31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

TRA kaa la moto kwa vigogo

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

HOJA kubwa nne ambazo wafanyabiashara walimweleza Rais Dk. John Magufuli juzi juu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zimechangia kwa kiasi kikubwa kung’olewa kwa aliyekuwa Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Charles Kichere na kuifanya taasisi hiyo kuwa kaa la moto kwa vigogo.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana ikiwa ni saa 12 tangu kukamilika kwa mkutano kati ya Rais Magufuli na wafanyabiashara uliofanyika Ikulu na kudumu kwa saa tisa, tangu saa tatu asubuhi hadi saa moja jioni, ilisema nafasi ya Kichere inachukuliwa na Edwin Mhede.

Novemba 20 mwaka 2016, Rais Magufuli alimteua Kichere kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA na Machi 25 mwaka 2017 akateuliwa kuwa Kamishna Mkuu akichukua nafasi ya Alphayo Kidata. 

Kichere anakuwa mtu wa nne kung’olewa kwenye kiti hicho ndani ya miaka minne, akitanguliwa na Rished Bade, Kidata na Dk. Philip Mpango.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Gerson Msigwa, iliyotolewa jana, ilisema Kichere ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe na nafasi yake kuchukuliwa na Mheda ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara.

WAFANYABIASHARA WALIVYOMMALIZA KICHERE

Katika mkutano wa juzi wa Rais Magufuli na wafanyabiashara, TRA ililalamikiwa zaidi na wafanyabiashara.

Malalamiko makubwa yaliyoelekezwa kwa mamlaka hiyo, ni pamoja na kudai kodi kwa kutumia vikosi kazi vinavyoenda kwa wafanyabiashara na mitutu ya bunduki, watumishi wake kuomba rushwa, kukadiria kodi kubwa na kutokuwa na uwiano kwa kodi kwa bidhaa za aina moja zinazoagizwa kutoka nje.

Katika kikao hicho, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa mfano wa mfanyabiashara mmoja ambaye aliombwa rushwa na maofisa wa TRA na alivyokataa kuwapa, walifungia mzigo wake katika bohari kwa miaka mitatu hadi pale yeye alipoingilia ndipo ukatolewa Aprili, mwaka huu.

Mfanyabiashara wa mafuta kutoka Mwanza, Agustino Makoye, alisema ukusanyaji wa tozo ya ushuru wa huduma mkoani humo ni wa vitisho.

Makoye alisema wahusika wamekuwa wakitumia silaha jambo alilodai linakatisha tamaa ya kufanya biashara.

“Wanakuja polisi wakiwa na bunduki na wanakuwa watu wengi, wakati ni ushuru tu ambao unakusanywa na jiji na halmashauri.

“Kwanza ukiwaona tu wakiwa na bunduki wanakufanya ukose raha ya kufanya biashara.

“Tumekuwa na wasiwasi na ukusanyaji huo kwa sababu mfumo si mzuri na tumekuwa tukipewa madai makubwa kuliko mtaji.

 “Wanakuja wanakuambia tangu mwaka 2015 hadi 2017 unadaiwa Sh milioni 200 na wewe una mtaji wa Sh milioni 20. Kwa hiyo Rais  nikuambie ukweli, wananchi hawa  wanachonganishwa na watumishi wasio waaminifu.

“Utakapoambiwa Sh milioni 200 utaambiwa ndani ya siku saba uzilete, utakapozunguka mlango wa nyuma utaambiwa leta Sh milioni 20 na ile ya kwanza haipo,” alisema Makoye.

Naye mfanyabiashara wa mafuta kutoka Singida, alilalamika kuwa biashara zake zimekuwa haziendi kwa sababu ya kodi nyingi hadi amefunga kiwanda chake cha mafuta cha mkoani Arusha.

“Hawa wakusanyaji wa kodi sifa yao kubwa imekuwa ni kufunga viwanda na hawatushauri tunafanyaje ili tusonge mbele.

“Mfano nalipa kodi 41, kila mmoja anataka apewe ushuru. Watu wengi hapa wameongelea ‘service levy’, sasa haya yote nilipie wapi? Hii ni changamoto kubwa, ukiuliza manispaa wanakwambia lipa kila mahali,” alisema. 

WATANGULIZI WA KICHERE WALIVYONG’OKA

Bade ndie wa kwanza kuanza kung’olewa na Rais Magufuli Novemba 27, 2015 kufuatia kasoro za kiutendaji zilizobainika TRA.

Rais alichukua uamuzi huo baada ya ziara ya kushtukiza ya Waziri Mkuu Majaliwa bandarini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, alibaini kuingizwa nchini kwa makontena zaidi ya 300 ambayo hayakulipiwa ushuru na hivyo kusababisha upotevu wa Sh bilioni 80.

Bade aliteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kushika nafasi hiyo Tangu Mei 6, 2014 akichukua nafasi ya Harry Kitilya aliyestaafu Desemba 14, 2013.

Baada ya Bade kuondolewa, Rais alimteua Dk. Mpango kukaimu nafasi hiyo, lakini hakukaa muda mrefu kwani Desemba 23, 2015, alimteua kuwa mbunge na kisha Waziri wa Fedha na Mipango.

Desemba 30, 2015 Rais Magufuli alimteua Eliakimu Maswi kuwa Kaimu Naibu Kamishna wa TRA, lakini naye hakukaa muda mrefu na Januari 2016, alirejeshwa mkoani Manyara kuendelea na kazi yake ya katibu tawala wa mkoa. 

Kuhusu Maswi, Rais alifafanua kuwa amekamilisha kazi aliyokwenda kuifanya katika taasisi hiyo.

Machi 13, 2016, Rais Magufuli alimteua Kidata kuwa Kamishna Mkuu wa TRA. 

Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nafasi aliyoishikilia tangu Agosti, 2013.

Machi 23, 2017 aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu (Ikulu) akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Peter Ilomo ambaye alistaafu. Alidumu katika nafasi hiyo hadi Januari 10, alipoteuliwa kuwa balozi.

Novemba 8 mwaka 2018, Rais Magufuli alitangaza kumrejesha Kidata nyumbani na kumvua hadhi ya ubalozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles