24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 13, 2024

Contact us: [email protected]

Tumieni takwimu sahihi kupanga shughuli za maendeleo-Dk. Mwigulu

Na Seif Takaza, Singida

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amewataka watendaji wa Serikali kuzingatia matumizi sahihi ya Sensa ya Watu na Makazi katika kupanga Mipango ya Maendeleo.

Dk. Nchemba ameyasema hayo juzi wakati akifungua mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi na watendaji wa Mkoa wa Singida yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Kizaga wilayani Iramba..

“Tuzingatie Takwimu sahihi zilizopo, matokeo ya takwimu itatusaidia sana siku zijazo katika kupanga miradi ya maendeleo kwani zamani sensa ililenga zaidi kujua idadi ya watu,” alisema Dk. Mwigulu. 

Alitoa mfano mdogo wa kutofanya mambo bila takwimu jambo ambalo linasababisha hata wakati mwingine kuwa na walimu wengi katika somo moja huku baadhi yamasomo mengine yakikosa walimu.

Amesema kutozingatia takwimu kumekuwa na dharura nyingi ambazo zimekuwa zikiipa nchi changamoto kubwa huku akitolea mfano wa Serikali ilipolazimika kujenga shule za sekondari za kata nchi nzima kufuatia kuwepo na wanafunzi wengi waliotakiwa kuanza kidato cha kwanza kushindwa kupelekwa shuleni kwa kukosa mahali pa kusoma.

Alisema mambo hayo ya dharula na kutozingatia takwimu yamekuwa yakimpa Rais wakati mgumu akitoa mfano kuwa leo anapelekewa idadi ya ujenzi wa madarasa pengine 100, anayajenga na baada ya siku chache anaambiwa tena idadi ile haikuwa sawasawa hivyo madarasa hayo hayatoshi.

Awali, kabla ya kufungua mafunzo hayo Dk. Mwigulu aliwaomba Watanzania kuendelea kumuombea Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi ambapo kwa muda mfupi aliokaa madarakani ameweza kufanya mambo makubwa ambayo yamemgusa kila Mtanzania.

Akitaja baadhi ya mambo hayo ni ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao ujenzi wake umebakia asilimia 15 ukamilike, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya nchi nzima, kuongeza bajeti ya ujenzi wa barabara za vijijini (TARURA) kutoka Sh.Bilioni 200 hadi kufikia Sh trilioni 1, kuongeza bajeti ya kilimo kutoka Sh bilioni 200 hadi kufikia trilioni 1.20 bajeti ambayo haijawa kufikiwa na awamu zote za serikali zilizopita.

Dk. Mwigulu alitumia nafasi hiyo kuipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) chini ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kukusanya takwimu sahihi kwa ajili ya kukamilisha mipango ya maendeleo nchini.

Aidha, alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhamasisha wananchi katika shughuli za maendeleo na kuifuatilia kwa karibu.

“Hii ni faida kubwa ya kuwa na Mkuu wa Mkoa ambaye aliwahi kuwa mbunge mwenye uwezo wa kujua mahitaji ya wananchi na kuyafanyia kazi anatusaidia hata sisi wabunge wa mkoa huu katika maeneo mbalimbali endeleeni kumpatia ushirikiano,” amesema Mwigulu.

Kwa upande wake, Serukamba alisema mipango na programu zote za maendeleo za mkoa huo zinapangwa kwa kuzingatia matokeo ya sensa hiyo ya Watu na Makazi, Majengo na Sensa ya Anuani za Makazi ya mwaka 2020/ 2022.

Alisema katika mipango na programu za mwaka wa fedha 2023/2024 zimezingatia matokeo ya Sensa na takwimu nyingine zinazozalishwa na NBS na kuwa ili wananchi wa mkoa wa Singida waweze kupata huduma bora, mipango ya mkoa huo itazingatia matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Mtakwimu Mwandamizi, Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mdoka Omary alisema madhumini ya mafunzo hayo ni kusambaza matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2020/ 2022 na kuwajengea uwezo wadau wote na viongozi namna ya kutumia matokeo hayo katika kutekeleza majukumu yao ya uongozi na utendaji katika Serikali kuu na mamlaka ya serikali za mitaa.

Amesema kufanya hivyo kutasaidia kuongeza uwezo na kupanua wigo wa matumizi ya sensa ya watu na makazi kwa serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles