20.8 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Siri mpya maduka ya fedha kufungwa

  • Waziri wa fedha ajibu maswali tata yaliyogubika sakata hilo

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

TAKRIBANI miezi sita tangu Novemba mwaka jana operesheni ya kufunga na kuchukua fedha za kigeni katika maduka ya kubadili fedha za kigeni ilipoanza, Serikali imejibu maswali yaliyoibuliwa kutokana na operesheni hiyo, ikiwamo wasisiwasi kwamba kukosekana fedha hizo nchini kuliichochea.

Maswali hayo yalijibiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Profesa Florence Luoga, walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma.

Baadhi nya maswali yaliyoibuka ni pamoja na je, Serikali haina fedha za kigeni za kutosha ndiyo maana inachukua za watu binafsi? Je, inataifisha fedha na mali za watu? Kwanini wahusika hawapelekwi mahakamani kama wamekiuka sheria? Kama ni utakatishaji ni maduka mangapi yalikutwa yakitakatisha fedha? Nini mafanikio ya operesheni hiyo?

Dk. Mpango alisema kwa kipindi kifupi cha utekelezaji wa operesheni hiyo, thamani ya shilingi imeimarika na upatikanaji wa fedha za kigeni katika benki za biashara umeimarika.

Alisema kabla ya udhibiti wa biashara ya kubadilisha fedha za kigeni, dola ya Marekani ilikuwa inauzwa kwa wastani wa Sh 2,450 na baada ya utekelezaji wa operesheni hiyo sasa dola ya Marekani inauzwa kwa wastani wa Sh 2,300.

Aidha, benki za biashara kwa wastani hivi sasa zinakusanya jumla ya Dola za Marekani milioni 15 kwa siku.

“Ni matarajio ya Serikali kuwa udhibiti huu utaziwezesha benki za biashara na taasisi nyingine kuuza fedha za kigeni kwa wingi kwenye soko la fedha za kigeni na hatimaye kuongeza akiba ya fedha za kigeni,” alisema Dk. Mpango.

MADUKA KUFUNGIWA

Dk. Mpango alisema katika kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha kuwa sekta ya fedha inachangia ipasavyo utulivu na ukuaji wa uchumi nchini, BoT ilibaini uwepo wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambayo yalikuwa yakiendeshwa pasipo kuzingatia sheria.

Alizitaja sheria hizo kuwa ni ya Foreign Exchange Act 1992, Kanuni za The Foreign Exchange (Bureau de Change) Regulations 2015 na marekebisho ya mwaka 2017 na taratibu za utoaji wa huduma za ubadilishaji wa fedha za kigeni.

“Kufuatia hali hiyo, zoezi maalumu la ukaguzi wa kina kwa maduka hayo lilifanyika Arusha Novemba 2018 na kwa Dar es Salaam siku ya tarehe 27 Februari 2019, 1 na 8 Machi 2019 kwa kuhusisha vyombo vya dola na kubaini ukwepaji mkubwa wa kodi na uvunjaji wa sheria.

 “Zoezi hili limebaini pia uondoshwaji wa fedha katika mfumo rasmi wa fedha na kuelekezwa kwenye mifumo ya utakatishaji wa fedha haramu, kupokea amana kutoka kwa wafanyabiashara kinyume cha matakwa ya leseni za biashara husika, kudhoofisha thamani ya shilingi na mambo mengine ambayo yalianza kuathiri usalama wa nchi.

“Baadhi ya maduka yaligundulika kutumia fedha nyingi za Tanzania kununua fedha za kigeni, lakini fedha kidogo za kigeni ziliuzwa na hakuna taarifa ya matumizi ya fedha za kigeni zilizobaki.

“Ni vizuri ieleweke kuwa zoezi la ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni lilitekelezwa kwa kuzingatia sheria za nchi tofauti na malalamiko na tuhuma mbalimbali zilizotolewa za kudai uwepo wa ukiukwaji wa sheria na haki kwa wamiliki wa maduka hayo.

“Jambo la kushangaza ni kwamba hakuna mmiliki yeyote wa duka aliyewasilisha malalamiko kuhusiana na zoezi hili kwenye mamlaka husika. Hata hivyo, Benki Kuu ya Tanzania na mamlaka nyingine za Serikali zinafuatilia kwa umakini ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo zinazotolewa,” alisema Dk. Mpango.

HAKUNA FEDHA ZILIZOTAIFISHWA

Katika hatua nyingine, Dk. Mpango alisema Serikali ya awamu ya tano inatekeleza majukumu yake kwa umakini.

Alisema Serikali inauthibitishia umma wa Watanzania kuwa katika ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni hakuna fedha au mali yoyote iliyotaifishwa.

Dk. Mpango alisema taratibu za kisheria zilifuatwa wakati wa kuchukua vielelezo mbalimbali zikiwemo fedha, kompyuta, simu za viganjani, mashine maalumu za kuhifadhi taarifa na taarifa mbalimbali ili kusaidia uchunguzi.

“Lengo la zoezi hili sio kufuta biashara ya maduka ya kubadilishia fedha za kigeni kwa watu binafsi, bali ni kudhibiti ukiukwaji wa sheria uliokithiri, ukwepaji wa kodi na utakatishaji wa fedha haramu.

“Maduka machache ya kubadilisha fedha za kigeni ambayo yalizingatia sheria na kanuni za Foreign Exchange na masharti ya biashara hiyo yaliachwa kuendelea na utoaji wa huduma hiyo,” alisema.

SERIKALI YATOA TAHADHARI

Dk. Mpango alisema Serikali inatoa tahadhari kwa wananchi kutoshiriki biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa njia zisizo halali.

“Hivi sasa kuna taarifa kwa baadhi ya maeneo ya mipakani na majiji ya Dar es Salaam na Arusha wamejitokeza watu wanaofanya biashara haramu ya kubadilisha fedha za kigeni ambao wamewaathiri baadhi ya wananchi kwa wizi.

“Vyombo vya usalama ikiwemo Jeshi la Polisi vimeongeza nguvu katika kuhakikisha biashara hii haramu (Black Market) inatokomezwa na hivi sasa wahalifu saba wamekamatwa na kufikishwa mahakamani,” alisema Dk. Mpango.

AKIBA FEDHA ZA KIGENI

Aidha Dk. Mpango alisema Serikali inayo akiba ya kutosha ya fedha za kigeni.

“Serikali inapenda kuwahakikishia Watanzania wote kuwa inayo akiba ya fedha za kigeni ya kutosha zipatazo Dola za Marekani bilioni 4.67 hadi tarehe 30 Machi 2019 zenye uwezo wa kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi 4.8.

“Hivyo wasiwasi kuwa Serikali imechukua hatua ya kufunga baadhi ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni kwa sababu haina akiba ya fedha za kigeni si ya kweli hata kidogo.

“Hofu kwamba nchi inarejea katika kipindi cha nyuma ambapo fedha za kigeni zilikuwa zinatolewa kwa vibali ili kukidhi mahitaji ya fedha hizo kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, nazo hazina msingi,” alisema.

KANUNI MPYA

Katika hatua nyingine, Dk. Mpango alisema Serikali imeandaa kanuni mpya kwa biashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambazo zitaelekeza jinsi ya kuomba leseni za uendeshaji wa maduka hayo kwa mtu binafsi au taasisi yeyote na masharti ya kuzingatiwa wakati wa shughuli hizo.

 Dk. Mpango alisema Serikali imeandaa kanuni mpya kwa biashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambazo zitaelekeza jinsi ya kuomba leseni za uendeshaji wa maduka hayo kwa mtu binafsi au taasisi yoyote na masharti ya kuzingatiwa wakati wa shughuli hizo.

Alisema kanuni hizo zinalenga kuweka mazingira mazuri ya biashara ambayo hayatatoa athari kwa sekta ya fedha na uchumi kwa jumla na inakuwa yenye manufaa kwa nchi.

CHAKULA CHA KUTOSHA KIPO

Aidha Dk. Mpango alisema nchi ina akiba ya kutosha ya chakula cha kutosheleza kwa asilimia 124.

 “Serikali inachukua fursa hii kuwaeleza wananchi kuwa nchi yetu ina akiba ya chakula cha kutosha ambacho kina utoshelevu wa asilimia 124 kwa mwaka huu wa fedha 2018/19. 

Hivyo Serikali haitarajii kutumia fedha za kigeni kuagiza chakula kutoka nje ya nchi isipokuwa tu kama ikitokea hali ya ukame ikawa mbaya katika siku zijazo.

GAVANA NA UTAKATISHAJI WA FEDHA

Akijibu swali la waandishi wa habari waliotaka kujua ni maduka mangapi yamekutwa na utakatishaji wa fedha, Gavana wa BoT, Profesa Luoga alisema uchunguzi bado unaendelea.

“Bado uchunguzi unaendelea, tulipofanya zoezi tulichukua vielelezo mbalimbali na vinachambuliwa na wataalamu kutoka vyombo mbalimbali vya dola na pale ambapo uchunguzi ukikamilika wale ambao kutakuwa na ushahidi watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.

MADUKA 82 DAR YAKUTWA UTAKATISHAJI FEDHA

Profesa Luoga alisema katika maduka 87 ya kubadilishia fedha Jijini Dar es Salaam, ni matano pekee ndiyo hayakukutwa na ukiukwaji wa sheria huku 82 yakikutwa na makosa mbalimbali.

“Hatuwezi tukasema ni maduka mangapi, lakini kwa kuangalia ni maduka mengi yalihusika katika utakatishaji wa fedha kwa sababu Dar es Salaam ilihusisha maduka 87, katika hayo maduka matano tu hayakukutwa na ukiukwaji wa sheria, lakini tusubiri taarifa kutoka kwa wataalamu,” alisema Profesa Luoga.

Alisema Mwanza kuna maduka mawili tu ambayo tayari yaliishapewa ‘notice’, Dodoma ni machache na mikoa iliyobaki yote imepewa ‘notice’.

Profesa Luoga alisema kwa Zanzibar aliishawasiliana na Waziri wa Fedha wa huko na watachukua hatua, lakini tayari maduka manne yalikuwa yameishajifunga yenyewe.

“Lakini Zanzibar tayari kuna maduka yamefunguliwa na Benki ya Posta na CRDB,” alisema.

MASHARTI MAGUMU YA USAFIRISHAJI DOLA

Kuhusu masharti magumu katika usafirishaji wa dola nje ya nchi, Profesa Luoga alisema si kweli kwamba kuna ugumu katika kusafirisha dola.

“Masharti yetu yameendelea kubaki katika sheria tangu mwaka 1992 na hayo masharti sio kwa nchi ya Tanzania peke yake, ni pamoja na nchi nyingine. Kwa mfano unaposafirisha dola kutoka Tanzania inategemea unazipeleka wapi.

“Ukizipeleka Marekani huruhusiwi kuingiza Marekani zaidi ya dola 10,000 ukipeleka Uingereza nako kuna kiwango hicho hicho, kwahiyo unavyotoka Tanzania pesa ambayo unaweza ukatoka nayo inalingana na pesa ambayo utaruhusiwa kuipeleka sehemu yoyote ile.

“Sio kwamba mashati ya Tanzania ni magumu, ni kwa nchi zote. Kwa mfano ukikutwa na dola 400,000 swali ni kwamba unaenda kuziingiza vipi katika nchi ambayo unaenda, ambayo haitakuruhusu kuingiza zaidi ya dola 10,000,” alisema.

NI DUKA MOJA LENYE UWEZO WA KUHAMISHA FEDHA

Profesa Luoga alisema kwa muda uliopita maduka ya kubadilishia fedha ambayo yalikuwa hayawezi kufanya shughuli za uhamishaji fedha ilikuwa lazima yawe na mtaji wa sh milioni mia tatu.

Alisema yale ambayo yalikuwa yanaruhusiwa kuweza kuhamisha fedha yalipaswa kuwa na mtaji wa sh bilioni moja.

“Na ni duka moja tu nchi nzima ndilo lililokuwa na leseni hiyo ya kuhamisha fedha,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles