27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 7, 2024

Contact us: [email protected]

TAJIRI WA MJINI AVURUGA MNADA MAHEKALU YA LUGUMI

Na Norah Damian – DAR ES SALAAM


MNADA wa nyumba za mfanyabiashara maarufu, Said Lugumi, umeingia dosari baada ya mnunuzi aliyejitokeza, Dk. Louis Shika, kushindwa kulipa asilimia 25 ya fedha kama taratibu zinavyotaka.

Mnada huo, ulioendeshwa na Kampuni ya Udalali ya Yono chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ulifanyika jana kwa nyakati tofauti maeneo ya Mbweni, Wilaya ya Kinondoni na Upanga Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam ambako nyumba hizo zipo.

Nyumba mbili za Mbweni ambazo kila moja ina ukubwa wa mita za mraba 1,500, ndizo zilizoanza kuuzwa saa 5:58 asubuhi.

Licha ya kuwapo kwa ushindani katika mnada huo, Dk. Shika alifanikiwa kuwazidi wateja wengine waliokuwa wakihitaji kununua nyumba hizo.

Wakati wa mnada wa nyumba ya kwanza, Dk. Shika ndiye aliyeanza kutaja bei. Alianza na Sh milioni 300 na hadi ilipofika Sh milioni 900 akauziwa.

Katika nyumba ya pili ambayo iko jirani na ile ya awali, alianza kutaja bei ya Sh milioni 500, kisha mnada uliendelea hadi ilipofika Sh bilioni 1.1 akauziwa.

 

NYUMBA YA UPANGA

Baada ya kuuzwa nyumba hizo, Dk. Shika alisikika akisema anahitaji pia kununua nyumba ya Upanga, hivyo aliingia katika gari la TRA na kuelekea eneo hilo.

Katika mnada wa Upanga ulioanza saa 7:37 mchana, aliyeanza kutaja bei alikuwa ni mteja mwingine ambaye alianza na Sh milioni 400, kisha akadakia Dk. Shika kwa kutaja Sh milioni 450.

Mnada uliendelea na hadi mwisho, Dk. Shika ndiye aliyeweza kununua kwa Sh bilioni 1.2.

 

MALIPO KIZUNGUMKUTI

Muda mfupi baada ya kununua nyumba hizo, Dk. Shika aliongozana na maofisa wa TRA na wale wa Kampuni ya Yono kwenda kulipa asilimia 25 ya mauzo ya nyumba zote ambayo ni Sh milioni 800.

Mkurugenzi wa Yono, Scholastika Kevela, alisema walipofika benki, Dk. Shika akasema fedha zake zinatoka Kenya, kwahiyo wasubiri awasiliane kwa ‘e-mail’ na wenzake.

Scholastika, alisema awali walimuuliza kama ana fedha za kununua nyumba hizo na yeye aliwajibu anazo.

“Tulimuuliza ana fedha akasema anazo, wateja walikuwa wengi, lakini yeye alishinda nyumba zote tatu ndiyo maana tulimshangilia.

“Hiki si kitu cha kawaida na tumeshtuka, kiuhalisia huyu ameharibu mnada kwa sababu tunachoelewa ni kwamba mtu ambaye yuko ‘serious’, lazima alipe asilimia 25 baada ya kununua na hizo ndizo taratibu za mnada,” alisema Scholastika.

Baada ya mteja huyo kushindwa kulipa fedha hizo, alichukuliwa na askari polisi waliokuwa eneo hilo na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Salender.

Taarifa za ndani zilieleza kuwa baadaye alihamishiwa Kituo cha Polisi Kati kwa mahojiano zaidi.

 

MNADA KURUDIWA UPYA

Kutokana na mnunuzi huyo kushindwa kulipa asilimia 25 ya malipo hayo, Kampuni ya Yono ililazimika kurudia upya mnada wa nyumba ya Upanga na akajitokeza mteja aliyetaka kuinunua kwa Sh milioni 980.

Hata hivyo, ofisa wa TRA aliyekuwapo eneo hilo, alisema mteja huyo bado hajafikia bei elekezi iliyopangwa na Serikali.

“Kama ukiweza kufika Sh bilioni moja tutakuuzia, nenda kaongeze fedha,” alisikika ofisa huyo akimweleza mteja.

Kampuni ya Yono, ilisema itarudia minada yote upya kwa sababu bado wanao wateja walioonyesha nia ya kununua nyumba hizo.

“Tutarudia minada yote kwa sababu wateja bado tunao,” alisema Scholastika.

 

  1. SHIKA NI NANI

Awali kabla hajakamatwa, Dk. Shika alizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa yeye ni daktari bingwa wa magonjwa ambukizi na kwa muda mrefu alikuwa akifanya shughuli zake Ulaya.

“Hapa nchini niliwahi kufanya kazi katika hospitali za Serikali zilizoko Songea na Mbeya, lakini baadaye niliamua kwenda nje.

“Mimi (Dk. Shika), ni rais wa kampuni inayojishughulisha na masuala ya kemikali za viwandani, ambayo makao yake makuu yapo Urusi,” alisema Dk. Shika.

Alisema kampuni hiyo ijulikanayo kama Lancefort, ilianzishwa mwaka 1999 na ina matawi katika nchi za Ujerumani, Uingereza na Hispania na wana mpango wa kufungua tawi hapa nchini.

“Nimekuwa nje kwa muda mrefu, nimekuja nchini kwa shughuli za kampuni, nikimaliza naondoka, tuna mpango wa kuwekeza hapa, hivyo tunatafuta kwanza mahala pa kukaa watu wetu,” alisema.

 

HOTELI BLUE PEARL

Katika hatua nyingine, Kampuni ya Yono, imeifunga hoteli ya Blue Pearl kutokana na kudaiwa kodi ya pango ya Sh bilioni 5.7.

Hoteli hiyo, inadaiwa kodi hiyo na Kampuni ya Ubungo Plaza ambayo inamilikiwa kwa ubia na Shirika la Bima la Taifa (NIC), Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Pensheni wa PSPF.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Ubungo Plaza, Harun Mgude, alisema mpangaji huyo alikuwa na mkataba wa miaka 15 tangu mwaka 2006, lakini tangu 2014 hajalipa kodi ya pango.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles