25.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

TAHARIRI: SERA YA ELIMU KWA WOTE MTIHANI BODI YA MIKOPO

BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza majina ya wanafunzi watakaofaidika na mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo wa 2017/2018, huku waombaji wengi wakikosa.

Kwa maoni yetu, tunaona taarifa hiyo si ya kujivunia sana, hasa ukizingatia kwamba ni nusu tu ya walioomba mikopo hiyo ndio watakaofaidika na Sh bilioni 427 zilizotengwa.

Kati ya zaidi ya wanafunzi 60,000 waliowasilisha maombi kwa mwaka mpya wa masomo unaoanzia mwezi ujao, ni wanafunzi 30,000 tu ndio watanufaika na mikopo hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul–Razaq Badru, alisema wanufaika watapata mikopo ya elimu kulingana na fani walizochagua kusoma.

Mkondo wa kwanza unawahusu wanafunzi wa fani za afya, sayansi ya elimu na hesabu, kundi ambalo litapata asilimia 40 ya mkopo huo ambao ni sawa na Sh bilioni 170.8.

Alidai kuwa mkondo wa pili umepangwa kupata asilimia 35 ya mkopo wote ambao ni sawa na Sh bilioni 149.45 na wanafunzi watakaonufaika ni wale wa fani za uhandisi, kilimo, misitu, sayansi ya ardhi, usafirishaji na fani nyingine kama hizo.

Mkondo wa tatu umepangwa kupata asilimia 25 ya mkopo wote ambao ni sawa na Sh bilioni 106.75 na wanufaika ni wanafunzi wote watakaosoma fani za lugha, sanaa, jamii na fani nyingine kama hizo.

Kwa sababu ya changamoto za ukosefu wa fedha, mpangilio huo hapo juu tunaweza kuuelewa, lakini nia iwe kutoa mikopo kwa wanafunzi wote na wa fani zote.

Tunaamini kuwa fani zote zina umuhimu katika jamii kwa njia moja au nyingine.

Tafakari kubwa sasa ni kwa wale watoto wa masikini ambao ni kati ya waombaji zaidi ya 30,000 waliokosa mikopo hiyo. Kinachotajwa hapa ni ufinyu wa fedha.

Kwa vile kuna changamoto ya ukosefu wa fedha, hatutegemei mtoto wa waziri kwa mfano, apate mkopo huo hata kama amefaulu katika masomo kwa kiasi gani. Kumpa mkopo mtoto wa ‘tajiri’ ni kumnyima mkopo huo mtoto wa mkulima mdogo kijijini.

Bado bodi inao muda wa kuendelea kuchambua tena orodha ya wanaotarajiwa kupata mikopo hiyo ili kubaini wanafunzi ambao wazazi au walezi wao wana uwezo wa kulipa ada.

Kama nia ni kuwasaidia watoto wa masikini, basi haifai watoto ambao wazazi wao wana uwezo wa kulipa ada ya chuo kuwamo kwenye orodha ya wanufaika wa mikopo.

Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, imekuwa ikiahidi kuwatetea wanyonge.

MTANZANIA Jumapili tunaungana na wadau wengine wa elimu kuishauri Bodi ya Mikopo iwe makini sana katika kuchuja majina ya waombaji ili kuhakikisha kuwa ni watoto wa masikini tu ndio wanapata mikopo hiyo.

Wanasema mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe, basi kazi ya watoto wa masikini iwe ni kufaulu katika masomo na Serikali ichukue jukumu la kuwalipia ada.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles