24.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 8, 2022

SIMBA YAUFYATA KWA KAGERA SUGAR

NA MWANDISHI WETU-BUKOBA

KWA mara nyingine tena Kagera Sugar, imepeleka maumivu kwa mashabiki wa Simba, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

Huo ni mchezo wa pili kwa Simba kupoteza msimu huu wakianza dhidi ya Mbao FC walipofungwa bao 1-0 Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Kagera Sugar wamekuwa kama wababe wa Simba kwani msimu uliopita ndiyo timu pekee iliyofanikiwa kuwafunga Wekundu hao wa Msimbazi, tena mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.

Katika mchezo huo wa msimu uliopita, Kagera Sugar walishinda bao 1-0 ukiwa ni mchezo wa mwisho Uwanja wa Taifa na kuwafanya Simba kukabidhiwa kombe na Rais Magufuli wakiwa vichwa chini.

Msimu wa 2016/17, Kagera hao hao ndio waliosababisha Simba kushindwa kupata ubingwa wakiwafunga mabao 2-1 na Wekundu hao wa Msimbazi kuleta madai kwamba Wakata Miwa hao walimchezesha kimakosa, Mohamed Fakhi, lakini suala hilo likamalizika kimya kimya na Yanga kutwaa ubingwa.

Msimu huu Kagera wanaonekana ni walewale wa kuionea Simba baada ya jana kuibuka na ushindi huo wa mabao 2-1 na kuwapunguza kazi mabingwa hao watetezi katika kuutetea ubingwa wao.

Kagera Sugar walikianza kipindi cha kwanza kwa kasi kubwa wakifanya shambulizi kali dakika ya tatu, Paul Ngwai, alikosa bao la wazi akiwa katika nafasi nzuri ambapo shuti lake lilishindwa kulenga lango.

Dakika ya nane, Aishi Manula, alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti kali la Ally Ramadhan, alilolipiga kwa njia ya faulo na kuwa kona ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.

Kassim Hamis, ndiye aliyewanyanyua mashabiki wa Kagera Sugar dakika ya 17 kwa shuti kali akiunganisha mpira wa krosi iliyochongwa kutoka winga ya kulia.

Manula alifanya tena kazi ya ziada dakika ya 22 mpira wa kona uliochongwa na David Luhende ambao ulikuwa unaelekea golini huku Ngwai akikosa tena bao dakika ya 25 ambapo shuti lake lilitoka nje.

Simba walijikuta wakifungwa bao la pili dakika ya 41 kupitia kwa Ramadhan Kapela kwa kichwa akiunganisha krosi iliyochongwa kutoka winga ya kulia kwa njia ya faulo na kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao hayo 2-0.

Katika kipindi hicho cha kwanza, Simba hawakufanya shambulizi lolote la maana huku kipa wa Kagera Sugar, akiwa kama yupo likizo kutokana na kazi nzuri iliyokuwa ikifanywa na walinzi wake wakiongozwa na mkongwe, Juma Nyoso.

Kipindi cha pili Simba ndio walioonekana kutawala mchezo wakifanya mashambulizi ya nguvu ambapo dakika ya 54, John Bocco, aliyeingia kuchukua nafasi ya Haruna Niyonzima, alikosa bao la wazi akiwa yeye na lango kutokana na krosi ya Erasto Nyoni, lakini mpira wake wa kichwa ukapaa juu.

Dakika ya 63, Emmanuel Okwi, alifunga bao kwa kushuti kali akipenyezewa pasi nzuri na Clatous Chama na kuwaamsha mashabiki wao waliokuwa wamekata tamaa.

Kama Paul Bukaba, angekuwa makini angeipatia Simba bao la pili dakika ya 72 akipiga kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na Chama, lakini ukagonga mwamba na kurudi uwanjani huku dakika ya 75, Chama akiachia shuti kali na kudakwa na kipa, Said Kipao.

Nusura Simba wasawazishe dakika ya mwisho ya mchezo baada ya Bocco kumpa pasi nzuri Okwi ambaye akiwa yeye na kipa alipiga kichwa dhaifu na mpira kuishia mikononi mwa kipa huyo na kuzifanya dakika 90 kumalizika kwa Kagera Sugar kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Kwa sasa Simba wanajiandaa kwenda jijini Mwanza kuwakabili Alliance na baadaye kucheza tena dhidi ya KCM michezo yote ikichezwa Uwanja wa CCM Kirumba na wakimaliza hapo wanafunga tena safari kuwafuata Biashara ya Mara kabla ya kwenda jijini Mbeya kucheza michezo miwili dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,235FollowersFollow
549,000SubscribersSubscribe

Latest Articles