29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

Stan Rhymes: Mwana Hip hop anayemzimia Young Lunya

*Atoa ushauri kuikuza Hip hop

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

“Mziki unanilipa japo bado kipato hakilingani na juhudi na uwezo nilionao lakini naamini manufaa makubwa sana yapo kwa ajili yangu kutokana na mikakati niliyojiwekea,’ ni maneno ya msanii wa miondoko ya Hip Hop, Stanley Wissa maarufu kama Stan Rhymes.

Licha ya udogo wa jina lake tayari mkali huyo wa kuchana ameshapewa nafasi na baadhi ya wasanii wakubwa wa muziki wa Hiphop nchini, akiwamo Izzo Bizness aliyemshirikisha kwenye remix ya Mr. Christmas ya mwaka 2022, na Nikki Mbishi waliyeshiriki naye kwenye project ya Wanene Studio ‘DaVinci Codes Freestyle Challenge’ akiwa na wakali wengine.

HISTORIA YAKE

Stan Rhymes mwenye uwezo wa kuandika mistari mikali, kuchana na mitindo huru, ni mtoto wa kwanza katika familia yenye watoto wawili akiwa na dada yake aitwaye, Witness Wissa waliozaliwa, kukulia na kusoma mkoani Njombe.

“Nimesoma shule ya msingi Mpechi iliyoko Njombe nikahamia Iringa ambako nilisoma shule ya sekondari Tagamenda, sikuendelea na masomo baada ya kumaliza kidato cha nne na baada ya kuwa mtaani kwa muda mrefu ndipo nilianza rasmi shughuli za muziki,” anasema Stan

ASILI YA JINA LAKE

Anasema jina la Stan Rhymes alipewa na watu wake wa karibu kutokana na tabia yake ya kupenda kurap, ambapo asili ya kupenda kujiita Njombe Finest ni kwa sababu anajivunia mahali alikotoka mkoani Njombe na ni rahisi kumtambua huku akiwa na malengo ya kuibeba nabegani Njombe na kuiheshimisha popote duniani.

“Mara nyingi nilikuwa nikipiga stori na watu maneno nayapanga kwa vina (Rhymes) basi wakawa wananiita Stan Vina ndipo baadaye nikatoa vina na kuweka neno Rhymes, pia najiita Njombe Town Finest kwa sababu niko proud na mitaa ninayotoka na ni desturi yetu ma emcee kuwakilisha maisha halisi ya jamii tulizokulia,” anasema Emcee huyo

 KAZI ZAKE

Mkali huyu wa vina na kuchora mashairi siyo mtu wa maneno tu bali kazi kwani tayari ana Mixtape tatu ambazo ni Heshima iliyotoka mwaka 2016, ya pili ni Miaka 800 ya mwaka 2018, na ya tatu ni History iliyotoka mwaka jana (2022).

“Sauti yangu na ma emcee wengine ni sound yangu na pia mimi nagusa angle nyingi katika nguzo ya emcee yaani naweza ku freestyle kutokana na mazingira yaliyonizunguka na pia nafanya freestyle battle. Pia ukija kwenye uandishi nazingatia content na mitindo, hutojua kama ndo yule Stan wa freestyles,” anaeleza

Mkali huyo wa mistari na vina, anafunguka kuhusu faida ambazo amezipata kwenye muziki mpaka sasa baada ya kuachia mixtape zake tatu.

“Mziki unanilipa japo bado kipato hakilingani na juhudi na uwezo nilionao lakini naamini manufaa makubwa sana yapo kwa ajili yangu kutokana na mikakati niliyojiwekea,” anasema na kuongeza

“Mara nyingi naingiza kipato kwa kuuza mixtapes zangu mwenyewe pia huwa napata baadhi ya shows lakini kubwa zaidi ni hata mishe ninayoifanya nje ya muziki ambayo kidogo inanofanya naishi mjini ni muziki ndio ulinikutanisha nayo,”

P FUNK, FID Q na PROF JAY WAMVUTIA

Kila mtu ana siri ya watu waliomvutia kufanya jambo fulani na watu ambao anawaangalia na kujifunza kutoka kwao kwenye faini aliyoichagua, ndivyo ilivyo pia kwa Stan Rhymes ambaye wakati anaanza harakati zake za kuingia kwenye muziki wa Rap alikuwa anawatazama na kujifunza kwa Fid Q, Prof Jay, Hashim Dogo, Nikki Mbishi, One The Incredible, Salu T na wengine.

Ukiachana na wasanii wenzake, Mkali huyo alikuwa anavutiwa na midundo na beat zilizokuwa zikisukwa na watayarishaji, P Funk Majani wa Bongo Records, Miika Mwamba na Duke Tachez

“Nilianza kupenda hip hop tangu sijui chochote kuhusu mapato wala changamoto zilizopo hivyo nimekuja kuvijua baadae na sikuona sababu ya kukimbia changamoto hizo kwa sababu nimezungukwa na watu wanaofanya mziki wa kuimba pia nikagundua hata wao wanazo changamoto zao pia kwahiyo ni kupambana nazo kisha muda utasoma,” anasema

MICHONGO YAKE

Miradi yangu huwa naiuza mwenyewe kwa sababu ndio njia inayonipa faida maradufu. Mfano nikitoa mixtape na nikauza elfu kumi kwa nakala mia moja nitapata milioni moja lakini kwenye streaming platforms watu kumi wakisikiliza mixtape yangu hata elfu hamsini hakuna pia kuna wadau wangu ambao wanathamini ninachokifanya na wanaweza kuja na offer wakalipa hata laki kwa nakala moja,” anasema na kuongeza:

“Uchanaji wangu unanilipa kila uchwao naona mafanikio zaidi mbeleni. Nje ya muziki nafanya biashara nyingine kitaa na deal na mavazi na vyakula kutanua wigo wa kipato,”

Kuhusu fursa za soko la kisasa la kidigitali, anasema “Fursa ipo kubwa kwenye digital hata kama isipokuwa ya kimaslahi ya pesa lakini ile ni njia ya kitaalam na kisasa zaidi ya kusambaza muziki ambapo simshauri msanii yeyote kuiepuka.

“Kuna kitu inaitwa google artist knowledge pannel hii ni kama profile ya msanii inakuwepo google ambapo inajumuisha viunga vyako karibu vyote na kumrahisishia mtu anyekutakuta google kupata kazi zako kwa urahisi sasa vigezo vya kuipata ni lazima uwepo kwenye hizo platform kwa hiyo ni muhimu sana,” anasema.

AWAPA NENO CHIPUKIZI

“Inawezekana kwa ma emcee wa undergound kuingia mainstream bila kuchakachua uhalisia kikubwa ni kusimamia na kuheshimu unachokifanya. Uhalisia una nguvu sana popote pale. Kila mtu ni shabiki wa uhalisia kwa sababu hata wanaofeki pia wana maisha yao halisi nje ya u feki wao.

“Na pia tukiwa kama wana Hip Hop tunapoanzisha vilinge tutoe elimu zaidi pia kuhusu soko. Ushauri wangu kwa ma emcee chipukizi au yeyote anayejihusisha na sanaa ni wajitahidi kuwa wabunifu zaidi na wakipe thamani chochote wanachofanya,” anasema mkali huyo wa Rhymes.

MALENGO YAKE

“Mimi malengo yangu ni kutengeneza kipato kupitia Sanaa ili niweze kusapoti vipaji vipya hasa vile vinavyotoka familia maskini na pia kuiwezesha rap ya bongo kutoboa kimataifa kwa lugha yetu ya kiswahili kwa sababu inawezekana mtu asiyeelewa kiswahili kupenda rap endapo mwandishi akawa na mbinu nyingi za kiuandishi,” anasema.

AMKUBALI YOUNG LUNYA, ATOA USHAURI

Stan Rhymes amekuwa na mtazamo tofauti na mashabiki na baadhi ya wadau wa muziki wa HipHop nchini ambao wamekuwa wakimkosoa Young Lunya kuwa siyo rapa mkali na hastahili sifa anazopewa, ambapo anasema Lunya ameleta mapinduzi makubwa kwenye muziki huo hasa sokoni na malipo huku akitoa wito kwa watu kuheshimu juhudi zake.

Young Lunya.

Pia ameshauri muziki huo kupewa muda wa kutosha kwenye vyombo vya habari na promo kubwa kama unavyopewa muziki mwingine ili kuwatangaza zaidi wasanii wa Tanzania, ambapo amesema ni vyema wasanii wa Hiphop kuongeza ubunifu kila siku ili kulikamata soko la muziki na kupata show za kutosha na kuingiza kipato cha uhakika.

“Mtu kama Young Lunya licha ya kwamba anafanya vizuri na anazungumziwa sana kwa sasa lakini mashabiki wengi wadau na wasanii wa hip hop wamekua wakimkosoa kwamba hastahili kuwa pale alipo kitu ambacho sio sawa, tunatakiwa kuangalia pia mapinduzi aliyoyafanya jamaa sokoni hawa ni watu ambao wanaiwakilisha tamaduni yetu sokoni tunapaswa kuwaheshimu japo kuwapenda ni hiari yetu.

“Ubunifu ni wakutosha japo tunapaswa kuendelea kubuni kila siku lakini kikubwa ni uwekezaji zaidi kwenye products zetu, misingi ya hip hop haituzuii kufanya video nzuri zenye ubora wala haitufungi kutoimba nyimbo za kuburudisha watu tusijiweke ndani ya box kwamba sisi ni watu wa kuonya tu au kukosoa hapana Nash MC ni mwana hip hop lakini ana kibao chake kinasema hakuna anyetudai kwa nini tusifurahi ni cha Ku party fresh tu,” anasema mkali huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles