24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

TADB yaendelea kutatua kero za kilimo

Mwandishi Wetu -Sinyanga

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, inaendelea kutatua changamoto na kuweka mikakati ya kuendeleza kilimo mkoani Shinyanga.

Hayo yamebainishwa wakati wa ziara ambayo imewahusisha Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack.

Mapema Telack alisema mkoa huo unategemea kilimo kwa asilimia 80 kama shughuli ya kiuchumi.

Alisema changamoto wanazokabiliana nazo mkoani Shinyanga ni pamoja na uhaba wa maghala ya kutosha, hasa kwa mazao ya biashara, huku akisisitiza kwamba hali ya hewa ya mkoa huo ambao ni jangwa kwa kipindi kirefu unaathiri sana shughuli za kilimo.

Akijibu changamoto zinazowakabili, Bashe alisema suluhu kubwa ya kuendeleza uzalishaji mkoani humo ni kuanza kufanya kilimo cha umwagiliaji.

Bashe aliagiza benki ya TADB kushirikiana na uongozi wa mkoa huo kufanya tathmini ya uwekezaji wa miradi ya umwagiliaji na ianze kufanya kazi mapema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Yasinta Mboneko, alisema kuna mradi ambao kama ukifanikishwa utaweza kuwasaidia wakulima wengi zaidi.

“Mojawapo ni mradi wa Nyida ambao unategemewa na zaidi ya wakulima 300 wa mpunga.

“Mradi huu ulianzishwa mwaka 2002, unahitajika kuboreshwa zaidi ili kufikia lengo la kufanya kilimo cha umwagiliaji,” alisema Yasinta.

Alisema awamu ya kwanza ni kipindi cha kuandaa mashamba ili kuweka malengo, pia wakishapanda mazao kwa ajili ya tathmini na baada ya kuvuna pia ambapo itasaidia kupata marejesho ya mara kwa mara na kutatua changamoto mbalimbali kwa wakati.

Kuanzia msimu ujao, Serikali imejipanga kumsaidia mkulima kwa kutoingilia bei, bali itaruhusu soko lipange bei, ila itahakikisha mkulima ananufaika, pia itafanya ‘Bulk procurement’, yaani manunuzi ya jumla ya viuatilifu bora ambayo itapunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima kwa asilimia 20 hadi 30.

 Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Justine, alisema benki inao mfuko wa dhamana kwa wakulima wadogo unaoitwa SCGS.

Alisema na kwa kwa kupitia mfuko wa dhamana, benki hiyo inashirikiana na benki nyingine za biashara.

Justine alisema msimu uliopita TADB iliwekeza zaidi ya Sh bilioni 20 kwa wakulima wa korosho, na zaidi ya wakulima 31,508 walinufaika na mpango huo, hivyo itatumia mfumo huo kwa wakulima wa pamba.

“Tutawekeza katika maeneo ya miradi ya maghala na umwagiliaji ili kuongeza kasi ya maendeleo ya mkoa, na kuwapunguzia adha ya kutegemea mvua,” alisema Justine.

Akiwa mkoani hapa, wametembelea Chama cha Ushirika Kahama (Kaku), lengo likiwa ni kuendeleza sekta ya kilimo na kufufua na kuviendeleza vyama vya ushirika.

 Mwenyekiti wa chama hicho, Namala Cherehani alisema; “Mwaka 2014 ndio ilikuwa mara ya mwisho kuchakata pamba ya wakulima kutoka Kahama na Mbogwe katika kiwanda hiki. Kwa wastani kiwanda hiki kilikuwa na uwezo wa kuchakata pamba hadi kilo milioni 20 kwa mwaka.”

Lakini Bashe amehimiza TADB kuhakikisha wanashirikiana vyema kurudisha kiwanda hicho ili kuendelea kuchakata pamba.

Justine alisema kuwa wamepokea wito huo na kuahidi kuufanyia kazi.

“TADB ni benki ya maendeleo, hivyo ina mikakati ya makusudi kufufua viwanda mbalimbali nchini, ili kuongeza tija ya uzalishaji na kumfungulia masoko mkulima jambo ambalo kwa ujumla wake litamnufaisha mkulima mmoja mmoja wa chini,” alisema Justine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles