea mzazi huyo alirejea na kukutana na mtoto huyo ambaye tayari alimfuta mzazi kichwani mwake, mtoto alionesha hasira kwa kulia, kumkataa mzazi, kugoma kukuhusiana tena au kumganda mzazi kwa hofu ya kuachwa.

Ikawa wazi kwamba hitaji la kwanza na la msingi la mtoto tangu anapozaliwa ni uwepo wa mzazi. Uwepo huu ndio unaojenga msingi wa haiba/tabia mtoto ambayo huongoza namna anavyohusiana na wazazi wake na watu wengine wote. Mpaka hapa ikaanza kuwa wazi kwamba ili mtoto awe na uhusiano mzuri na wazazi wake, kwa kweli anahitaji uhusiano wa karibu na endelevu na wazazi hao tangu anapozaliwa.

Aidha, yalianza kujitokeza maswali kuhoji ikiwa kuwapo kimwili kwa mzazi kunatosha kumfanya mtoto ajisikie salama. Tafiti zaidi zikaonesha kuwa si kweli kwamba uwapo wa mzazi kimwili unatosha. Ikaonekana mtoto anahitaji uwepo na ukaribu wa kihisia na mzazi kwa maana ya mzazi kutambua na kujibu mahitaji ya mtoto kwa wakati anapokuwa na hitaji.

Kwa kutambua matokeo ya tafiti nyingi yanayoonesha nafasi kubwa ya uhusiano wa mzazi na mtoto katika kujenga uelewa wa na afya ya mwili, makala hizi zitajikita katika kubainisha namna uhusiano huo unavyoathiriwa na haiba ya mzazi kuanzia dakika ya kwanza mtoto anavyozaliwa.

Mwandishi ni Mwalimu wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Anapatikana kwa barua pepe [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles