26.9 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

‘Vyoo bora shuleni kuondoa magonjwa ya mlipuko’

NA SAMWEL MWANGA, MASWA

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Dk Fredrick Sagamiko, amesema ujenzi wa vyoo vya kisasa katika shule za msingi wilayani humo, utaondoa magonjwa ya mlipuko kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Dk Sagamiko alisema hayo mara baada ya kutembelea ujenzi wa vyoo vya shule saba za msingi wilayani humo ambao umekamilika kwa asilimia 95.

Alisema mradi huo unatekelezwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ni katika shule hizo kupitia programu ya Afya na Elimu Shuleni (SWASH) ambao umegharim Sh milioni 178.7 kwa matundu 125 ya vyoo.

“Huu ni mradi wa benki ya dunia lakini chini ya usimamizi wa ofisi ya Raisi, Tawala za Mikoa na Serikal za mitaa (Tamisemi)  mradi huo unatekelezwa katika shule saba ambazo zilikuwa na changamoto ya vyoo kwa wanafunzi pamoja na walimu,”alisema.

Mkurugenzi huyo amezitaja shule hizo na idadi ya matundu ya vyoo kwenye mabango kuwa ni Jija A (20), Malampaka (33), Mandang’ombe (7), Maswa (30),Mwabulimbu (15), Mwashegeshi (9) na Sangamwalugesha (11).

Alisema katika ujenzi huo kuna mambo ya msingi ambayo yamezingatiwa ambayo ni elimu, afya na maji kwa lengo la kutunza mazingira na kuwa msafi ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko yanayotokana na uchafu.

Alisema wamehakikisha vyoo hivyo vinakuwa na mfumo wa maji ili kuhakikisha mtumiaji mara baada ya kutumia anakuwa msafi na hivyo kujiepusha na aina yoyote ya magonjwa yanayotokana na uchafu.

Alisema ujenzi wa vyoo hivyo umechangiwa na wananchi wa maeneo husika huku akiwashukuru kwa kujitoa katika kushiriki na kuhakikisha vyoo hivyo vinakamilika huku vingine vikifikia hatua za mwisho.

“Nawashukuru sana wananchi wa Wilaya ya Maswa wamejitoa sanasana kupitia viongozi wa serikali za mitaa kwani wananchi wamechimba Mashimo na kuyajengea kwa nguvu zao pia mradi huo wa ujenzi wa vyoo pia umeleta fursa kubwa kwa wanavijiji kupitia kwa kuwapa ajira kwa kuwa mafundi wote walipatikana kwenye jamii inayozunguka shule zilizokuwa na mradi huo,”alisema.

Naye Ofisa Elimu Msingi wilaya ya Maswa, Saimon Bujimu alisema changamoto zinazozikabili maendeleo ya shule za msingi wilayani humo katika mradi huo ni ukosefu wa maji unazikumba shule hizo lakini kwa kushirikiana na  Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) wameweza kutatua changamoto hiyo.

“Suala la upatikanaji wa maji ya uhakika katika shule zetu ni changamoto kubwa ila kwa kushirikiana na Ruwasa tumeweza kutatua suala hilo na tutaendelea kufanya hivi ili kuhakikisha wanafunzi wetu wanasoma katika mazingira salama,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles