Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Naibu Spika wa Bunge, Azzan Zungu, amewahakikishia mama lishe na baba lishe wa Soko la Samaki la Kimataifa Feri kuwa watafungiwa mtambo wa nishati safi ya kupikia ili kuwaepusha kutumia fedha nyingi kununua gesi kupitia mitungi midogo.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa mkakati wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kulinda mazingira, kuwaweka wanawake katika nafasi nzuri ya kujiendeleza kiuchumi.
Hayo ameyasema leo Machi 23, 2024 sokoni hapo, jijini Dar es Salaam wakati wa kugawa mitungi 200 kati ya 700 iliyotolewa kwa mama na baba lishe hao ambayo imetolewa kwa ushirikiano wa Zungu na kampuni ya Gesi ya Oryx Tanzania.
Naibu Spika huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilala, ametoa ahadi hiyo baada ya kupokea maombi ya wafanyabiashara hao kupitia kwa kiongozi Zone Namba 7 katika soko hili, Said Mpinji aliyelalamika kuwa wanalazimika kutumia Sh110,000 kila siku kujaza gesi ya kuendeshea shughuli za baba na mama lishe.
Amesema kilio hicho ni cha muda mrefu na kwamba tayari amezungumza na kampuni ya ya Oryx Tanzania kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wake, Benoit Araman ambaye amekubali kufunga mifumo ya gesi ya kisasa kisha kusambaza huduma hiyo kwa wafanyabiashara hao kwa gharama nafuu.
“Mkombozi wetu ni Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye alianzisha kampeni ya Nishati Safi ya kupikia, kuhakikisha Watanzania wanaishi maisha mazuri.
“Oryx wamekubali kuweka mtungi mmoja mkubwa na mifumo ya usambazaji, kisha watasambaza huduma kwa mama na baba lishe waliopo hapa na kuwafungia mita halafu watakuwa wakilipia huduma kama wanavyofanya katika umeme,” amesema.
Naya Benoit amesema wamewafikia wajasiriamali hao kwa lengo la kutekeleza mkakati wa Rais Dk. Samia wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kulinda mazingira na afya za wananchi.
Amesema kuwa tangu Julai mwaka 2021, walianza mkakati huo baada ya Rais kutangaza kwamba serikali yake inataka kuona hadi mwaka 2030 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Abbasi Mtemvu aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amesema kilichofanyika ni utekelezaji wa Ilani na kumpongeza Zungu kwa namna anavyowatetea wananchi katika jimbo lake.
“Zungu ni mfano wa kuigwa, amefanya makubwa, nimekuwa naye bungeni kwa miaka 10 muda wote ameonyesha dhamira ya kutetea wananchi wa jimbo lake, anastahili pongezi,” amesema Mtemvu.
Ameipongeza serikali kwa kuendelea kupeleka maendeleo kwa wananchi huku akiwataka mama na baba lishe wa sokoni hapo kujiandaa kupokea mitaji kutoka serikali ili kununua biashara zao.
Mtemvu ameeleza kuwa serikali imetenga Sh 8.0 bilioni kwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri na japokuwa ilisimama lakini muda si mrefu itaanza kutolewa tena.
“Serikali ya CCM ipo tayari kukupeni mitaji kwa kuwa imejiopanga vizuri, sasa jiandaeni kuchangamkia fursa. Aprili mwaka huu utaanza ujenzi mkubwa wa barabara zaidi ya kilometa 200 ambapo zaidi ya Sh 188 bilioni zitatumika, hii ni fursa kwa mama na baba lishe kupeleka chakula chenu kitamu na kujiingizia kipato,” amesema.