JAJI MKUU: SHERIA ZILENGE  USTAWI WA WANANCHI

0
655

Na Mwandishi Wetu-Dodoma


JAJI Mkuu, Profesa Ibrahim Hamis Juma,  amewataka wanasheria wa serikali  kuhakikisha sheria wanazozisimamia zinakidhi matarajio ya maendeleo na ustawi wa wananchi maskini.

Aliyasema hayo jana  wakati akifungua mkutano wa  siku mbili wa wanasheria walio katika utumishi wa umma,  unaofanyika  Dodoma.

“Wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote, kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano,  Serikali, Bunge na Mahakama, zinapata mamlaka zao kutoka kwa wananchi.

“Wanasheria katika sekta ya umma hakikisheni  sheria  zinalenga ustawi wa wananchi,” alisisitiza Jaji Mkuu

Mkutano huo unaowakutanisha  mawakili wa Serikali 900 kutoka wizara mbalimbali, idara, taasisi za Serikali na mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Alisema wadhifa mpana wa Wizara ya Katiba na Sheria, unampa waziri upeo mpana wa kuhakikisha sheria za Tanzania zinalenga katika ustawi wa wananchi ambao wengi wao ni wenye hali duni ya maisha.

Akitilia  mkazo  kuhusu sheria  zinazolenga  kuwasaidia wananchi maskini, Jaji Mkuu alisema sheria   hizo lazima ziwasaidie wananchi maskini kunufaika na Malengo ya  Dira ya Taifa ya  Maendeleo ya 2025.

Jaji Mkuu amewataka  mawakili wa Serikali wanaofanya kazi katika sekta ya umma kuhakikisha  ubora wa huduma za  sheria wanazozitoa zinakidhi mahitaji ya  uchumi wa kati.

“Uwakili wa Serikali ni utumishi unaohitaji kuaminiwa na kuaminika, tusitumie kuaminiwa  na kuaminika kwetu kwa maslahi binafsi dhidi ya manufaa binafsi ya umma,” alionya Jaji Mkuu

Amewataka  wanasheria hao walio katika utumishi wa umma na kama washauri wa sheria kwa viongozi mahali pao pa  kazi,  kutumia  ujuzi, weledi na uadilifu mkubwa kutoa ushauri  wao kwa  maslahi mapana ya taifa.

“Muwasaidie viongozi kwa kuwashauri kabla  hawajatoa amri na maagizo mbalimbali ambayo  huzidisha migongano ya sheria na hasara kwa serikali.

Katika hatua nyingine,  amewataka wawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya,madiwani,wakuu wa mashirika ya umma, wakubali ushauri wa sheria kutoka kwa wanasheria wa Serikali.

Alisema endapo  hawaridhishwi na ushauri wao  basi wafuate ngazi za kufuata hadi kupata ushauri kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakili Mkuu wa Serikali.

“Ujumbe wangu kwa mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa  wilaya, madiwani, wakuu wa mashirika ya umma, tukubali ushauri  wa sheria kutoka kwa wanasheria wa Serikali.

“Endapo ushauri huo hauturidhishi, basi zipo ngazi za kufuata hadi kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakili Mkuu wa Serikali,” alisema.

Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa  Palamagamba Kabudi alisema kutokuwapo mfumo rasmi wa kuwakutanisha  wanasheria walioko katika utumishi wa umma, kulisababisha  baadhi ya  wanasheria wa  serikali      kufanya uamuzi usio na  tija kwa taasisi na  taifa kwa kuingia mikataba mibaya.

“Serikali imekuwa ikiingia katika gharama kubwa  ya kulipa mabilioni  ya fedha   inaposhindwa katika mashauri mbalimbali mahakamani kutoka na uamuzi  na ushauri mbaya uliotolewa   na wanasheria waliopo katika utumishi wa umma,” alisema Profesa Kabudi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here