25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Sugu azungumzia madiwani chadema waliohamia CCM

Eliudi Ngondo – Mbeya

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mbeya, kimesema madiwani wake 11 waliohamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni, walianza harakati zao mwaka 2018 na kutaka wengine wenye nia kama hiyo waondoke mapema. 

 Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema madiwani hao wakiongozwa na Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi na Naibu Meya, Fanuel Kyanula, kuhamia CCM hakujaidhoofisha Chadema bali kumeiimarisha zaidi.

Alisema baada ya kupata taarifa ya madiwani hao kuhama, walipatwa na wasiwasi kuwa chama hicho kitakuwa kimepoteza mwelekeo, lakini ulipofanyika utafiti mdogo kwenye baadhi ya maeneo, walibaini bado chama hicho kinakubalika kwa wananchi.

 Sugu alisema hofu yake ilikuwa huenda madiwani hao walihama na wanachama, lakini baada ya kufanya utafiti wamebaini walioondoka ni viongozi na familia zao na si wanachama ambao ndio wapigakura.

 “Juzi alinipigia simu Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally akitaka kujua hali yangu na nilichomjibu nilimwambia ‘wewe ni rafiki na mtani wangu, lakini kwa sasa umekuwa ndugu kwa sababu umeniimarisha kisisa kuliko wakati wowote’ kwa sababu ametuondolea mizigo,” alisema Sugu.

 Alisema Meya wa Mbeya ambaye amejiuzulu, alikuwa hashiriki shughuli za chama hicho kwa muda mrefu kwani hata mkutano mkuu wa Chadema uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana Dar es Salaam hakuhudhuria.

Sugu alisema chama hicho kina mtaji wa wapigakura 250,000 ndani ya Jiji la Mbeya ambao 200,000 ni wanachama wa chama hicho na zaidi ya 50,000 ni wanachama wa vyama vingine kikiwemo CCM.

Alisema kupitia kampeni ya Chadema ni Msingi, chama hicho kimeandikisha wanachama zaidi ya 60,000 na hadi kufikia Juni kitakuwa kimeandikisha 100,000 na kufikia tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba wanachama watakaokuwa wameandikishwa watakuwa 200,000.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, Joseph China, alisema madiwani hao walianza muda mrefu kufanya majaribio ya kuhama.

 Alisema mwaka 2018 wakati wa ziara ya Katibu Mwenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole, baadhi ya madiwani walikuwa wanatakiwa kuhudhuria mkutano wake ili wapokewe, lakini alilazimika kujifungia nao kwenye ofisi za kanda siku nzima ili kuzuia jaribio hilo.

 “Mwaka jana Meya alikuwa anatakiwa aongozane na madiwani wote wa chama kwenda bungeni jijini Dodoma kwa mwaliko wa Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, lakini tulizuia na madiwani wetu watatu walienda na baada ya siku chache wakahamia CCM,” alisema China.

Alisema baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, chama hicho kilikuwa na madiwani 260 katika kanda nzima ya Nyasa ambao kati yao 39 wameshahamia CCM, wanne walifariki na Jiji la Mbeya walihamia CCM ni 14.

 Aliwataka na wengine wanaotaka kukihama chama hicho wahame mapema ili chama hicho kiwajue wasaliti mapema kabla muda wa uchaguzi haujafika.

 Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema Mbeya Mjini, John Mwambigija, alisema kwenye Uchaguzi Mkuu ujao moja ya ahadi ambazo madiwani watakuwa wanazitoa ni pamoja na kueleza kwa atakachofanywa endapo atakisaliti chama.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles