25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

SUGU, PROFEJA JAY WAMESHINDWA AU WAMEWEZA?

Na RAMADHANI MASENGA 

WANAMUZIKI wa Hip Hop pengine ndiyo wanaoongoza kwa tambo. Sikiliza mahojiano yao. Mbali na kujisifu kuwa wanajua sana kuandika mambo ya maana kuliko wasanii wa aina nyingine za muziki, ila watakuambia wao wanawakilisha mitaa.

Wanajiona ni zaidi ya wabunge na madiwani. Wanajiona wana sauti pana za kuwafikia watu na zenye mamlaka pengine kuliko hata waandishi  wa habari.

Kumbuka zile nyimbo kama Don’t Believe the Hype ya Naught by Nature na nyinginezo. Ukisikiliza mashairi ya wanamuziki wa Hip Hop unaweza kuamini ni watu wenye kufikiri zaidi na wenye uwezo wa kujenga na kutetea hoja namna inavyotakiwa.

Kwa namna hiyo, jamii nyingi zimekuwa zikiamini muziki wa Hip Hop ni muziki wa kutetea haki na kupigania watu.

Mwanamuziki wa Hip Hop ni mtu analiyejipambanua kama mtumiaji mzuri wa akili, asiyeyumbishwa na mwenye kujiamini. Hilo lilionekana kwa uwazi zaidi pale mwanamuziki mkorofi wa Hip Hop wa Marekani, Eminem alipomuongelea maneno ya kukera aliyekuwa rais wa taifa hilo, George Walker Bush.

Eminem alimkaripia hadharani Bush kwa kitendo chake cha kuanzisha vita Iraq baada ya kuisha ile ya Afghanistani.

Mwaka 2010 wakati Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alipoteuliwa na chama chake cha Chadema kugombea ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini, mbali na mengi aliyosema aliahidi kuwa anakwenda kupigania haki na kusimamia kile anachoamini kama ambavyo amekuwa akifanya miaka yote kupitia muziki wake.

Swali la kujiuliza, je, Sugu amefanikiwa kuwakilisha hisia na misimamo yake ipasavyo bungeni? Ni kweli Sugu hayumbishwi na maono ya chama chake hata kama siyo sahihi na badala yake anasimamia kile kikuu anachoamini?

Kuna mambo mengi yanafanywa na Sugu, ila wingi wa mambo hayo ni yale matarajio ya wengi kuwa watamuona mtu mwenye maono mapya na mwenye misimamo isiyoingiliwa ovyo.

Sugu ameweza kuwa mwana Hip Hop mwenye upeo mkubwa wenye kuwazidi hata wanasiasa ambao mara nyingi hapo kabla tuliona kama waongo na wapiga danadana za kauli?

Ukweli ni kwamba Sugu siyo mbunge mashuhuri sana bungeni. Yeye na mwenzake Profesa Jay wamebaki kuwa wafuasi wa wanasiasa wakongwe bungeni.

Hali hii ni dhihirisho kuwa ujanja na harakati ambazo huwa wanahubiri zimebaki katika nyimbo na siyo katika maisha halisi?

Wengi waliamini kuwa baada ya Profesa Jay kuingia bungeni siyo tu angeleta chachu na chimbuko la fikra halisi za mitaani bali pia wanasiasa wakongwe kama akina Freeman Mbowe (Mbunge wa Hai – Chadema) watajivunia kufanya nao kazi. Lakini hali  imekuwa tofauti.

Badala ya kuwaona Mbowe na Zitto wakijivunia kuwa karibu na akina Sugu, wao ndiyo wamekuwa wakionekana kuona fahari kuwa karibu na akina Mbowe!

Kwa hiyo Sugu na Profesa Jay, siyo tu wameangukia kuwa watumwa wa wanasiasa waliowakuta ila pia hawana ubavu wa kupindua chochote, hata kiwe tofauti na imani yao, kwa wanasiasa hawa.

Wakati wa kampeni za siasa, wengi waliamini Sugu na kisha baadaye Profesa Jay kuingia kwao bungeni kutafanya fikra za wahafidhina waliokuwa wanaamini Hip Hop ni uhuni kubadilika na kuona wana Hip Hop ni vichwa vyenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya kifikra na kiutendaji.

Sugu na Profesa Jay wamefanikiwa katika hili? Wanaonekana ni wakombozi na waletaji wa fikra mpya, au ni kama wasaka tonge wengine walioingia bungeni kuboresha maisha yao?

Sugu na mwenzake wanaonekana kuwa huru katika fikra zao na maamuzi au wamegeuka kuwa kasuku wa kumezeshwa lolote na wakuu wa vyama vyao ili kuwapigania kadiri inavyowezekana?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles