TAMWA YALAANI MAUAJI YA MWANAFUNZI

0
788

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimesikitishwa na kulaani vitendo na matukio ya ukatili uliopindukia, unaofanywa na baadhi ya walimu kuwapiga wanafunzi bila kufuata sheria zinavyoelekeza.

Tamwa imesema vipigo hivyo husababisha baadhi ya wanafunzi kuathirika kisaikolojia na hata kupoteza maisha.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga, ilisema miongoni mwa matukio ya kusikitisha ni lile la Agosti 27, mwaka huu ambalo mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kibeta mkoani Kagera, Sperius Eradius (13), alifariki dunia baada ya kupigwa na mwalimu wake kwa kumtuhumu kumwibia pochi yake.

Alisema tukio jingine ni lile la mwaka 2016 lililotokea kwa msichana wa kidato cha nne (17) aliyekuwa akisoma katika shule moja ya sekondari ya kata mkoani Mbeya, ambaye alivuliwa nguo za ndani na kucharazwa bakora zisizo na idadi kwa sababu za utoro shuleni.

“Tukio hilo limeripotiwa katika Kituo Kidogo cha Polisi Mbalizi, Wilaya ya Mbeya kwenye jalada la uchunguzi namba MBI/IR/967/2016 na kuwekwa kwenye taarifa yenye namba MBI/RB/2653/2016.

“Sheria juu ya viboko mashuleni katika kifungu 61(1)(v) cha Sheria ya Elimu Sura ya 353 marejeo ya mwaka 2002, kinampa mamlaka Waziri wa Elimu kutunga kanuni za masuala mbalimbali zitakazokidhi utekelezaji wa masuala ya sheria hiyo,” alisema Sanga katika taarifa yake.

Alisema kanuni ndogo ya (2) inaelekeza adhabu ya viboko itolewe kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko vinne kwa tukio lolote na ni nani mwenye mamlaka ya kumchapa mwafunzi.

“Tamwa inalaani kwa nguvu ukatili wa aina hii na ni matarajio yetu kuwa vipigo na mauaji mashuleni havitatokea tena.

“Aidha tunamshukuru na kumuunga mkono Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kwa kukemea vitendo hivi kwa wanafunzi pamoja na viongozi wenye mamlaka kuchukua hatua katika matukio haya ambayo yanarudisha nyuma na kukatisha ndoto za wanafunzi, familia zao na hata kudhalilisha taifa letu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here