27.2 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

SUMATRA CCC YAKOMESHA UNYANYASAJI KWA WANAFUNZI

Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


SEKTA ya usafirishaji ni tegemeo katika nchi mbalimbali duniani kwakuwa imekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi.

Miaka kadhaa ulifanyika utafiti uliobaini kuwa foleni ni kikwazo cha maendeleo kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Ilielezwa kuwa foleni katika maeneo mbalimbali ya jiji hili imekuwa ikisababisha wananchi kuchelewa kufika katika maeneo yao ya kazi na shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waliona jambo hilo, ndio maana hadi leo hii inaendelea kuboresha sekta hiyo kwa kufanya ukarabati wa miundombinu ya barabara kwa viwango tofauti.

Ukarabati wa barabara umesaidia maeneo mengi kufikika kwa urahisi na kuzidi kuimarika kibiashara kwa sababu ya usafiri wa uhakika.

Tangu Serikali ilipounda Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA CCC) ni zaidi ya miaka 10 ambapo lengo kubwa likiwa ni kuhakikisha changamoto zilizopo katika sekta ya usafiri zinatokomezwa.

Baraza hilo liliundwa kwa madhumuni mbalimbali ili kuimarisha sekta hiyo lakini kikubwa ni mtoa huduma na anayehudumiwa kila mmoja ahakikishe anatimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na kupewa haki zake za msingi.

Mwanafunzi Idrisa Mussa wa Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa ambao ni miongoni mwa wanachama wa klabu za Sumatra CCC anaishukuru elimu inayoendelea kutolewa na baraza hilo kwani imesaidia kuwapa uwezo wa kujiamini katika kudai haki zao za msingi.

“Elimu inayotolewa na baraza hili kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini, inasaidia kwa kiasi kikubwa jamii kutambua haki na wajibu wao wanapokuwa katika vyombo vya usafiri,” anasema Mussa.

Mussa anasema hivi sasa hata madereva pindi wanapotaka kukatisha ruti wanajiuliza mara mbili kwa sababu abiria wengi wanafahamu haki zao za msingi.

Anasema elimu inayoendelea kutolewa na SUMATRA CCC imesaidia kukomesha ukatishaji ruti katika mabasi ya daladala hasa kwa nyakati za jioni.

Sumatra CCC imefanya jitihada ya kuelimisha umma ili kila mwananchi atakayeona vitendo vya ukiukwaji kanuni zitolewazo na baraza hilo atoe taarifa kwa mamlaka zinazohusika ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Baraza limeweza kutoe elimu ya wajibu wa abiria anapokuwa katika chombo cha usafiri alichokipanda.

Ofisa Elimu kwa Umma wa Sumatra CCC, Nicholous Kinyariri anasema abiria anatakiwa anapokuwa kwenye chombo cha moto kujiandaa kwa safari ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhari endapo kutatokea ajali.

Anasema pia anatakiwa anapokuwa katika chombo cha usafiri kufuata utaratibu uliopo ikiwamo kufunga mkanda wa kiti ili kupunguza madhara ya ajali pale pindi itakapotokea.

Pia anatakiwa kulipa kiasi cha nauli kilichothibitishwa na SUMATRA vinginevyo abiria anatakiwa kuwajibika kwa kutoa taarifa kwa wahusika ili aweze kupata msaada zaidi.

Kinyariri anasema abiria anatakiwa akiwa katika chombo hicho hataki kusumbuliwa kwa kushikwashikwa na konda, dereva au wakala wa gari hilo.

“Abiria ana wajibu wa kutoshirikiana na dereva wa basi kuficha makosa ya kuvunja masharti ya leseni kwa kuwa ni ukiukwaji wa sheria,” anasema Kinyariri.

Pia elimu hiyo inayotolewa inamsaidia abiria kuwa mwerevu na hawezi kupata usumbufu au kuibiwa wakati anapokuwa katika chombo cha usafiri kwa sababu haki na wajibu wa abiria tayari anakuwa ameshafahamu.

Kinyariri anasema baraza halikuishia kutoa elimu kwa abiria, pia wameanzisha vilabu kwa wanafunzi nchi nzima na hivi sasa tayari wana vilabu 46 kutoka shule za msingi na sekondari nchi nzima.

Anasema vilabu hivyo vinasaidia kwa kiasi kikubwa kueneza ujumbe wa usalama barabarani na abiria kujua haki na wajibu pale anapokuwa amepanda chombo cha usafiri.

Kwa upande wake, Kamishna wa Bima nchini, Dk. Baghayo Saqware anasema ili kuondoa kero wanazozipata abiria wakati wa kufanya safari, tayari wamebadili sheria mbalimbali za bima.

Anasema ni kwa muda mrefu abiria wamekuwa wakipata shida pindi wanapopata ajali kwa kushindwa kulipwa fidia.

Saqware anasema zipo sababu nyingi zinazochangia abiria kukosa fidia ikiwamo utapeli wa baadhi ya wenye kampuni za bima.

Anasema ongezeko la malalamiko na kero wanazozipata abiria katika kudai fidia, Mamlaka ya Usimamizi Shughuli za Bima nchini (TIRA), ipo kwenye mchakato kuhakikisha wamiliki wa mabasi ya umma tiketi zao zinabandikwa pia nembo ya bima ambayo mmiliki amekata.

Anasema hali hiyo itaondoa usumbufu kwa abiria pindi wanapopata ajali iwe rahisi kufahamu watalipwa na kampuni ipi.

“Mpango huu tumeshirikiana na Mamlaka ya Usimamizi Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ili kuondoa adha ya ubabaishaji kulipa fidia na tutahakikisha tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara,” anasema Saqware.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles