24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Wakazi Sangabuye wanufaika na mradi wa kuboresha makazi, TAHEA yatoa wito

Na Clara Matimo, Mtanzania Digital

WANACHAMA 21 wa kikundi cha Muungano FC katika mtaa wa Imalang’ombe kata ya Sangabuye wilayani Ilemela, Mwanza wamejikwamua kiuchumi kwa kuboresha makazi yao kutokana na kugawana faida za kuweka akiba na mikopo.

Kikundi hicho ambacho ni moja ya vikundi 33 vilivyowezeshwa na Shirika lisilo la serikali linalojishughulisha na Uchumi wa Nyumbani (TAHEA) kupitia mradi wa miaka mitano (2018-2022) wa boresha makazi uliofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la We Effect, wanakikundi hao hugawana wastani wa Sh 315,000 kila mmmoja kwa mwaka, lakini badala ya kugawana fedha hununua vifaa vya ujenzi (saruji na mabati), milango, vyombo vya nyumbani na magodoro ili kujiletea maendeleo yanayoonekana.

Baadhi ya wanachama wa kikundi cha Muungano katika mtaa wa Imalang’ombe kata ya Sangabuye wilayani Ilemela wakiwa wameshika moja ya mlango kwa ajili ya kuwekwa kwenye nyumba ya mwanachama mwenzao, wakati wa sherehe ya kugawana faida za kikundi hicho leo Julai 11,2023.

Akizungumza leo Julai 11, 2023 wakati wa sherehe ya kugawana mafao kwa wanachama, Katibu wa kikundi hicho, Vumilia Mashauri amesema kila mwaka kikundi chao hugawana faida mwezi Julai ambapo wamekubaliana kununua mabati, saruji, milango, madirisha na vyombo vya ndani ili kuboresha makazi yao, huku wakijenga darasa la awali kwa watoto wa kijiji hicho, kuchimba kisima cha maji na kununua kalamu kwaajili ya wanafunzi wasiojiweza.

“Kikundi chetu kilianzishwa mwaka 2014 kikiwa chini ya uelimishaji wa Tahea waliotushauri kuanzisha vikundi tulianza kwa hisa tukaenda kwenye vifaa vya ujenzi na vyombo vya ndani, kwahiyo katika mgao huu kuna wanachama waliotaka mabati, saruji, kuna mwingine ameshamaliza ujenzi hivyo anahitaji vyombo vya ndani hivyo aliyeomba mabati anapata 14, wa saruji anapata mifuko 14, na wengine magodoro mawili,”

“Nyumba yangu nimeshapaua kwahiyo nimeagiza plate mbili za milango ya geti tumefanya hivyo kwa sababu tulipokuwa tukichukua fedha hatunufaiki nazo, tulikuwa na nyumba za majani na tope sasa tuna za mabati na matofali. Nawaomba wananchi wenzangu wanaounda vikundi vya ujasiriamali tujifunze tabia za kuchukua na kurejesha mikopo ili itunufaishe familia ifaidike kwa maendeleo yanayoonekana kwa macho,”amesema Mashauri.

Mwanakikundi, Restuta Malima ambaye alijiunga mwaka 2021 amesema “Nilijiunga baada ya mme wangu kuanza kunipa Sh 2,000 kila wiki na tumefanikiwa kujenga nyumba ya kisasa tulianza kujenga kwa kufyatua matofali kutokana na saruji tuliyokuwa tunagawana kwenye kikundi, leo natarajia kupata mabati 28, nashauri wananchi wenzangu tuwe kwenye vikundi ili kusaidiana na kuleta maendeleo katika jamii,”

Naye, kijana aliyenufaika na kikundi hicho, Majige Samson ambaye katika mgawo huo amepata mabati 14 amewaomba vijana kujiunga na vikundi vya aina hiyo huku akiwataka kutumia vyema faida wanazozipata ili kuleta maendeleo kuliko kuishia kulewa na kufanya mambo yasiyo ya kiungwana.

“Mwanzo tulianza na wanachama 40 tukayumba na kubaki sita lakini tulisimama kidete matunda yakaonekana watu wakashawishika na sasa tupo 21, nilinufaika kwa kununua kiwanja na kujenga nyumba yenye vyumba vitatu na sebule, nafuga bata na nimekuwa na uhakika wa kukopesheka.

Tunashukuru Tahea wanatupa muongozo wa kupata shughuli za kujiinua kiuchumi ili tuweze kumiliki ardhi,” amesema Samson.

Mtoa mafunzo kwa vikundi vya akiba na mikopo kutoka Tahea, Bundala Ramadhan, amesema hatua hiyo ni matunda ya wana ushirika waliohamasishana kutokana na mradi huo ulioanza mwaka 2018-2022, kwani familia ikiwa na makazi bora watoto watapata sehemu ya uhakika ya kulala na jamii kuweza kutoa malezi bora ya mtoto wa awali.

“Vikundi hivi tunaviunda kuanzia wanachama 15-35 ambao wakishasajiliwa wanatengeneza shirika tunawaunganisha chini ya mwamvuli mmoja ili washughulikie kuboresha makazi, hawa ni miongoni mwa vikundi 33 vilivyoanzishwa vingine vinakomea njiani na vinavyofikia ukomavu vinajitegemea zaidi.

“Changamoto tunazoona bado wako nyuma kwenye makazi lakini kwakuwa wamekomaa na wananunua vifaa vya ujenzi matarajio yetu wataboresha makazi yao, kuboresha kipato na kuboresha afya za familia zao. Tunafarijika kuona kikundi hiki bado kina lengo tulilokubaliana, tunawapongeza sana muendelee na utaratibu huo msiishie njiani, kujenga ni hatua endeleeni kukusanya nguvu mtimize malengo yaliyokusudiwa,” amesema Ramadhan.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Tahea linalojishughulisha na elimu, kilimo, nyumba, lishe, afya na kipato ngazi ya familia, Mary Kabati amesema uboreshaji wa makazi unaendana na vitu vingi ikiwamo uhakika wa kipato, chakula, nguvu na afya ambapo wamejikita kwenye kundi la wanawake na vijana ambao ndiyo wenye nafasi kubwa katika kuleta mabadiliko.

“Sisi kama shirika tunaloshughulika na uchumi wa nyumbani tunaona kwamba ili uingize suala la uboreshaji wa nyumba na makazi lazima uwe na kipato kwahiyo tunawafundisha kukaa kwenye vikundi waanze kununua hisa na kuweka kupata mtaji ili wakopeshane na kuwekeza kwenye miradi midogo ya kujiinua kiuchumi mfano kuuza dagaa, mbogamboga, kilimo cha bustani, hivyo ndivyo tunafikiria kumwezesha kijana na mwanamke. Baada ya kumwezesha tunaingiza suala la lishe, wanapofanya shughuli zao za kila siku wasisahau kuzalisha chakula kwa ajili ya familia,” amesema Kabati.

Ameongeza kuwa: “Pia tunawaingizia suala la uboreshaji wa makazi tunawafungua macho kuwa hata mwanamke na kijana anaweza kumiliki ardhi, wanapokuwa kwenye kikundi na kukopeshana basi wanaweza kukusanya kidogo na kununua kipande cha ardhi. Kwenye kuboresha nyumba wanaongeza vyumba, kurekebisha sakafu, kupiga ripu nyumba, kuweka madirisha ambayo yanaingiza hewa safi lakini kuna ambao hawajaanza kabisa na wanahitaji kujenga nyumba ya matamanio yao.

“Tahea na We Effect tunaamini kwamba masuala ya makazi bora yanahamasisha afya bora, kutokuwa na pesa mkononi au mkopo kutoka taasisi za kifedha siyo sababu ya kushindwa bali kujiunga pamoja yote yanawezekana. Wananchi wajiunge kwenye vikundi watafute namna bora ya kuweka na kujikopesha wenyewe, wakiwa kwenye vikundi itakuwa rahisi kufikiwa na elimu na msaada wa uwezeshaji kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo,” amesema Kabati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles