29.3 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Uchaguzi wa ubunge Arusha kuahirishwa

act+death+picNA ELIYA MBONEA, ARUSHA

 

CHAMA cha ACT Wazalendo kimepata pigo baada ya mgombea wake wa Ubunge Jimbo la Arusha Mjini, Estomih Mallah kufariki katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC Mjini Moshi.

Katika hilo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa mujibu wa sheria italazimika kuusogeza mbele uchaguzi wa ngazi ya ubunge.

 

Ilidaiwa kuwa Septemba 6, mwaka huu Mallah alianza kujisikia vibaya wakati akiwa katika mkutano wa mgombea urais wa chama chake, Anna Mghwira na kwamba baada ya mkutano alipelekwa Hospitali ya St. Thomas ya jijini Arusha kwa ajili ya matibabu.

Mallah, ambaye alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu (PB) hata hivyo baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo na hali yake kutoonyesha mafanikio alihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi.

 

Hata hivyo hadi kufikia saa 7 usiku wa kuamkia juzi Mallah, aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Rasilimali Fedha Taifa wa ACT na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, alifariki dunia.

 

Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Jiji la Arusha, Juma Idd, alisema ni kweli mgombea huyo amefariki katika Hospitali ya KCMC alikokuwa amelazwa.

 

“Alfajiri saa 12 Katibu wa Jimbo la Arusha wa ACT Wazalendo, Eliamani Mitivo alinipigia simu kunijulisha taarifa za kifo hicho,” alisema Idd na kuongeza:

 

“Baadaye nilimuomba waniandikie taarifa ya maandishi ili niipeleka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), watakaotoa mwongozo wa nini kinatakiwa kuendelea baada ya hili kutokea,” alisema.

Alisema kutokana na kifo hicho, wapiga kura wa Jimbo la Arusha Mjini watalazimika kupiga kura za wagombea wa udiwani na urais tu, huku nafasi ya ubunge italazimika kufanyika baadaye.

 

“NEC ndio wenye mamlaka ya kupanga tarehe za mchakato wa kumtafuta mgombea ndani ya ACT Wazalendo na baadaye tarehe ya kampeni za wagombea ubunge Jimbo la Arusha,” alisema Idd, ambaye ndiye Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Arusha.

 

Naye Katibu wa Jimbo la Arusha wa ACT Wazalendo, Mitivo akizungumzia kuhusu kifo hicho akiwa ofisi za chama hicho zilizopo Kata ya Levolosi, alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha kiongozi wao.

“Mallah alikuwa ni mlezi wetu, hili ni pigo kubwa sana kwetu, kwani yeye ndiye aliyekipokea chama hapa Arusha,” alisema Metivo.

Marehemu Mallah kabla ya kujiunga na ACT Wazalendo alikuwa Diwani Kata ya Kimandolu kupitia Chadema, ambapo pia aligombea nafasi ya Meya wa Jiji la Arusha kabla ya kutokea sintofahamu baina ya Chadema na CCM.

Hakudumu katika nafasi hiyo ya udiwani, kwani Chadema walimfukuza uanachama yeye na madiwani wenzake watatu baada ya kukubali kufanya mazungumzo ya kumaliza mgogoro wa nafasi ya Meya wa Jiji la Arusha.

Kutokana na kuvuliwa uanachama, Mallah alipoteza nafasi ya udiwani na hivyo kukaa nje ya siasa hadi pale ACT Wazalendo kilipoanzishwa ambapo yeye ndiye alikuwa mwasisi wake katika Mkoa wa Arusha.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles