25.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

SIMBA, YANGA ZITAMUDU GWARIDE LA KIJESHI?

NA ASHA KIGUNDULA-DAR ES SALAAM

MIAMBA ya soka nchini,timu za Simba na Yanga, leo zinashuka katika viwanja viwili tofauti kusaka pointi tatu, katika michezo yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku kila moja ikimwombea dua mbaya mwenzake apoteze.

Simba ambayo ni bingwa mtetezi wa ligi hiyo,itakuwa Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga kuumana na wenyeji wao Tanzania Prisons, huku Yanga ikiwa nyumbani dimba la Uhuru jijini Dar es Salaam kupepetana na Polisi Tanzania. Prisons inamilikiwa na Jeshi la Magereza Tanzania, huku Polisi Tanzania ikiwa chini ya Jeshi la Polisi hapa nchini.

Dua mbaya dhidi ya mwenzake kati ya timu hizo zenye upinzani wa jadi, zinatokana na nafasi zilizopo kwa sasa katika msimamo wa Ligi Kuu.

Katika msimamo wa Ligi Kuu, Simba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 13, baada ya kushuka dimbani mara tano, ikishinda mara nne na sare moja sawa na Yanga iliyoko nafasi ya tatu kutokana na kigezo cha wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa. 

Hii ina maana kwamba, mmoja wao akishinda mchezo wa leo na mwenzake kuanguka, itarefusha pengo kati yao katika msimamo wa ligi hiyo.

Kikosi cha Yanga kitashuka uwanjani kikiwa na Kocha Mkuu mpya, Mrundi, Cedric Kaze, ambaye alikabidhiwa mikoba ya kuinoa Ijumaa iliyopita, iliyoachwa na Zlatko Krmpotic aliyevurushwa.


Kiu ya mashabiki wa Yanga ni kuiona timu yao ikiwa na mabadiliko ya kiuchezaji leo, kutoka soka la butua butua na mabao ‘kiduchu’, hadi soka la pasi nyingi na mabao ya kutosha.

Yanga itajitupa dimba la Uhuru, ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union, katika mchezo wake uliopita uliochezwa Oktoba 3,Uwanja wa Mkapa ,Dar es Salaam.

Wageni wao Polisi Tanzania ina kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 na Gwambina, mchezo uliochezwa Oktoba 19, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Timu hizo zilipokutana msimu uliopita, hakuna aliyeibuka mbabe kwenye michezo yote miwili, zikianza kufungana mabao 3-3, Uwanja wa Mkapa kabla ya sare ya bao 1-1, Uwanja wa Ushirika, Moshi.

Simba inayofundishwa na Sven Vandenbroeck, itaingia uwanjani ikifahamu ugumu ambao huwa inaupata inapokutana na Tanzania Prisons.

Wekundu hao wataingia uwanjani wakitoka kuirarua JKT Tanzania mabao 4-0, mchezo uliochezwa Oktoba 4, Uwanja wa Mkapa.

Wapinzani wao Prisons wanakumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 na JKT Tanzania.

Sven atawakosa wachezaji wake watatu tegemezo katika mchezo huo Pascal Wawa, Meddie Kagere na Clatous Chama kutokana na sababu tofauti ikiwemo majeraha, hii itamlazimu kuweka tumaini kwa mpachika mabao wake Chris Mugalu.Mugalu amekuwa na kasi nuzri ya kufunga kwa wastani wa bao moja katika kila mchezo anaopata nafasi ya kucheza.

Timu hizo zilipokutana msimu uliopita, hakuna aliyevuna pointi tatu kwani michezo yote miwili ilimalizika kwa sare.

Wachezaji wa Prisons wataingia uwanjani wakiwa na  dhamira ya kuendelea kutokuwa wanyonge mbele ya Simba iwe wanacheza nyumbani au ugenini.

Wakizungumzia maandalizi ya mchezo huo,Sven alisema anahitaji pointi tatu, icha ya kutambua haitakuwa kazi nyepesi kutokana na uimara wa wapinzani wao.

Kocha Salum Mayanga wa Prisons alisema anajivunia kikosi imara chenye uwezo wa kupambana ili kupata matokeo ya ushindi, ingawa alikiri Simba ni timu nzuri hivyo hautakuwa mchezo mlaini.

Kwa upande wa Kaze wa Yanga alisema licha ya ugeni alionao Tanzania, ana amini kikosi chake hakitamwangusha leo, hiyo inatokana na maandalizi waliyofanya.

“Nina timu nzuri ya ushindi, nahitaji pointi tatu muhimu za mchezo huu na nyingine zinazofuata, kikosi changu kipo sawa,”alisema kocha huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,444FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles