23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 10, 2022

SMZ yapata gawio Sh bilioni 25

Mwandishi wetu -Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imepata faida zaidi ya Sh  bilioni 25, ikiwa ni malipo ya  huduma za matumizi ya mkonga wa taifa na Serikali Mtandao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mkonga wa Mawasiliano Zanzibar, Shukuru Awadhi Suleiman, alisema fedha hizo zimelipwa kutoka katika kampuni ambazo zinatumia huduma zao.

“Tumepata fedha hizo kutoka Kampuni ya simu ya Zantel, ikiwa ni malipo kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2024,” alisema Suleiman.

Alisema Serikali Mtandao imekuwa na faida kwa wananchi ambapo sasa huduma za afya, kodi na elimu zimekuwa zikitolewa kwa urahisi na ufanisi mkubwa.

Suleiman alisema katika sekta ya afya, kumekuwa na mafanikio katika huduma, vituo vya afya 24 Unguja na Pemba vimeunganishwa katika mfumo wa Serikali Mtandao.

“Leo hii mgonjwa anaweza kufanyiwa vipimo kama vya X-ray katika Hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja na vipimo vile vitasomwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja bila ya mgonjwa au daktari kulazimika kusafiri,” alisema Suleiman.

Alisema kwa kutumia huduma za Serikali Mtandao, huduma za vyeti vya kuzaliwa imekuwa rahisi kwa sasa kwani wananchi wanavipata katika wilaya zao.

Mbali ya sekta hizo, pia Kampuni ya Uunganishaji Maudhui ya ZMUX inatumia mkonga wa taifa katika kurusha matangazo ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).

Akizungumzia sekta ya kodi, Suleiman alisema Bodi ya Mapato Zanzibar ni moja ya watumiaji wakubwa wa huduma za Serikali Mtandao na sasa huduma za kodi zimeunganishwa katika mtandao mmoja.

Alisema tayari wamepokea maombi ya Kampuni ya mawasiliano  ya TTCL na Comnet kutaka kutumia huduma za mkonga wa taifa.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano, Dk. Mzee Suleiman, alisema kumekuwa na mafanikio katika matumizi ya Tehama, hasa baada ya kukamilika kwa mkonga wa taifa.

Dk. Mzee alisema mwaka 2011, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein alitoa agizo la kuhakikisha Zanzibar inaongeza kasi ya matumizi ya Tehama katika shughuli mbalimbali.

Alisema kuna vituo 10 vya kuwafundisha wananchi matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, na mafunzo hayo yanatolewa bure kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,395FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles