29.6 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Simba, Yanga hapa kazi tu

03NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

 

DAKIKA tisini za pambano kati ya Simba na Yanga leo ndilo litaamua mshindi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano hili la kwanza kwa msimu wa 2015/16, limesubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini kutokana na upinzani wa jadi uliopo miongoni mwa timu hizo mbili za Kariakoo, Dar es Salaam.

 

Timu zote mbili zitaingia kwenye pambano hilo zikitokea visiwani Zanzibar, ambako ziliweka kambi kwa ajili ya maandalizi.

Yanga iliweka kambi kisiwani Pemba wakati mahasimu wao, Simba waliweka kambi Unguja na hii yote ni katika kuhakikisha zinapata matokeo mazuri kwenye mchezo huo muhimu, ambao pengine ndiyo hasa unaweza kutoa mwelekeo katika mbio za kukalia usukani wa ligi hiyo msimu huu.

 

Timu itakayopoteza mchezo huo ndiyo itakuwa imeachwa na sare ya aina yoyote itatoa nafasi wapinzani wao wa pamoja Azam FC, hasa kama itafanikiwa kupata ushindi katika mechi yake ya kesho dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Azam Complex, uliopo Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Yanga iko kileleni mwa msimamo  ikiwa na pointi tisa, sawa na Simba na Azam, lakini Yanga ina mabao tisa, huku Simba ikiwa na mabao sita na Azam matano, huku timu zote zikiwa zimefungwa bao moja.

 

Kwa uwiano huo ni wazi kwamba yeyote atakayeteleza katika mechi ya leo atatoa nafasi ya kuachwa kwa pointi.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa mkali sana kutokana na hali ya vikosi vyote viwili hivi sasa, timu zote zinaonekana kuwa na safu nzuri ya ulinzi kwa kuwa zimeruhusu bao moja tu katika michezo mitatu, huku Yanga wakionekana kuwa na safu kali ya ushambuliaji kuliko ile ya Simba, ingawa Hamis Kiiza wa Simba ndiye anaonekana kuwa mshambuliaji mwenye shabaha zaidi kwa kuwa amepachika mabao matano.

 

Hata hivyo, washambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma  na Amissi Tambwe nao wametupia mabao matatu kila mmoja, hivyo katika mchezo wa leo vita kubwa itakuwa kwa washambuliaji hawa wa kigeni ambao bila shaka kila mmoja atataka kuwafurahisha mashabiki wa timu yake, huku akitaka kujiongezea idadi ya mabao katika mbio za kuwania kiatu cha ufungaji bora wa ligi.

Kwa upande mwingine inaweza kuwa mechi ya kisasi kwa Yanga kutaka kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 katika mechi ya ligi msimu uliopita, huku pia ikitaka kufuta uteja wa kufungwa mara kwa mara na Simba katika kipindi cha miaka miwili ya hivi karibuni.

 

Yanga haijaifunga Simba tangu Mei 18, 2013 iliposhinda mabao 2-0, yakifungwa na Didier Kavumbavu na Kiiza, wakati huo wakiichezea. Kiiza sasa atakuwa anakutana na timu yake ya zamani kwa mara ya kwanza tangu alipotemwa katika  usajili wa mwezi Julai na kocha Mbrazil, Marcio Maximo, ili kumpisha Geilson Santos Santana ‘Jaja’ ambaye aliletwa na kocha huyo.

 

Yanga imeifunga Simba mara moja tu katika michezo sita iliyopita ya ligi kuu na wataingia kwa mara ya saba wakitaka kupata ushindi na kufuta rekodi ya kufungwa kwenye Ligi Kuu.

Msimu wa 2012/13 timu hizo zilifungana bao 1-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, kisha Yanga ikaishinda Simba kwa mabao 2-0, Mei 18, 2013 na kutwaa ubingwa.

 

Msimu wa 2013/14 katika mchezo wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3, Yanga ikimaliza dakika 45 za kwanza wakiwa katika kiwango cha juu, huku wakiwa mbele kwa mabao 3-0, lakini dakika 45 za pili Simba nao wakaibuka na kusawazisha mabao yote matatu. Katika mchezo wa pili uliochezwa mwishoni mwa msimu huo ambao Azam FC ilitwaa ubingwa Yanga walisawazisha kupitia kwa Saimon Msuva katika dakika za majeruhi baada ya Simba kuongoza kwa bao la mapema.

Oktoba 2014, timu hizo zilitengeneza sare nne mfululizo katika ligi kuu baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana na mchezo wa pili wa Machi mwaka huu, Yanga ililala kwa bao 1-0 lililofungwa na Emmanuel Okwi kwa shuti la mbali.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles